Apr 06, 2019 03:59 UTC
  • Jumamosi, 06 Aprili, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 30 ya mwezi Rajab 1440 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 6 Aprili 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 439 iliyopita, ardhi ya Ureno moja kati ya nchi iliyokuwa na nguvu barani Ulaya katika karne za 15 na 16 iliunganishwa na Uhispania. Ureno ilikuwa ikihesabiwa kama mpinzani mkuu wa kisiasa na kikoloni wa Uhispania huko Asia, Afrika na Marekani. Hata hivyo pole pole Ureno ilianza kupoteza satwa na nguvu yake ya kisasa kutokana na raia wa nchi hiyo kuhamia kwa wingi katika nchi makoloni ya Ureno na vile vile kufuatia hali mbaya ya kiuchumi. Udhaifu na kutokuwa na nguvu Ureno uliipelekea Uhispania kuivamia nchi hiyo. Pamoja na hayo yote hatimaye mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Ureno ya mwaka 1640 yalipelekea kukombolewa nchi hiyo. ***

Bendera ya Ureno

Miaka 102 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya Marekani ilitangaza vita dhidi ya Ujerumani na ikaingia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kwa maslahi ya waitifaki. Tab'an kabla ya hatua hiyo, Marekani ilikuwa imekata uhusiano wake wa kisiasa na Ujerumani na ilikuwa ikizisaidia nchi waitifaki. ***

Katika siku kama ya leo miaka 34 iliyopita Jaafar Nimeiry, Rais wa zamani wa Sudan alipinduliwa na Jenerali Abdulrahman Swarul Dhahab aliyekuwa Waziri wa Ulinzi ambaye alichukua madaraka ya kuiongoza Sudan. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Nimeiry pia aliingia madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Sudan mwaka 1969. Nimeiry aliongoza Sudan kimabavu kwa miaka 16 na kuanzisha uhusiano mkubwa kati ya nchi hiyo na Marekani. ***

Jaafar Nimeiry

Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, Wahutu wenye misimamo mikali wa Rwanda walianzisha mauaji makubwa dhidi ya Watutsi. Katika mauaji hayo Wahutu wenye misimamo mikali waliwauwa kwa umati raia wa Kitutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani karibu milioni moja na kuwafanya wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi. Wahutu wanaunda asilimia 84 ya jamii ya Rwanda na kabila hilo lilikuwa madarakani hadi mwaka 1994. ***

Mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyotokea mwaka 1994