May 07, 2019 04:13 UTC
  • Jumanne, Mei 7, 2019

Leo ni Jumanne tarehe Mosi Ramadhani 1440 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Mei, 2019 Milaadia.

Leo ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria; mwezi ambao ndani yake iliteremshwa Qurani Tukufu. Ni mwezi wa rehema na baraka za kiroho. Katika kubainisha utukufu wa mwezi huu, Mtume Mtukufu SAW amesema, siku za mwezi huu ndizo siku bora zaidi kuliko siku nyingine zote na kuwataka Waislamu wachume na wafaidike kutokana na fadhila na baraka za kiroho za mwezi huu. Allah SWT anasema: ((Hakika tumeiteremsha (Qurani) katika usiku wa heshima. Na nini kitakujulisha usiku huo wa heshima ni nini? Laylatul Qadr (usiku huo wa heshima) ni bora kuliko miezi elfu.))

Tukio la kuhuzinisha moyo la kuuawa shahidi Imam Ali AS na kuzaliwa Mjukuu wa Mtume SAW,  Imam Hassan AS,  ni katika matukio muhimu yaliyotimia katika mwezi huu. Tunamuomba Allah SW atupe baraka za kimaanawi za mwezi huu na kwa fadhila za mwezi huu mtukufu tuwe karibu na rehema na msahamaha Wake.

 

Aidha katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kiliteremshwa kitabu cha Suhf cha Nabii Ibrahim AS. Jina Ibrahim limetajwa mara 69 katika Qur'ani Tukufu kwa heshima na taadhima ambapo maisha yake yameashiriwa kwa njia mbali mbali kama ibra na ruwaza njema kwa waumini. Mwenyezi Mungu amemtaja kuwa ni mtu mwenye kumuabdudu Mungu mmoja na dini imetajwa kuwa ya Hanifa katika aya ya 67 ya Sura Aal Imran na pia katika aya ya 125 ya Sura An Nisaa. Alikuwa Nabii mkweli kama tunavyosoma katika Surat Maryam aya ya 41. Aidha Mwenyezi Mungu alimpa yeye na familia yake neema na mamlaka kama tunavyosoma katika Surat An Nisaa aya ya 54.

Kuna vitabu kadhaa vya mbinguni ambavyo waliteremshiwa Mitume kama vile Suhf cha Ibrahim AS na Nuh AS, Taurati ya Musa AS na Injili ya Issa AS na kitabu kilicho kamilika kati ya vyote hivyo ni Qur'ani Tukufu.

 

Katika siku kama ya leo miaka 1012 iliyopita alifariki dunia Ibn Sina maarufu kwa jina la Sheikhur Rais, tabibu, mtaalamu wa hisabati, falsafa na mnajimu mkubwa wa Kiirani. Ibn Sina alifariki dunia katika mji wa Hamadan ulioko magharibi mwa Iran akiwa na umri wa miaka 58. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana na akapata kusoma elimu za mantiki, uhandisi na utaalamu wa nyota. Baada ya kumtibu Nuh bin Mansur, mmoja wa Wafalme wa Kisamani akiwa kijana, Ibn Sina alipata idhini ya kutumia maktaba kubwa ya mfalme huyo. Katika maktaba hiyo, Ibn Sina alipata kusoma vitabu vingi vya elimu tofauti. Abu Ali Sina alitokea kuwa msomi, mwandishi na mtafiti mashuhuri. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha "Shifaa" kinachohusu elimu ya falsafa, "Qanun" kinachohusu tiba na "Daneshnameh Allai".

Abu Ali Sina (Avicenna)

 

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mei 1888, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilianzisha uvamizi katika ardhi ya Zimbabwe ya sasa. Mipango ya kuikalia kwa mabavu Zimbabwe ilibuniwa na mwanasiasa na mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina la Cecile Rhodes, ambaye aliasisi shirika la Afrika Kusini la Kiingereza nchini humo. Kwa kusaidiwa na jeshi la Uingereza, Rhodes aliuwa kwa umati maelfu ya raia wazalendo na kuwakamata mateka wengine wengi, na hivyo kuweza kuidhibiti ardhi yote ya Zimbabwe na kuipachika jina lake la Rhodesia.

Bendera ya Zimbabwe

 

Miaka 211 iliyopita katika siku kama ya leo wananchi wa Uhispania walianzisha harakati dhidi ya vikosi vya jeshi la Mfalme Napoleon wa Ufaransa, vilivyokuwa vinakalia kwa mabavu nchi yao. Wakati huo Uhispania pia ilikuwa ikihesabiwa kuwa moja ya makoloni makubwa ya Ulaya na ilikuwa ikikalia kwa mabavu ardhi nyingi nje ya bara hilo. Lakini wananchi wa Uhispania walikuwa wameonja uchungu wa nchi yao kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya kigeni. Baada ya miaka mitano ya mapambano dhidi ya vikosi vamizi vya Ufaransa, walifanikiwa kuvifukuza vikosi hivyo mwezi Disemba mwaka 1813 kutoka nchini kwao. Wakati huo huo kutokana na kushindwa katika Amerika ya Kusini, Uhispania ililazimika kuziacha huru nchi kadhaa ilizokuwa ikizikoloni.

Bendera ya Uhispania

 

Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, alizaliwa Robert Browning, malenga na mwanafikra wa nchini Uingereza. Akiwa kijana mdogo Browning alikuwa na maandalizi ya kuwa malenga ambapo alitoa shairi lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 12. Taratibu akaanza kupata umashuhuri katika jamii ya Uingereza kama malenga mkubwa. Robert Browning alikuwa akiwasilisha itikadi yake juu ya umoja wa Mungu duniani kupitia mashairi yake. Ameacha athari nyingi katika uwanja huo. Robert Browning alifariki dunia mwaka 1889.

Robert Browning

 

Tags