Nov 22, 2018 02:42 UTC
  • Alkhamisi tarehe 22,Novemba, 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 14 Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na 22 Novemba mwaka 2018.

Siku kama ya leo miaka 1376 iliyopita Yazid bin Muawiya aliangamia. Yazid alikuwa mtawala dhalimu na fasiki na alitawala kwa muda wa miaka mitatu na miezi tisa. Katika kipindi cha utawala wake Yazid mwana wa Muawiya alifanya kila aina ya jinai na alitambulikana kwa ufuska. Miongoni mwa jinai zake ni kumuua shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW yaani Imam Hussein bin Ali AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala huko Iraq mwaka 61 Hijria, kushambulia kinyama miji mitakatifu ya Makka na Madina na kubomoa nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani Al-Kaaba.

Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, alizaliwa Bi. Mary Ann Evans maarufu kwa jina la George Eliot, mwandishi wa riwaya na simulizi wa Uingereza. Akiwa mtoto mdogo Evans alipendelea zaidi kusoma vitabu, na taratibu akaingia katika fani ya uandishi. Aidha akiwa kijana Evans alikuwa na misimamo mikali ya dini ya Kikristo, hata hivyo misimamo hiyo ilipungua baadaye. Akiwa na umri wa miaka 30, aliandika kitabu cha ‘Maisha ya Nabii Issa-as’ huku akiandika vitabu mbalimbali vya riwaya simulizi na kutokea kupata umaarufu mkubwa katika karne ya 19.

Mary Ann Evans

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, kufuatia kujiri kwa Vita vya Pili vya Dunia, nchi ya Lebanon ilijipatia uhuru. Lebanon ilitoka katika udhibiti wa utawala wa Othmania mnamo mwaka 1918 Miladia na kudhibitiwa baadaye na Ufaransa. Mwaka 1923 Miladia Ufaransa iliikalia nchi hiyo kwa idhini ya Umoja wa Mataifa. Tangu wakati huo Lebanon ikaanza kushuhudia siasa za ukoloni wa Mfaransa vikiwemo vitendo vya ubaguzi na machafuko. Nchi hiyo ilijipatia uhuru wake mwaka 1943.

Bendera ya Lebanon

Katika siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, John F. Kennedy, rais wa wakati huo wa Marekani aliuawa na raia mmoja wa nchi hiyo akiwa ziarani katika mji wa Dallas huko katika jimbo la Texas. Kennedy alizaliwa mwaka 1917 na alikuwa mwakilishi wa bunge la Marekani kwa duru tatu kuanzia mwaka 1946 na duru moja alikuwa mwakilishi wa seneti ya nchi hiyo. Siku kadhaa baadaye Lee Harvey Oswald ambaye alimuua Kennedy naye pia aliuawa na mtu aliyejulikana kwa jina la Jack Ruby na polisi ya Marekani ilidai kuwa mtu huyo vilevile aliaga dunia baadaye akiwa jela kutokana na maradhi ya saratani.

John F. Kennedy

Na tarehe 22 Novemba miaka 51 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 242 kuhusu Palestina. Miongoni mwa vipengee vya azimio hilo ni udharura wa kuondoka askari wa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi zote za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu Juni mwaka 1967 katika vita vya Waarabu na Israel, kusimamishwa operesheni za kijeshi na kutatuliwa kadhia ya wakimbizi wa Palestina kwa njia ya uadilifu. Hata hivyo kutokana na himaya ya pande zote ya Marekani na nchi za Magharibi kwa utawala ghasibu wa Israel, utawala huo haramu umekataa kutekeleza azimio hilo.

Bendera ya Palestina