Jumapili 23 Disemba
Leo ni Jumapili tarehe 15 Rabiul Thani 1440 Hijria sawa na Disemba 23, 2018 Milaadia.
Katika siku kama ya leo miaka 93 iliyopita mji wa Jeddah ulitekwa na Ibn Saud na kwa msingi huo utawala wa Ukoo wa Hashemi ukahitimishwa mjini humo. Baada ya kusambaratishwa uasi wa Mawahhabi katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 Miladia, kundi hilo liliendelea kuwachochea wengine dhidi ya serikali ya Uthmaniya. Mwanzoni mwa karne ya 20, Abdul Aziz ibn Abdulrahman ibn Saud, kinara wa moja kati ya makabila ya Hijaz aliamua kuteka moja ya maeneo ambayo yalikuwa yanatawaliwa na Ukhalifa wa Uthmaniyah ambayo alidai eti yalikuwa yameghusubiwa. Kwa msingi hyuo mwaka 1906, baada ya kutea eneo la Riyadh, alijitangaza kuwa mtawala wa eneo hilo. Baada ya hapo watawala wa Uthmaniya walimpa eneo la Al Ahsa la masahriki wa Hijaz na akapata tamaa ya kuendelea kuteka maeneo mengine. Mwaka 1924, Shariff Hussein, Amiri wa Makka ambaye alikuwa kutoka katika ukoo wa Hashemi, alijitangaza Khalifa na hapo Abdul Aziz ibn Saud kwa kisingizo kuwa Amiri alikuwa amejipachika cheo asichostahiki, alianza vita dhidi yake na katika uasi wake huo alifanikiwa kupata uungaji mkono wa makabila na mashekhe wa Kiwahhabi. Hatimaye Disemba 23 mwaka 1925 Miladia, Ukoo wa Hashemi ulisalimu amri na 8 Januari 1926, Abdul Aziz ibn Saud alijitangaza kuwa mfalme wa eneo lote la Hijaz. Hatua hiyo ilikuwa utangulizi na kuundwa rasmi Ufalme wa Saudi Arabia mnamo September 18 mwaka 1932.

Miaka 70iliyopita katika siku kama ya leo, watu saba miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia walinyongwa, kufuatia hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Tokyo. Mahakama hiyo ambayo iliundwa ikiwa ni katika muendelezo wa mahakama ya Nuremberg ya Ujerumani ili kuwahukumu watenda jinai za kivita huko Japan, iliwahukumu viongozi 25 wa Japan ambapo 18 kati yao walihukumiwa kwenda jela. Waziri Mkuu wa wakati huo wa Japan, alikuwa kiongozi wa ngazi za juu zaidi aliyefikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Tokyo na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, mkuu wa zamani wa shirika la kuogofya la usalama na la siri la Urusi ya zamani ambaye pia alikuwa kiongozi nambari mbili wa nchi hiyo katika zama za Joseph Stalin, Lavrentiy Pavlovicha Beria, alihukumiwa kifo na kunyongwa kwa tuhuma za kwenda kinyume na misingi ya sheria za Chama cha Kikomonisti sambamba na kufanya njama dhidi ya serikali. Katika kipindi cha utawala wa Stalin, Pavlovicha Beria alitoa amri ya kuuliwa watu wengi na akafanya umwagaji damu ndani ya Chama cha Kikomonisti na katika Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani.

Siku kama ya leo, tarehe 23 Disemba miaka 5 iliyopita mwaka 2013, aliaga dunia Mrussia Mikhail Kalashnikov ambaye alivumbua bunduki mashuhuri ya Klhashnikov ambayo inajulikana kama AK-47.
Alizaliwa mwaka 1919 katika familia masikini kaskazini mwa Russia, na hakufanikiwa kupata masomo ya juu na hivyo alijiunga na Jeshi la Shirikisho la Sovieti akiwa na umri mdogo. Mwaka 1941, kufuatia shambulizi la Jeshi la Shirikisho la Sovieti dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi, Klashnikov alijeruhiwa na kulazwa hospitalini. Akiwa hospitalini alitumia muda wa kuuguza majeraha kufanya uchunguzi kuhusu sifa za kipekee za bunduki ya Kimarekani ya M1 Garand na bunduki ya StG 44 ya Ujerumani na kwa kutegemea sifa za silaha hizo mbili akaanza kuunda silaha mpya. Uundwaji silaha hiyo ulikamilika mwaka 1947 na kukabidhiwa rasmi Jeshi la Shirikisho la Sovieti mwaka 1951. Bunduki hiyo ilipewa jina la AK-47.

Mwishoni mwa Umri wake, Klashnikov alikuwa amelazwa hospitalini mjini Moscow kutokana na matatizo ya moyo na Septemba 2013 alihamishwa na kupelekwa katika hospitali moja huko Izhevsk, mji mkuu wa Jamhuri ya Udmurtia katika Shirikisho la Russia na hatimaye 23 Disemba 2013, akiwa na umri wa miaka 94 aliaga dunia akiwa anapata matibabu hospitalini.