Jumapili, 14 Julai, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 11 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1440 Hijria, inayosadifiana na tarehe 14 Julai 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1292 iliyopita, yaani sawa na tarehe 11 Dhulqaad mwaka 148 Hijria, alizaliwa Imam Ali bin Mussa Ridha (as), mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (as) katika mji wa Madina. Imam Ridha alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu mara baada ya kufariki dunia baba yake Imam Mussa al-Kadhim (as), mnamo mwaka 183 Hijiria. Mtukufu huyo alikuwa mtu bora zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu wakati wa zama zake. Kwa minajili hiyo, Ma'amun Khalifa wa Bani Abbas alijaribu kumpatia kazi Imam Ridha (as) kwa shabaha ya kuimarisha nafasi yake na wakati huo huo kumdhibiti Imam. Imam Ridha (as) alikubali pendekezo hilo kwa kulazimishwa na kwa mashinikizo ya utawala wa Ma'amun. Mtukufu huyo aliwaeleza Waislamu wote, wakiwemo watu wa eneo la Khorasan, ukweli wa mambo ulivyokuwa, na kuwaathiri mno wananchi kuhusiana na uhakika wa Ahlul-Bayt wa Mtume (as). Redio Tehran inatoa mkono wa heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani hususan wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume (as) kwa mnasaba huu adhimu wa kuzaliwa mtukufu huyo (as).
Siku kama ya leo miaka 1104 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 11 Dhul Qaad 336 Hijria, ilizaliwa Muhammad bin Muhammad mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na mwanafaqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad. Sheikh Mufid alilelewa katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na kisha kujipatia elimu kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Miongoni mwa harakati zake za kifikra na kiutamaduni ilikuwa ni kufanya midahalo na mafaqihi na wasomi wa Madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu vingi vyenye thamani vikiwemo vya al Irshaad, al Arkaan na Usuulul Fiqh.
Siku kama ya leo miaka 230 iliyopita, sawa na tarehe 14 Julai 1789 Miladia, gereza la kihistoria la Bastille lilitekwa na wakazi wa Paris katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa na sehemu kubwa ya gereza hilo kuharibiwa. Jela hiyo ilijengwa mwaka 1369 kwa lengo la matumizi ya kijeshi. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa iligeuzwa na kuwa gereza la kutisha ambapo ndani yake walizuiliwa wafungwa wengi wa kisiasa hususan watu waliokuwa wakiendesha harakati za kudai serikali ya jamhuri nchini humo. Gereza la Bastille lilidhihirisha udikteta wa wafalme wa Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita ilitengenezwa bunduki ya kwanza ya rashasha. Bunduki hiyo ilitengenezwa na msomi wa Kimarekani Dr. Richard J. Gatling kwa kutumia uzoefu wa wavumbuzi wa kabla yake wa silaha. Bunduki iliyotengezwa na Gatling haikuwa ya utomatiki lakini baadaye teknolojia ya kutengeneza silaha hiyo iliboreshwa zaidi na hii leo bunduki ya rashasha inatambuliwa kuwa silaha muhimu sana katika medani za vita.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, yaani sawa na tarehe 14 Julai 1958 Miladia, Jenerali Abdul Karim Qassim alifanya mapinduzi ya kijeshi nchini Iraq na kuuondoa madarakani utawala wa Kifalme na kisha kuanzisha mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri. Mfalme Faisal II, Abdallah, Mrithi wake wa Kiti cha Ufalme na Nuri Said Waziri Mkuu wa Iraq waliuawa katika tukio hilo la mapinduzi. Aidha wafuasi wa utawala wa Kifalme walikandamizwa na kusambaratishwa kabisa. Baada ya mapinduzi hayo, Abdul Karim Qassim aliyekuwa na mitazamo ya utaifa alishika hatamu za uongozi nchini Iraq hadi mwaka 1963, wakati alipokuja kuondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi pia na Abdul Salam Arif aliyekuwa muitifaki wake mkubwa na wa karibu.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita yaani tarehe 23 Tir mwaka 1362 Hijria Shamsia, duru ya kwanza ya Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi Zake ilianza shughulki zake. Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Baraza la Wanazuoni ni moja ya nguzo na asasi muhimu katika mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini. Wawakilishi wa baraza hilo ni lazima wawe mafakihi waliotimiza masharti na huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi. Jukumu muhimu la Baraza la Wataalamu ni kumchagua Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusimamia utendajikazi wake. Uchaguzi wa baraza hilo la Iran hufanyika mara moja kila baada ya miaka minane.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, alifariki dunia Mahdi Hamidi Shirazi, malenga, mtafiti na mwandishi mkubwa wa zama hizi. Mahdi Shirazi alizaliwa mwaka 1293 Hijria katika mji wa Shiraz wa kusini mwa Iran na kutunukiwa shahada ya udakta katika taaluma ya lugha na fasihi ya Kifarsi. Dakta Hamidi ameandika vitabu vingi vya mashairi ya Kifarsi, ambapo vingi vinahusiana na elimu ya mitindo, fasihi, historia na taaluma mbalimbali za mashairi.
Na katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, alifariki dunia Dakta Abdul-Hadi Hairi, mmoja wa walimu wakubwa wa historia nchini Iran. Dakta Hairi, alizaliwa mjini Qum katika familia ya kidini. Aidha msomi huyo alikuwa mjukuu wa marjaa mkubwa na mwasisi wa hauza ya masomo ya kidini ya mjini hapo, Ayatullah Haj Sheikh Abdul-Karim Hairi. Baada ya kusoma masomo ya awali ya theolojia, aliendelea na masomo yake huko nchini Canada.