Pakistan na Afghanistan zafikia makubaliano ya kusitisha mapigano
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i132172-pakistan_na_afghanistan_zafikia_makubaliano_ya_kusitisha_mapigano
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imetangaza kuwa Pakistan na Afghanistan zimekubaliana kusitisha mapigano mara moja katika mazungumzo yaliyofanyika Doha.
(last modified 2025-10-19T11:18:56+00:00 )
Oct 19, 2025 11:18 UTC
  • Pakistan na Afghanistan zafikia makubaliano ya kusitisha mapigano

Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imetangaza kuwa Pakistan na Afghanistan zimekubaliana kusitisha mapigano mara moja katika mazungumzo yaliyofanyika Doha.

Baada ya takriban wiki mbili za mapigano makali yaliyosababisha vifo vya raia na wanajeshi kadhaa, mazungumzo yaliyoandaliwa na Doha yamepelekea kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Makubaliano hayo yanatarajiwa kukomesha makabiliano ya kijeshi yaliyochochewa na masuala ya usalama. Pakistan inaishutumu Afghanistan kuwa imeyapa hifadhi makundi yenye silaha yanayoongozwa na kundi la Taliban la Pakistani katika ardhi yake, madai ambayo Kabul inayakanusha.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imesema kwamba pande hizo mbili zimekubaliana kusitisha mapigano mara moja na kuanzisha taratibu za kuimarisha amani na utulivu wa kudumu.

Pande hizo mbili pia zimekubaliana kufanya mikutano ya ufuatiliaji katika siku zijazo ili kuhakikisha usitishaji mapigano endelevu na kuimarisha utekelezaji wake, hivyo kuchangia katika kufikia usalama na utulivu kati ya nchi zote mbili.

Awali Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ilisema kwamba mazungumzo hayo yatalenga kuchukua hatua za haraka za kukomesha kile ilichoeleza kuwa ni ugaidi unaovuka mpaka na kurejesha amani na utulivu katika mpaka wa Pakistan na Afghanistan.

Makubaliano hayo yanakuja baada ya shutuma za Afghanistan kwamba Pakistan imekiuka mapatano yaliyoanza Jumatano kufuatia mashambulizi ya siku ya Ijumaa ambayo yaliuwa takriban raia 10, wakiwemo watoto wawili na wachezaji watatu wa kriketi.

Hata hivyo wakazi wa maeneo ya mpakani bado wanaishi kwa hofu na woga kutokana na mapigano makali yaliyotokea katika eneo hilo siku chache zilizopita.