Feb 24, 2019 02:41 UTC
  • Jumapili 24 Februari 2019

Leo ni Jumapili tarehe 18 Jamadith-Thani 1440 Hijiria, sawa na tarehe 24 Februari, 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 494 iliyopita, alizaliwa Luis Vaz de Camoens, malenga mkubwa wa Kireno na mmoja wa wanafasihi wakubwa wa Ulaya huko Lisbon mji mkuu wa Ureno. Mbali na kuwa mshairi, De Camoens alikuwa mpiganaji jasiri na shujaa. Moja ya kazi muhimu za utunzi za Luis Vaz de Camoens ni ile aliyoipa jina la" The Lusiads." Mshairi huyo mahiri wa Kireno aliaga dunia mwaka 1580.

Luis Vaz de Camoens

Siku kama ya leo miaka 421 iliyopita aliuawa shahidi Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari, faqihi, mwanatheolojia na alimu mkubwa. Alizaliwa mwaka 956 Hijiria katika familia bora na ya kielimu mjini Shushtar, kusini magharibi mwa Iran. Sayyid Nurullah Shushtari alijifunza masomo ya awali ya kidini kwa baba yake na kisha akaelekea mjini Mash’had, kaskazini mashariki mwa Iran na kuweza kustafidi na elimu kutoka kwa maulama wakubwa wa mji huo. Yapata mwaka 993, Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari alielekea India kwa ajili ya kufanya tablighi ambapo wakati huo nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Mfalme Akbar Shah katika silsila ya Mongolia huku ikiwa na utulivu. Hadhi yake, elimu na uadilifu wa Sayyid Shushtari vilimfanya ateuliwe kuwa kadhi wa mji wa Lahore nchini humo. Baada ya kufariki dunia Mfalme Akbar Shah, wapinzani wa alimu huyo walimwendea mfalme aliyechukua uongozi kwa jina la Jahangir Shah na kumwambia maneno ya uongo na ya uchonganishi ambapo kwa kutumia kisingizio cha madhehebu ya Shia ya alimu huyo mkubwa akauawa shahidi katika siku kama ya leo. Sayyid Nurullah Shushtari aliandika vitabu kadhaa miongoni mwavyo ni ‘Majaalisu-Mu’miniina’ ‘Ihqaaqul-Haqqi’ na ‘Tuhfatul-Uquul.’

Eneo alipozikwa Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari

Siku kama ya leo miaka 171 iliyopita, utawala wa muda au duru ya pili ya mfumo wa jamhuri ulianza huko Ufaransa baada ya wananchi kuendesha mapambano ya ukombozi na kumuondoa madarakani Luis Phillipe Mfalme dikteta wa nchi hiyo. Utawala wa aina hiyo unajulikana pia katika historia ya Ufaransa kwa jina la "Utawala wa Waandishi wa Habari". Hii ni kwa sababu waandishi habari 11 waliokuwa wakipigania mfumo wa jamhuri chini ya uongozi wa Alphonse de Lamartine malenga na mwandishi wa Kifaransa, ndio waliokuwa wakisimamia utawala huo. 

Luis Phillipe

Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita, alifariki dunia Nikolay Ivanovich Lobachevsky, mwanahisabati wa Russia. Alizaliwa mwaka 1792 Miladia katika familia masikini. Nikolay Ivanovich Lobachevsky alikuwa na kipawa kikubwa ambapo akiwa katika rika la ujana alifanikiwa kuwa mhadhiri wa chuo kikuu na baadaye kuwa rais wa chuo Kikuu cha Gazan, kusini mwa Russia. Umashuhuri wa msomi huyo uliongezeka zaidi kutokana na utafiti na uvumbuzi wake. Nikolay Ivanovich Lobachevsky alifariki dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 63.

Nikolay Ivanovich Lobachevsky

Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, yaani tarehe 18 Jumadi Thani 1281 aliaga dunia faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq. Alizaliwa mwaka 1214 Hijria Shamsia katika mji wa Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasail na Makasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.

Sheikh Murtadha Ansari

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita sawa na tarehe 24 Februari 1949 wawakilishi wa Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel walisaini mkataba wa kusitisha mapigano kati ya pande mbili hizo huko katika kisiwa cha Rhodes kilichoko katika bahari ya Aegean. Ni vyema kutaja hapa kuwa, baada ya kuundwa serikali ya Kizayuni mwaka 1948 huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Misri ilishirikiana bega kwa bega na baadhi ya nchi za Kiarabu katika kupigana vita dhidi ya utawala wa Kizayuni. Hata hivyo wanajeshi wa utawala huo walifanikiwa kuingia katika ardhi ya Misri na Lebanon baada ya kuishambulia safu ya vikosi vya mapambano vya Waarabu ambavyo vilikuwa na zana chache za kisasa za kivita na hivyo kutoa pigo kwa vikosi vya nchi za Kiarabu.

Kusitishwa mapigano baina ya Misri na utawala wa Kizayuni