Nov 18, 2018 02:46 UTC
  • Jumapili Novemba 18

Leo ni Jumapili tarehe 10 Mfungo Sita Rabiul-Awwal 1440 Hijiria, sawa na tarehe 18 Novemba 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka miaka 1485 iliyopita, alifariki dunia babu yake Mtume Muhammad (saw), Abdul Muttalib katika mji wa Makka. Mtukufu huyo alikuwa miongoni mwa wakuu wa kabila la Kuraish kabla ya kudhihiri Uislamu na alikuwa hodari mno katika fasihi ya lugha ya Kiarabu. Bwana Abdul Muttalib alikuwa msimamizi na mshika ufunguo wa Nyumba Tukufu ya al-Kaaba. Vilevile babu huyo wa Mtume alikuwa akitayarisha chakula na maji kwa ajili ya watu wanaozuru nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu na kazi hiyo aliirithi kutoka kwa baba yake. Aliheshimu mno mikataba na ahadi zake na kwa sababu hiyo alikuwa na ushawishi mkubwa baina ya watu. Miongoni mwa watoto wa mtukufu huyo ni Abdullah, baba yake Mtume wetu Muhammad (saw) na Abu Twalib, baba yake Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Abdul Muttalib

Siku kama ya leo miaka 1468 iliyopita, yaani sawa na tarehe 10 Rabiul Awwal miaka 28 kabla ya Hijra, Mtukufu Mtume Muhammad (saw) alimuoa Bibi Khadija binti Khuwailid (as). Bibi Khadija alikuwa mwanamke sharifu, mwenye imani na maarufu kwa ukarimu wake katika zama za ujahilia na alikuwa maarufu kwa lakabu ya "Twahira" kwa maana ya msafi na mtoharifu. Baada ya kufunga ndoa na Nabii Muhammad (saw), Bibi Khadija alikuwa msaidizi mkubwa na mwenzi wa mtukufu huyo katika hatua zote za maisha yake. Alisabilia kila kitu kwa ajili ya Uislamu na Mtume Muhammad (saw). Aidha Bibi Khadija (as) aliishi pamoja na Mtume kipindi cha miaka 25 na daima alikuwa mke mwema na mwenye kujitolea kwa mumewe Mtume Muhammad (saw) mbora wa walimwengu.

Siku kama ya leo miaka 231 iliyopita, Louis Daguerre mchoraji, mvumbuzi na mtaalamu wa elimu ya fizikia wa Kifaransa alifariki dunia. Mwaka 1789 mtaalamu huyo alifanikiwa kuvumbua mambo kadhaa. Miongoni mwa uvumbuzi muhimu wa Louis Daguerre ni ule wa mwaka 1839 ambapo alifanikiwa kuvumbua camera ya kupigia picha na kwa kutumia camera hiyo akapiga picha ya kwanza iliyokuwa ikionekana vizuri.

Louis Daguerre

Siku kama ya leo miaka 179 iliyopita, duru ya pili ya mapambano ya wananchi wa Algeria dhidi ya mkoloni Mfaransa ilianza kwa uongozi wa Abdul Qadir bin Muhyiddin. Mwaka 1830 Ufaransa iliishambulia kijeshi Algeria ikitaka kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Abdul Qadir akiwa na wapiganaji wake 50,000 alifanikiwa kukabiliana na mashambulio hayo hadi mwaka 1847. Hatimaye alishindwa na kuchukuliwa mateka.

Bendera ya Algeria

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita ulitiwa saini mkataba wa Mfereji wa Panama kati ya Marekani na Jamhuri ya Panama. Kwa mujibu wa mkataba huo mfereji huo ulikodishwa milele kwa Marekani mkabala wa Panama kupewa dola milioni 10 taslimu na dola laki mbili na nusu kila mwaka. Baadaye wananchi wa Panama walianzisha mapambano ya kupinga mkataba huo na hatimaye wakailazimisha Marekani kutazama upya kipengee cha kukodishwa milele mfereji huo. Kwa msingi huo mwaka 1978 Jimmy Carter na Jenerali Omar Efraín Torrijos viongozi wa wakati huo wa Marekani na Panama walitia saini mkataba mpya ambao kwa mujibu wake mfereji wa Panama ulirejeshwa chini ya mamlaka kamili ya nchi hiyo mwishoni mwa mwaka 1999.

Mfereji wa Panama

Siku kama ya leo Miaka 62 iliyopita yaani tarehe 18 Novemba mwaka 1956, nchi ya Morocco ilipatia uhuru. Kabla ya hapo ardhi hiyo ilikuwa chini ya tawala na mataifa mbalimbali. Hata hivyo kufuatia kuenea dini Tukufu ya Kiislamu katika maeneo mbalimbali duniani, yakiwemo maeneo ya kaskazini mwa Afrika, ardhi ya Morocco nayo ikawa miongoni mwa ardhi za utawala wa Kiislamu. Mwaka 1921 Ufaransa iliidhibiti Morocco hadi mwaka 1956 wakati nchi hiyo ilipojitangazia uhuru.

Bendera ya Morocco

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, alifariki dunia msomi na mwanafizikia wa Denmark, Niels Bohr, akiwa na umri wa miaka 82. Bohr alizaliwa mwaka 1885 na kuvutiwa mno na elimu ya hisabati. Msomi huyo alifanya uchunguzi na uhakiki mkubwa katika elimu hiyo. Niels Bohr pia alifanya uhakiki katika masuala ya atomu na mwaka 1945 akatunukiwa Tuzo ya Nobel katika medani ya fizikia kutokana na uvumbuzi wake katika masuala ya atomu.

Niels Bohr

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita kanali Abdul Salam Arif alishika hatamu za uongozi nchini Iraq baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu. Ikulu ya Rais na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq zilishambuliwa kwa mabomu na kupelekea kuuawa Abdul Karim Kasim aliyekuwa rais wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, Abdul Karim Kasim naye aliingia madarakani mwaka 1958 baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu yaliyohitimisha utawala wa Kifalme nchini humo.

Abdul Salam Arif

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita wiki mbili tu baada ya wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini kuteka ubalozi wa Marekani mjini Tehran ambao ulitambuliwa kuwa pango la ujasusi la nchi hiyo, mateka wanawake na weusi wenye asili ya Afrika waliokamatwa katika ubalozi huo waliachiwa huru kwa amri ya hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA). Ubalozi huo ulikuwa kituo cha ujasusi na kupanga njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa sababu hiyo wafanyakazi wake walishikiliwa mateka kama majasusi wa Marekani hapa nchini. Hata hivyo Imam Khomeini kwa sababu za kibinadamu na vilevile kwa kutilia maanani kwamba, wanawake na Wamarekani weusi wanadhulumiwa na kubaguliwa nchini kwao, alitoa amri waachiwe huru. Sehemu moja ya barua ya hayati Imam Khomeini kwa wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakiwashikilia mateka wamarekani hao inasema: 'Uislamu umetunga sheria makhsusi kwa ajili ya wanawake, na watu weusi kwa miaka mingi wamekuwa chini ya mashinikizo na dhulma za Marekani na pengine wamelazimishwa kuja Iran. Kwa msingi huo wapeni tahfifu iwapo haitathibitika kwamba wamefanya ujasusi." Mwisho wa kunukuu. Kwa utaratibu huo mateka 13 wa kike na wale wenye asili ya Afrika waliachiwa huru.

Kutekwa ubalozi wa Marekani na wanafunzi mjini Tehran

Na siku kama ya leo miaka miwili iliyopita aliwafiri dunia Bi Marzieh Hadidchi, mmoja wa wanamapambano wakubwa wa mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Bi Marzieh Hadidchi alizaliwa mwaka 1318 Hijiria Shamsia mjini Hamadan. Alianza kujishughulisha na masuala ya kisiasa yapata mwaka 1346 kwa kugawa vipeperushi na mwaka 1353 akatiwa mbaroni na maafisa wa Shirika la Intelijinsia na Usalama wa Taifa la Iran, maarufu kwa jina la SAVAK akiwa pamoja na binti yake kwa jina la Ridhwanah na kufungwa jela sambamba na kuteswa vikali. Wakati Imam Khomein (MA) alipowasili nchini Ufaransa sambamba na serikali ya nchi hiyo kutaka kumuwekea polisi mwanamke kwa ajili ya kumlinda, Imam alikataa jambo hilo. Kwa ajili hiyo Bi Marzieh Hadidchi alisafiri kwenda Ufaransa na kutokana na mafunzo maalumu aliyosomea, akawa mlinzi wa Imam Khomeini huko Nofel Loshato. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Bi Marzieh Hadidchi, alikuwa mmoja wa waasisi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) sambamba na kuwa mmoja wa makamanda wa jeshi hilo eneo la Hamadan, magharibi mwa nchi.

Bi Marzieh Hadidchi