Jumatano tarehe 30 Januari 2019
Leo ni Jumatano tarehe 23 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na Januari 30 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 10 Bahman 1357 Hijria Shamsia, wahadhiri na matabaka mengine ya wananchi walitangaza mshikamamo wao na kuamua kuungana na viongozi wa kidini waliokuwa wamekusanyika katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran nchini Iran kuupinga utawala wa Shah. Katika hali ambayo idadi ya watu katika mkusanyiko ilikuwa ikiongezeka kila lahadha, Shapour Bakhtiyar, Waziri Mkuu kibaraka wa utawala wa Shah alilazimika kukubali Imam Khomeini arejee nchini Iran kutoka uhamishoni nchini Ufaransa. Sambamba na hayo ndege za kijeshi za Marekani zilianza kuwaondoa raia wa nchi hiyo nchini Iran.
Katika siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, kiongozi wa taifa la India na mpigania uhuru wa nchi hiyo Mohandas Karamchand Gandhi aliuawa na kijana mmoja wa Kihindu aliyekuwa na misimamo mikali. Gandhi alizaliwa mwaka 1869 na baada ya kukamilisha masomo alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya sheria nchini Uingereza. Mohandas Gandhi kwa muda fulani pia alikuwa kiongozi wa wanamapambano wa Kihindi huko Afrika Kusini. Gandhi pia aliwaongoza wananchi wa India dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika kupigania ukombozi wa nchi hiyo. India ilipata uhuru mwaka 1947 chini ya uongozi wa Gandhi.
Miaka 85 iliyopita katika siku kama ya leo, kilianza kipindi cha uongozi wa Adolph Hitler, dikteta mbaguzi wa Kinazi wa Ujerumani. Chama cha Taifa cha Kisoshalisti cha Wafanyakazi wa Ujerumani ambacho kiliasisiwa na Hitler kilishinda viti 107 vya bunge katika uchaguzi wa mwaka 1930. Adolph Hitler alijitangaza kuwa kiongozi wa Ujerumani mwaka 1934 baada ya kuwa Kansela na Rais wa nchi hiyo. Hitler aliwafanya mamilioni ya wanadamu kuwa wahanga wa malengo yake ya kibaguzi. Hatua ya Adolph Hitler ya kuivamia Poland mwezi Septemba mwaka 1939 ilichochea Vita vya Pili vya Dunia na hatimaye Ujerumani na waitifaki wake walishindwa katika vita hivyo. Hitler alijiua mwaka 1945 baada ya Ujerumani kushindwa katika vita hivyo.
Na miaka 133 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Muhammad Ibrahim mashuhuri kwa lakabu ya Sayyidul Ulamaa, alimu na fakihi wa Kiislamu wa nchini India. Alikuwa mmoja miongoni mwa maulama watajika na mahiri mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria. Baada ya kufariki dunia baba yake, Muhammad Ibrahim alichukua jukumu la kueneza mafundisho ya dini katika baadhi ya miji ya India. Mwanazuoni huyo alifanya hima kubwa ya kueneza misingi na itikadi za Kiislamu katika ardhi ya India. Vilevile ameandika vitabu na makala nyingi.