Sura ya Ya-Sin, aya ya 10-12 (Darsa ya 790)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 790 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 10 na ya 11 ambazo zinasema:
وَسَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَأَنذَرْتَهُمْ أَمْ لَمْ تُنذِرْهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ
Ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.
إِنَّمَا تُنذِرُ مَنِ اتَّبَعَ الذِّكْرَ وَخَشِيَ الرَّحْمَـٰنَ بِالْغَيْبِ ۖ فَبَشِّرْهُ بِمَغْفِرَةٍ وَأَجْرٍ كَرِيمٍ
Hakika wewe unamwonya yule tu anayefuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo maghufira na ujira mwema.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoeleza kuhusu adhabu kali watakayopata makafiri na washirikina Siku ya Kiyama. Aya hizi tulizosoma zinasema, sababu ya kufikwa na adhabu hiyo ni ukaidi na inadi walioyifanyia haki kwa namna ambayo hawakuwa tayari hata kuyasikiliza maneno ya Bwana Mtume Muhammad SAW na hoja wadhiha za mantiki alizokuwa akiwapa; na kama waliyasikiliza basi wala hawakuyajali, ikawa kama hawakuyasikia. Kwa hivyo hakuna tofauti yoyote kwao wao kama Bwana Mtume atawapa indhari au la, kwa sababu wameshajiamulia kutoiamini haki. Nyoyo zao ni mithili ya ardhi kavu na yabisi ambayo maji ya mvua hayawezi kupenya ndani yake. Na tab'an hakuna mmea wowote utakaoota na kukua kwenye ardhi kama hiyo. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: onyo na indhari huwa na taathira na faida kwa mtu aliye tayari kusikiliza mawaidha na ukumbusho na kuufuata. Aya zote za Qur'ani tukufu zinatoa ukumbusho; na yeye Bwana Mtume SAW pia ametajwa katika aya kadhaa kuwa ni "mudhakkir" yaani mkumbushaji. Kimsingi hasa, mafundisho na hakika nyingi za dini zimejikita ndani ya fitra na hali ya maumbile aliyojaaliwa mja na Mola wake, lakini sababu mbalimbali humfanya mtu aghafilike nazo. Ili kuuondoa utandu huo wa mghafala katika nafsi ya mtu na kumkumbusha ule utambuzi wa kifikra aliojaaliwa kuwa nao, Allah SW amewatuma Mitume na vitabu vya mbinguni ili kila mtu anayetaka kuijua haki na hakika aweze kuongoka, na kuokoka na njia ya upotofu. Ni wazi kwamba mtu yeyote mwenye kuuzingatia na kuutafakari ujumbe wa Mitume wa Mwenyezi Mungu huwa anamzingatia Mola wake katika hali zote, hadharani na katika faragha; na mara chache huteleza kwa kufanya makosa na madhambi. Kwa sababu hiyo, muamala wa Allah kwa mtu kama huyo huwa ni wa maghufira na ukarimu. Huyasitiri makosa yake na kumsamehe na humpa malipo mema kwa amali zake njema alizofanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutimiza dhima kwa watu wote ni jambo la lazima. Lakini uwezekano wa kuathiriwa na wito wa haki upo kwa wale tu walio tayari kuyakubali mawaidha na maonyo na wenye kiu ya kuifuata hakika na haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Qur'ani ni kitabu cha ukumbusho ili kuizindua fitra na maumbile ya mwanadamu na kuyavua na mambo yanayoighafilisha fitra hiyo na haki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba alama ya imani ya kweli kwa Mwenyezi Mungu SW ni kumcha Yeye Mola kwa siri na kwa dhahiri; na si kwa dhahiri pekee mbele ya macho ya watu. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kuwa watu wanaoyajali maonyo na indhari za Mitume watarehemewa na kubashiriwa Pepo ya Allah.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 12 ya sura yetu ya Ya-Sin ambayo inasema:
إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ ۚ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ
Hakika Sisi tunahuisha wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na athari zao. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha.
Moja ya maonyo muhimu zaidi ya Mitume na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo ni kuhusu Kiyama na kuhesabiwa amali za waja. Hii ikiwa na maana kwamba baada ya mtu kufa, atafufuliwa katika ulimwengu mwengine ambako atasailiwa na kuulizwa kuhusu yote aliyoyafanya katika ulimwengu huu. Ni wazi kwamba ili watu waweze kuhudhurishwa kwenye mahakama ya Siku ya Kiyama inabidi amali zao zote walizofanya hapa duniani zihifadhiwe na kwenda kuhukumiwa kulingana na amali zao hizo. Kimsingi ni kwamba kinachofanywa katika mifumo ya mahakama na uendeshaji kesi ya hapa duniani ni kutoa adhabu tu kwa wahalifu; tena basi, kwa kiwango cha kosa lililofanywa na athari zake zinazoonekana mbele ya macho ya watu. Lakini mahakama ya Siku ya Kiyama inazingatia matendo mema ya mtu na kumlipa thawabu, na pia matendo maovu aliyofanya na kumlipa adhabu. Si hayo tu, mbali na athari za wakati uleule wa dhambi aliyofanya mtu, hata athari zilizoendelea kuwepo kwa makumi au hata mamia ya miaka baada ya kufa kwake, nazo pia zitakuwa na malipo. Chukulia mfano wa mtu aliyeua. Inachofanya mahakama ni kutoa hukumu ya kosa lake la kuua tu, ilhali mke na watoto wa aliyeuliwa huweza kwa miaka na miaka kutaabika na kukumbwa na matatizo kadhaa wa kadhaa ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni baada ya kuuawa kwake. Katika mfumo wa mahakama uliopo duniani matatizo hayo hayazingatiwi katika uendeshaji kesi na wala hakuna adhabu inayotolewa kwa muuaji kutokana na matatizo na masaibu yatakayoipata baadaye familia ya mtu aliyeuliwa. Lakini katika mahakama ya uadilifu ya Allah Jalla Jalaluh yanazingatiwa pia matokeo na athari zilizoendelea kwa muda mrefu baadaye kutokana na amali za mtu. Kisha aya inatilia mkazo kuhifadhiwa kwa amali za watu na kueleza kwamba: mambo yote yanahifadhiwa kwenye Lawhun-Mahfudh, yaani loho inayohifadhi kila kitu pasina kusahaulika chochote. Kwa kuwa Siku ya Kiyama, hiyo Lawahun-Mahfudh itakuwa ndiyo mwongozo na dira ya kufuatwa na malaika wote katika kusimamia utoaji malipo ya thawabu na adhabu kwa watu na ndiyo itakayokuwa mizani ya kupimia amali zao njema na mbaya, katika aya hii ya 12 ya Surat Ya-Sin imetajwa kuwa ni "Imamu" na kiongozi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, daftari la amali za mtu linaendelea kubaki wazi baada ya kufa kwake mpaka kitakaposimama Kiyama. Hata athari za matendo yake, nazo pia zitaendelea kuhifadhiwa kwenye daftari hilo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa katika utamaduni wa Kiislamu mtu habebi dhima na mas-ulia ya amali anazofanya tu lakini atawajibika pia Siku ya Kiyama kutokana na athari zilizosababishwa na amali na matendo yake katika familia na jamii kwa jumla. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba mahakama ya Allah Siku ya Kiyama haitokuwa ya kuhukumu mambo kwa dhana na ukisiaji, bali itawahukumu waja kwa kutegemea ushahidi makini ulioandikwa kwa namna inayodhihirisha na kushuhudisha kila kitu pasi na kuwa na kasoro wala nuksani yoyote. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 790 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa katika wale ambao mizani za amali zao njema zitakuwa nzito Siku ya Kiyama na si wale ambao mizani za amali zao njema zitakuwa nyepesi. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.