Feb 12, 2019 04:24 UTC
  • Jumanne, tarehe 12 Februari, 2019

Leo ni Jumanne tarehe 6 Jamadithani 1440 Hijria sawa na Februari 12 mwaka 2019.

Tarehe 12 Februari miaka 11 iliyopita aliuawa shahidi Imad Mughnia maarufu kwa jina la Haj Ridhwan, ambaye alikuwa miongoni mwa makamanda wa Hizbullah ya Lebanon, katika shambulizi la kigaidi lililofanyika mjini Damascus, Syria. Kamanda Mughnia aliuawa katika mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa na vibaraka wa Israel katika gari lake. Shahid Mughnia alijiunga na harakati za mapambano baada ya uvamizi wa Israel nchini Lebanon. Baadaye kidogo alijiunga na harakati ya Hizbullah na kushika nyadhifa za juu katika harakati hiyo. Shahid Mughnia alikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Hizbullah dhidi ya Israel katika vita vya siku 33 vya utawala huo nchini Lebanon mwaka 2006.

Imad Mughnia

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita serikali ya mpito ya Mapinduzi ya Kiislamu ilianza rasmi kazi zake katika siku za mwanzo kabisa za umri wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Wakati huo huo wananchi waliendeleza mapambano ya kuangamiza kikamilifu mabaki ya utawala wa Shah. Baadhi ya makundi ya wananchi yalichukua jukumu la kulinda taasisi muhimu za serikali katika miji mbalimbali. Wakati huo ulidhihiri udharura wa kuwepo chombo cha kushughulikia kadhia hiyo na kukabiliana na vibaraka na mabaki ya utawala wa Shah. Kwa msingi huo Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Kamati ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Kamati ya Mapinduzi ya Kiislamu

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita aliuawa shahidi mwasisi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin na mwanamapambano mashuhuri wa Misri, Ustadh Hassan al Banna. Hassan al Banna aliuawa shahidi katika njama iliyopangwa na Uingereza kwa kushirikiana na Mfalme Faruq wa Misri. Alianza mapambano yake dhidi ya ukoloni na vibaraka wake akiwa chuo kikuu ambapo alianzisha harakati ya kupambana na sera za kupinga dini ya Kiislamu za Uingereza kwa kuasisi hatakati ya Ikhwanul Muslimin hapo mwaka 1928. Harakati hiyo ilikuwa kwa kasi na kuenea katika nchi za Syria, Jordan, Lebanon, Palestina na katika baadhi ya nchi za kaskazini mwa Afrika. Serikali ya Misri ilipiga marufuku harakati ya Ikhwanul Muslimin mwaka 1948 na kuwatia jela wanachama wake wengi na kisha kumuua shahidi kiongozi wake Sheikh Al Banna.

Ustadh Hassan al Banna

Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita nchi ya Chile ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Chile ilikaliwa kwa mabavu na Uhispania mnamo mwaka 1536. Mwaka 1788, Mfalme Charles III aliyekuwa mfalme wa Uhispania aliangalia upya makoloni yake na hivyo akaamua kuikabidhi nchi hiyo kwa Peru. Harakati ya kwanza ya kupigania uhuru nchini Chile ilianza mwaka 1814 Miladia. Katika harakati hizo wapiganaji waliokuwa wanataka kujitenga walishindwa vibaya na askari wa serikali ya kikoloni. Hata hivyo mwaka 1817 Miladia, José de San Martín, raia wa Argentina akishirikiana na maelfu ya wapiganaji alianzisha harakati dhidi ya makoloni ya Mfaransa ikiwemo Peru na Chile. Kwa uungaji mkono wa raia wa Chile hatimaye alifanikiwa kuwatimua wakoloni wa Uhispania na nchi hiyo kupata uhuru wake mwaka mmoja baadaye yaani mwaka 1818 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 210 iliyopita alizaliwa mtaalamu wa elimuviumbe wa Uingereza, Charles Darwin. Msomi huyo alifanya utafiti kuhusu namna ya kutokea viumbe mbalimbali na alifanya safari ya muda mrefu duniani kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wake wa kielimu. Baada tu ya kurejea aliandika kitabu maarufu cha "On the Origin of Species". Kwa mujibu wa nadharia ya Darwin ambaye ndiye aliyeanzisha mfumo wa Darwinism, chanzo cha viumbe vya leo ni viumbe vidogovidogo ambavyo vilibadilika kutokana na mazingira tofauti kwa miaka mingi na kufikia hali ya sasa.

Charles Darwin

Siku kama ya leo miaka 215 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 Immanuel Kant, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchini Ujerumani. Kant alizaliwa mwaka 1724 katika familia ya kidini na alitumia sehemu kubwa ya umri wake katika kusoma, kufundisha na kuandika vitabu katika taaluma mbalimbali kama hisabati, nujumu, mantiki na falsafa. Ameacha athari nyingi ikiwa ni pamoja na 'Misingi ya Falsafa' 'Ukosoaji wa Akili ya Kivitendo' na 'Ukosoaji wa Akili ya Nadharia.'

Immanuel Kant

 

Tags