Sura ya Ya-Sin, aya ya 5-9 (Darsa ya 789)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.
Hii ni darsa ya 789 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 5 na ya 6 ambazo zinasema:
تَنزِيلَ الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ
Ni uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
لِتُنذِرَ قَوْمًا مَّا أُنذِرَ آبَاؤُهُمْ فَهُمْ غَافِلُونَ
Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa, basi wao wamekuwa wenye kughafilika.
Aya tulizosoma katika darsa iliyopita zilizungumzia sifa ya Qur'ani tukufu kuwa ni kitabu chenye mafunzo ya hikima, kilicho imara na chenye adhama. Aya hizi tulizosoma hivi punde kwanza zinasema: Qur'ani ni maneno ya Allah, si maneno ya Bwana Mtume, japokuwa yametamkwa kupitia kinywa cha mtukufu huyo, lakini yanatafautiana na maneno mengine ya mbora huyo wa viumbe. Kama tutarejelea Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW na vitabu vilivyokusanya hadithi hizo tutabaini kuwa tuni au lahani na mtindo wa ubainishaji uliotumika kwenye Hadithi za Bwana Mtume ni tofauti na ule wa Qur'ani. Bila shaka mtu mwenye uelewa mdogo tu wa lugha ya Kiarabu anaweza kuhisi kwa uwazi tofauti hiyo. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Qur'ani imeteremshwa kwa ajili ya kuwaonya watu na kuwapa indhari ili waondokane na mghafala na kupata uelewa wa hakika ya ulimwengu wa uumbaji. Hakika ambazo zina uhusiano na hatima ya mwanadamu; na kutokuwa na uelewa nazo kutamfanya mwanadamu aione dunia tu na kughafilika na akhera ambayo ndiyo makazi ya maisha ya milele. Kisha aya zinabainisha umuhimu wa risala ya Bwana Mtume SAW katika ardhi ya Bara Arabu kwa kusema: hapo kabla hakuwahi kubaathiwa na kupewa Utume katika eneo hili Nabii ambaye asili yake inatokana na Waarabu; na watu wake walikosa neema ya kufikiwa na Mtume ambaye ni Ulul-azm. Tab'an kwa mujibu wa aya nyingine za Qur'ani, katika jamii hiyo, siku zote wametokea watu ambao wamefanya kazi ya kuwafikishia maonyo na indhari watu wa jamii hiyo na kutimiza dhima ya kuwabainishia haki, hata hivyo hawakuwa miongoni mwa manabii mashuhuri, kama ambavyo katika kipindi cha tangu alipokuja Nabii Isa (AS) hadi alipodhihiri Bwana Mtume Muhammad SAW hakuwahi kutumwa kwa watu hao Mtume yeyote miongoni mwa manabii ambao ni Ulul-azm. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Allah SW amepambika kwa sifa zote za ukamilifu; Yeye ni Mwenye nguvu na Uwezo na pia ni Mrehemevu na Mwenye huruma. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa maonyo na indhari zinatolewa kuwafanya watu wazinduke na kutoka kwenye usingizi wa mghafala ni utaratibu uliowekwa na Allah na ni moja ya majukumu makuu ya Mitume.
Ifuatayo sasa ni aya ya 7 ya sura yetu ya Ya-Sin ambayo inasema:
لَقَدْ حَقَّ الْقَوْلُ عَلَىٰ أَكْثَرِهِمْ فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ
Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini.
Aya hii inaendeleza maudhui iliyozungumziwa na aya zilizotangulia zilizoeleza kwamba Mitume walitumwa kwa lengo la kuondoa utandu wa mghafala na kujisahau uliogubika nyoyo za watu na kubainisha kuwa: watu wengi huwa hawayajali maonyo na indhari za Mitume na kuamua kutowaamini. Ni wazi kwamba watu kama hao watafikwa na adhabu tu Siku ya Kiyama. Bila shaka watu watakaostahiki kupata adhabu Siku ya Kiyama ni wale ambao hawakutubia hadi mwisho wa uhai wao na hawakuwa tayari kuacha upotofu na kufuata njia ya uongofu au wale waliokuwa vinara wa shirki na ukafiri ambao waliwapotosha watu wengi na kuwafanya wasifuate njia ya uongofu. Lakini kama kabla ya kufikwa na ishara za mauti, mtu atajuta na kutubia kwa kuacha njia ya upotofu au matendo maovu aliyokuwa akifanya na kuomba maghufira kwa Allah atapata msamaha na rehma zake Mola. Allah atamuokoa mtu kama huyo na hilaki ya kuselelea kwenye Moto wa Jahanamu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kipimo katika suala la kushikamana na dini si wingi au uchache wa watu. Hata kama akthari ya watu duniani wataiacha dini ya Mwenyezi Mungu hiyo si hoja kwamba wanayoyafanya ni sahihi. Haipasi kwa waumini walio wachache kuingiwa na shaka juu ya njia ya haki wanayofuata au kuvunjika moyo na kukata tamaa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kughafilika na hakika za masuala ya ghaibu humuelekeza mtu kwenye ukafiri na kuwa na inadi na uadui na haki.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 8 na ya 9 ambazo zinasema:
إِنَّا جَعَلْنَا فِي أَعْنَاقِهِمْ أَغْلَالًا فَهِيَ إِلَى الْأَذْقَانِ فَهُم مُّقْمَحُونَ
Hakika tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juu tu.
وَجَعَلْنَا مِن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ سَدًّا وَمِنْ خَلْفِهِمْ سَدًّا فَأَغْشَيْنَاهُمْ فَهُمْ لَا يُبْصِرُونَ
Na tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho yao; kwa hivyo hawaoni.
Aya hizi za 8 na 9 zinaeleza kuhusu adhabu watakayopata makafiri duniani na akhera. Kuhusu adhabu ya Siku ya Kiyama zinayataja makongwa na minyororo watakayozongwa nayo watu wa motoni vichwani na shingoni mwao na kuwafanya washindwe hata kutikisika; ambapo mbali na kuwaunguza itakuwa na hali maalumu pia ya kuwadunisha na kuwadhalilisha. Hao ni watu ambao, hapa duniani hawakuwa tayari kuiona haki na hakika za mbele na nyuma yao, kwa kushindwa kumtambua Mwenyezi Mungu ambaye ndiye chimbuko na asili ya ulimwengu wala kuiamini na kuikubali akhera ambako ndiko iliko hatima ya amali na matendo yao. Kwa sababu hiyo huko akhera pia watafufuliwa vivyo hivyo kwa kudhihiri hakika ya upofu wa nyoyo zao waliokuwa nao hapa duniani. Ukweli ni kwamba Siku ya Kiyama ni siku ya kudhihiri hakika ya amali za watu kwa sura nyengine. Bila shaka dhahiri ya amali hapa duniani inakuwa ya namna ambayo mtu mwenyewe si hasha hata asiweze kuiona hakika ya uchafu na ubaya wake, lakini kwa kuwa Siku ya Kiyama watu watafufuliwa kwa sura ya batini zao, upofu wa kidhahiri wa nyoyo zao na wa kutoijali kwao haki na hakika ya mambo hapa duniani, utadhihiri siku hiyo katika hali ya upofu halisi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba makongwa na minyororo ya Siku ya Kiyama, kwa hakika ni minyororo waliyojifunga nayo makafiri duniani mikononi na miguuni mwao. Wao wenyewe wanadhani kwamba wako huru, lakini ukweli ni kwamba ni mateka na wafungwa wa hawaa na matamanio ya nafsi zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wanachowaza makafiri ni juu ya leo yao tu na jinsi ya kujistarehesha na raha za kupita za dunia. Wameifumbia macho nyuma na mbele yao na utando umegubika macho yao, kwa hivyo hawawezi kuona hakika ya mambo. Hawapati ibra na mafunzo kwa yaliyopita wala hawatafakari juu ya hatima na mwisho wao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 789 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutupa taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.