Dec 19, 2018 10:20 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 788. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 35 ya Fatir, katika darsa hii tutaanza kuizungumzia sura ya 36 ya Ya-Sin. Sura hii ambayo imeteremshwa Makka imepewa jina hili kutokana na aya yake ya mwanzo ambayo ni ya herufi za mkato. Surat Ya-Sin ina aya 83. Sura hii inazungumzia zaidi masuala ya kiitikadi. Katika baadhi ya aya zake, Surat Ya-Sin imeashiria pia adhama ya Mwenyezi Mungu SW, Muumba wa ulimwengu. Katika sehemu nyingine ya aya za sura hii, yamezungumziwa pia masuala kuhusu maadi, yaani marejeo na kufufuliwa viumbe, masuali na majibu katika mahakama ya Siku ya Kiyama pamoja na sifa maalumu za Pepo na Moto. Surat Ya-Sin imetajwa katika hadithi kuwa ni moyo wa Qur'ani. Baada ya maelezo hayo machache, sasa tunaianza darsa yetu ambayo kwa leo itazungumzia aya nne za mwanzo za sura hiyo ambazo zinasema:

يس

Ya-Sin

وَالْقُرْآنِ الْحَكِيمِ

Naapa kwa Qur'ani yenye hikima!

إِنَّكَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ

Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa,

عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

Juu ya Njia Iliyo Nyooka.

Kuhusu herufi za mkato tumeshawahi kulielezea suala hilo hapo kabla katika sura kadhaa zikiwemo za Al-Baqarah na Aal Imran. Suratul Baqarah, Suratu Aal Imran na baadhi ya sura nyingine za Qur'ani zinaanza kwa herufi hizi za mkato. Herufi hizi si maneno yenye kujitegemea. Kama yalivyo maneno ya ufupisho mathalani ya mashirika na taasisi ambayo hubainishwa kwa njia ya ufupisho kwa kutumia herufi zao za mwanzo, herufi hizi za mkato, nazo pia ni alama na ishara za maneno ambayo hakika yake haiko wazi kwetu sisi. Herufi hizi ni miongoni mwa mafumbo ya Qur'ani, ambayo ni Bwana Mtume SAW na Maimamu  maasumu (AS) wa kizazi chake peke yao ndio wanaoelewa maana yake halisi; na hakika yao itabainika na kuwa wazi zaidi atakapodhihiri Imam wa Zama, Imam Mahdi (AS). Kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, herufi ya mkato ya "Ya-Sin" ni moja ya majina ya Bwana Mtume Muhammad SAW; na hoja iliyothibitisha hilo ni aya zinazofuatia ambazo zinamhutubu moja kwa moja Mtume huyo wa Allah. Kama tulivyoeleza hapo kabla pia, kwa kawaida baada ya herufi ya mkato huwa linafuatia jina la Qur'ani na sifa zake. Sura hii, nayo pia  imetilia mkazo sifa maalumu ya utoaji mafunzo ya hekima iliyonayo Qur'ani na kuliapia suala hilo. Kitabu ambacho humfungulia mtu milango ya hekima na kumuelekeza kwenye njia sahihi na iliyonyooka. Kwa kawaida viapo vya Qur'ani huwa ni kwa ajili ya kubainisha adhama ya kitu kinachoapiwa, na si kwamba Allah SW anahitaji kuapa ili kuthibitisha ukweli wa analolieleza. Aya hizi tulizosoma za Suratu Ya-Sin zimeelezea kwa uzuri uhusiano uliopo kati ya risala ya Bwana Mtume SAW na kuteremka Qur'ani na kumwambia mtukufu huyo: Qur'ani ni hoja madhubuti zaidi ya kuthibitisha Utume wako, kwa sababu ni muujiza wa Allah ambao, hakuna yeyote awezaye kuleta kilicho mfano wake; na wewe kama walivyokuwa Mitume waliotangulia una jukumu la kuwaelekeza watu kwenye uongofu. Mwenyezi Mungu anashuhudia kwamba wewe uko kwenye Siratul-Mustaqim, yaani njia iliyonyooka, pia u mwenye kuijua njia hiyo sawasawa na unayatambua mambo yanayomkengeusha mtu na njia hiyo. Kwa kuzingatia muhtawa wa aya ya tatu ya Surat Ya-Sin, Bwana Mtume Muhammad SAW, sio tu yuko kwenye njia iliyonyooka, lakini kimsingi hasa ana udiriki kamili wa njia hiyo. Ni wazi kwamba mtu anayetaka kuwalingania watu kufuata njia hiyo inapasa yeye mwenyewe awe mfano wa kivitendo wa ufuataji njia iliyonyooka na pia inatakiwa awe na uwezo wa kuwaelekeza watu kwa namna sahihi kufuata njia hiyo na kuwafanya wadumu katika ufuataji wao. Inapasa tuzingatie pia kwamba kuwa njia ya Allah ni njia iliyonyooka hakumaanishi kuwa ni kitu chepesi na rahisi kuweza kukifuata; sivyo hivyo abadani! Tusidhani kwamba njia hiyo haina vigingi, mashimo wala misukosuko yoyote. Madhumuni ya njia iliyonyooka ni njia sahihi kwa ajili ya kufika kule kulikokusudiwa mkabala na njia nyingine kadhaa zilizopinda na za upotofu. Japokuwa njia hizo kidhahiri huwa hazioneshi kuwa na mipindo na vichochoro lakini ukweli ni kwamba haziwezi kumfikisha mtu alikokusudiwa kufika. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Qur’ani ni kitabu makini na madhubuti cha hekima na chenye mafunzo ya hekima. Moja ya hali ya kimiujiza ya Qur’ani ni mafunzo yake ya hekima katika masuala yote ya mtu binafsi, familia na jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mafundisho yenye kumjenga mtu na ya uongofu ya Qur'ani yanahitaji mwalimu kama Bwana Mtume SAW, ambaye atayafundisha na vilevile yeye mwenyewe ni kigezo na mfano wa kivitendo wa mafundisho hayo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika kila Sala huwa tunamwomba Allah atuongoze kwenye njia iliyonyooka. Na Yeye Mola amemtaja Mtume wake kuwa ni mfano na kigezo cha njia iliyonyooka; kwa hivyo inatupasa kuielewa kwa usahihi sira na mwenendo wa mtukufu huyo na kufanya amali zetu kwa mujibu wa sira hiyo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 788 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuongoze njia iliyonyooka. Njia ya wale aliowaneemesha juu yao. Si ya wale walioghadhibikiwa wala ya wale waliopotea. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.