Dec 05, 2018 01:08 UTC
  • Jumatano tarehe 5 Disemba 2018

Leo ni Jumatano tarehe 27 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na Disemba 5 mwaka 2018.

Siku kama ya leo miaka 5 iliyopita, alifariki dunia shujaa wa mapambano ya ukombozi na kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela akiwa na umri wa miaka 95. Mandela alizaliwa mwaka 1918 na alitumia zaidi ya nusu ya umri wake akipambana na utawala wa kibaguzi nchini kwake. Utawala wa wazungu wabaguzi ulimfunga jela kwa kipindi cha miaka 27 hadi mfumo wa ubaguzi wa rangi ulipofutwa mwaka 1990. Mwaka 1994 wananchi wa Afrika Kusini walimchagua Mandela kuwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo. Mwaka 1993 Mandela alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel.

Mzee Nelson Mandela

Siku kama ya leo Miaka 50 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim

Tarehe 5 Disemba miaka 117 iliyopita alizaliwa Walt Disney shakhsiya mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto. Disney alizaliwa katika mji wa Chicago huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya udaktari katika sayansi ya uchoraji na uchongaji (Fine Art). Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni. Miongoni wma kazi muhimu za Walt Disney ni Snow White, The Seven Dwarfs, Polar Bears.

Walt Disney

Siku kama ya leo miaka 144 iliyopita, Iran ilijiunga na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Jitihada za awali za Iran kutaka kujiunga na shirika hilo zinarejea nyuma katika kipindi cha utawala wa Mfalme Nassereddin Shah Qajar. Katika kipindi cha utawala wake, Disemba 1874 Iran iliukubali mkataba uliopasishwa Geneva Uswisi, lakini licha ya kupita miaka kumi tangu isaini mkataba huo, utawala wake haukuchukua hatua yoyote ile ya kuasisi taasisi au jumuiya ambayo itatekeleza hati ya mkataba huo hapa Iran.

Katika siku kama ya leo miaka 148 iliyopita, aliaga dunia Alexander Dumas mwandishi mtajika wa Kifaransa. Mwandishi huyo ambaye ni mashuhuri pia kwa jina la Dumas Baba baada ya kumaliza masomo yake aliajiriwa katika ofisi moja ya kiwanda kama katibu kutokana na kuwa na hati nzuri.

Alexander Dumas

Tarehe 27 Rabiul Awwal miaka 1077 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu, Abul Alaa al Maarry katika mji wa Maarrat al-Nu'man karibu na mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria. Abul Alaa alifariki dunia mwaka 449 Hijria katika mji huo huo ulioko umbali wa kilomita 33 kusini mwa Idlib. Baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."

Abul Alaa al Maarry

 

Tags