Feb 07, 2019 02:47 UTC
  • Alkhamisi tarehe 7 Februari 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Jamadithani 1440 Hijria sawa na Februari 7 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 541 iliyopita, alizaliwa Thomas More, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchini Uingereza. Mwanzoni More alisomea elimu ya sheria na baada ya kujiunga bungeni akapewa mazingatio na malkia wa wakati huo na kutunukiwa hadhi ya Ulodi. Hata hivyo Thomas More alitofautiana kinadharia na mfalme wa wakati huo wa Uingereza na hivyo akatiwa jela na kuhukumiwa kifo. Hatimaye More alinyongwa mnamo tarehe sita Julai mwaka 1535 akiwa na umri wa miaka 57.

Thomas More

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, alizaliwa mjini Newcastle Edward Granville Browne, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, mtafiti na fasihi wa nchini Uingereza. Awali Browne alisomea fani ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Cambridge na kuhitimu masomo yake chuoni hapo. Hata hivyo kutokana na kupendelea kwake kusoma tamaduni za mashariki mwa dunia alifanya safiri nchini Iran akiwa na umri wa miaka 25. Aidha mtafiti huyo aliitaja lugha ya Kifarsi kuwa njia bora ya kunakili fikra na tamaduni za Wairan kuelekea maeneo mengine ya dunia. Ni kwa msingi huo ndio maana akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na historia na utamaduni wa Wairani. Mwishoni Edward Granville Browne alijikita katika kufundisha lugha ya Kifarsi na Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Cambridge, na kufariki dunia mwaka 1926 akiwa na umri wa miaka 54. 

Edward Granville Browne

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Februari 1974, nchi ndogo ya Grenada iliyoko Amerika ya Latini ilijipatia uhuru wake. Nchi hiyo iliyoko kisiwani, ilivumbuliwa mwaka 1498 na mvumbuzi mashuhuri wa Kihispania Christopher Columbus. Amma baada ya kutokea sutafahumu kati ya nchi za Uhispania, Ufaransa na Uingereza juu ya umiliki wa kisiwa hicho, hatimaye Ufaransa iliidhibiti na kuitawala nchini hiyo mwaka 1674. Baada ya kupita karibu karne moja, mnamo 1783, Waingereza waliikoloni nchi ya Grenada kwa muda wa karne mbili, na hatimaye mwaka 1974 katika siku kama ya leo nchi hiyo ikajipatia uhuru wake.

Bendera ya Granada

Tarehe 18 Bahman miaka 35 iliyopita aliuawa Jenerali Gholam-Ali Oveissi aliyehusika na mauaji ya wananchi wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Jenerali Oveissi ambaye alikuwa kamanda Mkuu wa Jeshi la Utawala wa Kifalme alihusishwa na mauaji ya wananchi wa Iran mwaka 1962 na 1978 katika vuguvugu la wananchi wa Iran la kutaka kuanzishwa Jamhuri ya Kiislamu na kuuondoa madarakani utawala wa dhalimu wa kifalme. Oveissi alikimbia nchi mwezi mmoja kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hata kabla ya Shah Pahlavi kutoroka nchi. Mwezi mmoja baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jenerali Oveissi alifanya jitihada za kuwakusanya tena waungaji mkono wa utawala wa kifalme nchini Iran na kutoa dharba kwa Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo njama hizo zilishindwa na hatimaye kibaraka huyo wa Shah aliuawa katika siku kama hii leo akiwa Paris nchini Ufaransa. 

enerali Gholam-Ali Oveissi

Na siku kama ya leo miaka 20 iliyopita aliaga dunia Hussein bin Talal mfalme wa zamani wa Jordan kwa ugonjwa wa saratani. Alizaliwa mwaka 1935 huko Amman mji mkuu wa Jordan na kuhitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Uingereza. Mfalme Hussein alikalia kiti cha usultani huko Jordan mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 17 kufuatia kuuawa babu yake mfalme Abdallah na baada ya baba yake Amir Talal kukalia kiti cha uongozi kwa miezi kadhaa tu. Mapinduzi na mauaji mengi yalitokea wakati wa usultani wa mfalme Hussein bin Talal huko Jordan. Mfalme huyo alijulikana sana kwa kuunga mkono utawala haramu wa Israel na Julai mwaka 1994 aliutambua rasmi utawala huo ghasibu. 

Hussein bin Talal

 

Tags