Nov 19, 2018 09:15 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Nov 19

Haya ni baadhi ya matukio ya spoti yaliyogonga vichwa vya habari ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa....

Soka: Iran yainyuka Trinidad 1-0

Timu ya taifa soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliinyuka Trinidad and Tobago bao 1-0 katika mchuano wa kirafiki uliopigwa Alkhamisi usiku katika Uwanja Taifa wa Azadi hapa jijini Tehran. Bao hilo la kipekee la mchezo lilifungwa na strika wa Iran ambaye anaichezea Nottingham Forest, Karim Ansarifard, dakika tano baada ya kuanza kipindi cha pili. Mchezaji huyo nyota wa Iran hata hivyo alipoteza penati katika kipindi cha kwanza.

Mkufunzi wa Team Melli, Carlos Queiroz

 

Wachezaji hao wa mkufunzi Carlos Queiroz wanatazamiwa kuvaana na Venezeula katika mchezo mwingine wa kirafiki, utakaopingwa Jumanne hii mjini Doha, Qatar. Queiroz amelaumu uwanja wa Azadi uliokuwa umelowa maji na kusisitiza kuwa ndio uliofanya vijana wake wasipate mabao zaidi. Timu hiyo ya kandanda ya Iran inatumia michuano hiyo ya kirafiki kama sehemu ya kupasha misuli moto, kuelekea Kombe la Asia la AFC, mwaka ujao 2019. Iran ipo katika kundi moja na Yemen, Iraq na Vietnam. Iran ambayo imeorodheshwa kama timu ya kwanza barani Asia, itafungua kampeni zake za kutwaa Kombe la AFC kwa mchuano dhidi ya Yemen, unaotazamiwa kupigwa Januari 7 mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Taekwondo Poomsae; Iran yamaliza ya 4

Timu ya taifa ya taekwondo mtindo wa poomsae ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemalia katika nafasi ya nne kwenye mashindano ya mabingwa wa mchezo huo uliofanyika katika jiji la Taipei nchini China. Wanatekwondo hao wamezoa medali 3 za dhahabu, moja ya fedha na shaba 7.

Wanataekwondo wakipambana

 

Korea Kusini ndio waliobuka kidedea kwenye mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama World Taekwondo Poomsae Championships, huku mwenyeji China Taipei ikibuka ya pili, ikifuatiwa na Mexico iliyofunga orodha ya tatu bora. Duru ya mwaka huu ya mashindano hayo ya dunia ilianza Novemba 15 na kufunga pazia lake Jumapili ya Novemba 18.

Mbio za kutinga AFCON

Matumaini ya Taifa Stars ya Tanzania kufuzu katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 yameanza kufifia tena baada kutandikwa bao 1-0 na Lesotho Jumapili. Stars ilifungwa kutokana na uzembe wa mabeki, huku mashabiki wao wakisema wao kuchezea ugegeni mjini Maseru hakukulalisha wao kufungwa kizembe katika mchezo muhimu kama huo. Tanzania ilihitaji kuvuna alama tatu katika mchuano huo dhidi ya Lesotho ili kufuzu katika fainali hizo kwa mara ya kwanza toka mwaka 1980. Hata hivyo kitumbua chao kiliingia mchanga katika dakika ya 76 kwa goli la kichwa la Nkau Lerotholi.

Kombe la Afcon

 

Baada ya matokeo hayo, sasa Lesotho imefikisha alama 5 sawa na Tanzania huku Cape Verde akishuka mpaka mkiani kwa alama zao 4. Ili Tanzania wafuzu itabidi waifunge Uganda katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo utakaopigwa mwezi wa Machijijini Dar es Salaam na kuomba Cape Vede waifunge Lesotho. Waziri wa Michezo wa Tanzania, Dakta Harrison Mwakenyembe mbaye alikuwa uwanjani akifuatia mchuano huo, anasema matumaini yanagalipo.

Itakumbukwa kuwa, Rais wa Tanzania John Magufuli Oktoba 19 alikutana na timu hiyo ya taifa na kuichangia Shilingi milioni 50 kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Lesotho na kuwapa onyo hili.

Timu ya taifa ya soka ya Uganda imekuwa ya kwanza kutoka kanda ya Afrika Mashariki na Kati kujikatia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), zitakazochezwa mwaka ujao 2019 nchini Cameroon. Uganda imetinga fainali hizo baada ya kuibanjua Cape Verde bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Mandela Jijini Kampala. Bao la Uganda Cranes lilifungwa na mchezaji Kaddu Patrick katika kipindi cha pili cha mchezo huo na kuwanyayua toka vitini maelfu ya mashabiki waliokuwa wamefurika uwanjani hapo. Rais Yoweri Museveni ametumia ukurasa wake wa Twitter kuwamiminia salamu za pongezi Uganda Cranes na benchi la ufundi, hii ikiwa ni mara ya saba kwa Uganda kutinga fainali hizo. Uganda inaongoza Kundi L ikiwa na alama 13.

Matumaini ya Kenya kufuzu katika fainali hiyo, yameongezeka, baada ya FIFA kuendelea kuifungia Sierra Leone na mchuano wake wa kufuzu uliokuwa umepangwa kufanyika siku ya Jumapili kuahirishwa. Kenya inatarajia kurejea katika mashindani hayo baada ya miaka 15. Harambee Stars imepokea zawadi ya dola elfu 30 sawa na shilingi milioni 3 kutoka kwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko. Gavana Sonko ametoa fedha hizo baada ya kuiahidi Harambee Stars kuizawaidia iwapo itaishinda timu ya taifa ya Ethiopia. Harambee Stars iliibuka mshindi kwa mabao 3 kwa 0 kwa mechi iliyochezwa Jumatatu ya wiki iliyopita.  Moroco pia imetinga fainali hizi kwa mara ya 17 baada ya kuisasambua Malawi mabao 2-1 katika mechi ya Kundi B. Green Eagles ya Nigeria pia ina tiketi mkononi, licha ya kuambulia sare ya bao 1-1 ilipovaana na Afrika Kusini, huku Mali ikitinga fainali hizo baada ya kuiadhibu Gabon bao 1-0 na kukweni kileleni mwa Kundi C. Mwezi uliopita, timu za taifa za soka za Madagascar, Senegal, Tunisia na Misri zilijikatia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON, mwaka ujao nchini Cameroon. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa kisiwa cha Madagascar kutinga fainali hizo. 

UEFA Nations League; Uingereza yaizaba Croatia na kutinga nusu fainali

Timu ya taifa ya soka ya Uingereza siku ya Jumapili ilishuka dimbani kutoana udhia na Croatia, katika mchuano robo fainali ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya almaarufu UEFA Nations League, na kupata ushindi mnono. Uingereza ilitoka nyuma na kuisasambua Croatia mabao 2-1, katika mchuano wa kusisimua uliopigwa katika Uwanja wa Wimbley. Croatia ndio waliokuwa wa kwanza kucheka na nyavu za England, kutokana na bao la Andrej Kramaric la dakika ya 57.

Croatia ikipambana na Uingereza

 

Hata hivyo Uingereza wakiwa na hasira za kuchabangwa na Croatia katika mchuano muhimu wa Kombe la Dunia, ilikaza buti na kucheza kufa kupona. Mabao ya Harry Kane na Jesse Lingard katika dakika ya 77 na 85, mbali na kuifanya Uingereza itinge nusu fainali ya dimba hilo, lakini pia yaliifanya isishushwe daraja katika Kundi A4.

……………………TAMATI………………..