Dec 22, 2018 07:48 UTC
  • Na alipotangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.
    Na alipotangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia maudhui ya ‘kushukuru’

 

Kama mnakumbuka tulisema kuwa, kuonyesha shukurani maana yake ni kushukuru na kuthamini kwa ulimi na vitendo neema za Mwenyezi Mungu. Wasomi na wanazuoni wa elimu ya Akhlaq wameigawa shukurani au kushukuru katika sehemu tatu za ulimi, moyo na vitendo. Tulikunukulieni hadithi kutoka kwa Imam Jafar bin Muhammad al-Swadiq inayosema: Shukurani ya neema ni kujiepusha na dhambi. Tulieleza pia kwamba, baadhi ya neema za Mwenyezi Mungu humfikia mja kupitia watu wengine. Katika mazingira kama haya, mja mbali na kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye mtoaji wa asili wa neema hiyo, anapaswa kumshukuru pia mtu ambaye alikuwa wenzo wa neema hiyo kumfikia. Tuliashiria pia madhara ya kukufuru neema za Allah ambayo ni kupata adhabu kali ya Allah. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 136 ya mfululizo huu kitaendeea na maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo.

 

Nabii Suleiman (as) alipewa na Mwenyezi Mungu nguvu na ufalme wa ulimwengu mzima. Nabii huyo wa Allah alikuwa alitukuzwa na kufunzwa lugha za wanyama na kupambanuliwa ishara za lugha za wanyama. Licha ya kuwa wanadamu wengi wanapopata nguvu na utajiri hughafilika na kumsahau Allah ambaye kimsingi ndiye mmiliki wa asili wa neema, lakini Nabii Suleiman AS, wakati aliporuzukiwa na Mwenyezi Mungu neema za kimaada na kimaanawi, alimshukuru Mola Muumba na kuthamani neema hizo. Aya ya 19 ya Surat inasema:

Basi (Sulaiman) akatabasamu akacheka kwa neno hili, na akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nipate kutenda mema uyapendayo, na uniingize kwa rehema yako katika waja wako wema.

Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi

 

Aidha katika aya ya 39 Mwenyezi Mungu anasema:

Akasema mwenye ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni katika fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu.

Kadhalika Mwenyezi Mungu anasema katika sura hiyo hiyo aya za 15 na 16 kwamba: Na hakika tuliwapa Daudi na Sulaiman ilimu, na wakasema: Alhamdu Lillahi, Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu aliyetufadhilisha kuliko wengi katika waja wake Waumini. Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri.

 

Wapenzi wawasikilizaji aya tulizotangulia kuzisoma ni baadhi tu ya aya nyingi zinazoonyesha jinsi waja wema wa Mwenyezi Mungu walivyothamini na kuonyesha kushukuru neema walizopatiwa Mola Muumba.

Bwana Mtume Muhammad SAW ambaye ndiye mja aliyetukuka zaidi kwa sifa na fadhila za kimaadili na alifikia upeo wa juu kabisa wa kuonyesha ushukurivu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Imam Muhammad Baqir AS amenukuliwa akisema: Siku moja mmoja wa wakeze Bwana Mtume SAW alimwambia Mtukufu huyo, Mwenyezi Mungu ameshakurehemu kwa rehma Zake kwa amali zako zote zilizotangulia na zitakazofuatia, kwa nini basi unajihangaisha kufanya ibada kiasi hiki? Mtukufu Mtume SAW akajibu kwa kusema: Basi siwezi mimi kuwa mja mshukurivu?

Kama ambavyo tunafahamu kuwa, kila jambo jema au baya lina athari na matokeo yake mabaya au mazuri, kushukuru neema za Mwenyezi Mungu kuna matunda na athari zake. Moja ya matunda hayo ni kukamilika na kuendelea na kuongezwa neema mja aliyeshukuru.

Aya ya 7 ya Surat Ibrahim inasema:

Na alipotangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.

Inanukuliwa katika hadithi kwamba, Is’haq bin Ammar amesimulia kuwa, siku moja Imam Ja’afar bin Muhammad Swadiq (AS) alinitazama na kuniambia, Ewe Is’haq, kila wakati Allah anapomtunuku na kumpatia neema mja wake na mja huyo akatambua thamani ya neema hiyo na kisha akamshukuru Mwenyezi Mungu wazi wazi, wakati bado hajamaliza kumshukuru Muumba, hutolewa amri na Allah ya kuongezewa neema mja huyo.

Kwa hakika hadithi hii inaonyesha ni kwa namna gani, kushukuru neema kulivyokuwa na taathira kubwa mno katika kuongezewa ujazi na neema mja mwenye kumshukuru Allah kutokana na kupatiwa neema.

 

Wapenzi wasikilizaji, akili, uzima wa afya, uongofu, imani na uwepo wote wa mwanadamu katika ulimwengu huu ni ujazi na neema za Mwenyezi Mungu ambazo wanadamu tunapaswa kutoa shukurani na kumshukuru Mola Muumba kwa kututunuku neema hizi.  Hata hivyo nguvu ya kushukuru bila kujali ni kwa moyo, ulimi au kwa vitendo nayo ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa maana kwamba, hata tawfiki ya kuweza kushukuru nayo ni neema kutoka kwa Allah.

Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.

Imam Ali bin Hussein al-Sajjad AS, Imam wa 4 wa mlolongo wa Maimamu 12 kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume SAW anaashiria jambo hili katika maneno yake mazuri mno kwa kusema:

Ewe Mola wangu! Vipi nitatekeleza haki yako ya kukushukuru, ilihali hii hii shukurani yangu, inahitajia kushukuru? Na kila mara ninaposema "nakushukuru" inakuwa kwangu ni wajibu kusema na kutoa shukrani kutokana na kunipatia tawfiki hii ya kuweza kukushukuru.

Ni kutokana na sababu hii ndio maana, shakhsia wakubwa wa dini wanasema kuwa, kushukuru neema za Allah njia yake ni moja tu nayo ni kuonyesha udhaifu na kutokuwa na uwezo wa kushukuru neema za Mola Muumba.

Siku moja Imam Sajjad AS aliulizwa: Pamoja na kuwa wewe unatokana na kizazi cha Bwana Mtume SAW na mjukuu wake, kwa nini unapata tabu na kujipa masaibu yote haya kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu?

Imam Sajjad AS aliashiria ufanyaji ibada mgumu na wa hali ya juu wa Bwana Mtume SAW na kusema: Swali hili hili ambalo nyinyi mnauliza, aliulizwa mbora wa viumbe Mtume Muhammad SAW na mtukufu huyo alijibu kwa kusema: Ninaapa kwa Mola! Endapo viungo vyangu vyote vitakatwa vipande vipande, na machozi kutoka katika macho yangu yakatiririka katika kifua changu, katu siwezi kutoa shukurani ndogo kwa neema nyingi alizonipatia Mwenyezi Mungu.

Hapana shaka kuwa, Mwenyezi Mungu ni Mkwasi na wala si mhitaji wa shukurani za binadamu kwa sababu ya ujazi na neema zisizohesabika alizowajaalia na kuwapatia wanadamu. Kwa msingi huo basi, ametuamrisha tuwe washukurivu kwa sababu, ya taathira njema ya kufanya hivyo katika maisha yetu wenyewe ambapo moja ya taathira hizo nzuri ni kuongezewa neema.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa, jiungeni nasi wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Ahsanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini…….

Na Salum Bendera.