Jul 10, 2019 02:34 UTC
  • Jumatano, 10 Julai, 2019

Leo ni Jumatano tarehe 7 Mfunguo Pili Dhulqaada 1440 Hijria sawa na tarehe 10 Julai 2019.

Miaka 724 iliyopita  siku kama ya leo alifariki dunia Ibn Baswis mtaalamu wa hati aliyejulikana kama Damashki. Alizaliwa mwaka 651 Hijiria katika mji wa Damascus na kwa muda wa miaka 50 alijishughulisha kufundisha hati na wakaazi wa mji huo walistafidi kwa elimu na sanaa kutoka kwake. Ibn Baswis aliandika hati kwa mitindo tofauti ya kupendeza na katika umri wake wa uzeeni aliandika kurasa za Qur'ani Tukufu kwa maji ya waridi na kwa hati zilizo nzuri sana. Qur'ani hiyo pamoja na athari nyingine za Ibn Basis bado ziko hadi leo.

ابن بصیص

 

Miaka 278 iliyopita ardhi ya Alaska iligunduliwa na mvumbuzi wa Kidenmark kwa jina la Vitus Bering. Mvumbuzi huyo aligundua ardhi ya Alaska inayopatikana kaskazini magharibi mwa Canada akiwa katika safari yake kuelekea Urusi. Hadi kufikia mwaka 1867 eneo tajiri kwa mafuta la Alaska lilikuwa sehemu ya mamlaka ya Urusi ya Kitezari. Hata hivyo mwaka huo Urusi iliiuzia Marekani ardhi ya Alaska kwa kiasi cha dola milioni saba, eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa jimbo la 49 la Marekani.

Vitus Bering

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita inayosadifiana na 10 Julai 1940 Jemedari Henri Petain Waziri Mkuu wa muda na afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Ufaransa, alichukua uongozi baada ya Ufaransa kushindwa na Wanazi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa mkataba wa kivita uliosainiwa na nchi mbili hizo tarehe 22 Juni 1940, eneo la kaskazini mwa Ufaransa, ukiwemo mji wa Paris lilibaki chini ya himaya ya jeshi la Manazi wa Ujerumani.

medari Henri Petain

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Bahamas huko Amerika ya Kati vilipata uhuru kutoka Uingereza na siku kama ya leo hufahamika visiwani humo kama siku ya taifa. Visiwa vya Bahamas viligunduliwa mwaka 1492 na mvumbuzi wa Ulaya Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania. Visiwa vya Bahamas vilipata uhuru mwaka 1973 na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Visiwa vya Bahamas viko kaskazini mwa Cuba na kusini mashariki mwa Marekani.