Aug 04, 2019 02:36 UTC
  • Jumapili, 04 Agosti, 2019

Leo ni Jumapili tarehe Pili Mfunguo Tatu Dhulhija 1440 Hijria sawa na tarehe 4 Agosti mwaka 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 227 iliyopita, alizaliwa Percy Bysshe Shelley malenga wa Uingereza. Percy alianza kupenda taaluma ya fasihi tangu utotoni na kuonyesha kipawa kikubwa katika uwanja huo. Alikuwa mfuasi na muungaji mkono wa thamani za upendo, urafiki na uhuru na sababu hiyo ndiyo iliyomfanya avutiwe na mapinduzi ya Ufaransa ambayo ndio kwanza yalikuwa yametokea. Percy Bysshe Shelley aliaga dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 30 baada ya boti yake kuzama katika Bahari ya Mediterrania. ***

Percy Bysshe Shelley

Miaka 214 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu wa elimu ya fizikia wa Ireland alizaliwa.  Alikuwa na kipaji cha hali ya juu kiasi kwamba akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa amejifunza lugha 12 za dunia zikiwemo Kiarabu na Kifarsi. William Rowan Hamilton taratibu akaanza kuwa na mapenzi makubwa na elimu za fizikia na hisabati. Aidha alifanikiwa kuanzisha baadhi ya kanuni na mifumo muhimu katika elimu hizo. Akiwa na umri wa miaka 22 Hamilton alikuwa tayari ni mwalimu wa elimu ya nujumu. Msomi huyo aliaga dunia 1865. ***

William Rowan Hamilton

Katika siku kama ya leo miaka 144 iliyopita, aliaga dunia Hans Christian Andersen mwandishi wa vitabu vya watoto wa nchini Denmark. Alizaliwa mwaka 1805 na tangu akiwa mdogo alikuwa na mapenzi makubwa na visa. Baada ya kuaga dunia baba yake, Hans Christian Andersen akiwa na umri wa miaka 11 aliacha shule na kuanza kufanya kazi. Baada ya kuingia katika maonyesho na michezo ya kuigiza ya kifalme, hali yake ya maisha iliboreka na hivyo akaamua kuendelea na masomo. Mwandishi huyo wa Kidenmark awali alianza kujihusisha na utungaji mashairi na kuandika visa na simulizi. Hata hivyo baadaye Andersen aliondokea kuwa na mapenzi makubwa na visa vya watoto na alionyesha kipaji kikubwa alichokuwa nacho katika uwanja huo. ***

Hans Christian Andersen

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, vikosi vilivyokuwa na mrengo wa utaifa nchini Uturuki vikiongozwa na Mustafa Kemal Ataturk vilianza kuwashambulia wanajeshi wa Ugiriki waliokuwa wameikalia kwa mabavu nchi hiyo. Baada ya kusambaratika utawala wa Othmania katika Vita vya Kwanza vya Dunia, ardhi asili ya utawala huo yaani Uturuki iliangukia mikononi mwa tawala waitifaki. ***

Mustafa Kemal Ataturk

Katika siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, alizaliwa katika mji wa Mash'had Iran Ayatullah Sayyid Ali Sistani fakihi, alimu na marjaa taqlidi wa Kishia.  Alianza kujifunza Qur'an akiwa na miaka 5 na akiwa na umri wa miaka 11 alianza kusoma masomo ya kidini ya utangulizi baada ya kutakiwa na baba yake kufanya hivyo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Baadaye Ayatullah Sistani alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Najaf Iraq. Hii leo Ayatullah Sistani si tu kwamba, anahesabiwa kuwa marjaa mkubwa zaidi nchini Iraq bali amekuwa pia na nafasi muhimu katika kuleta umoja, mshikamno na utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu. ***

Ayatullah Sayyid Ali Sistani

Na siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, Marekani ilishindwa katika vita vya baharini vilivyozishirikisha meli za kivita za Marekani na Vietnam ya Kaskazini katika Ghuba ya Tonkin inayopatikana kwenye bahari ya China ya Kusini. Mivutano hiyo ya kijeshi iliipa Marekani kisingizio cha kuingia vitani moja kwa moja na Vietnam ya Kaskazini. Wakati huo Washington ilikuwa ikiiunga mkono kwa pande zote Vietnam ya Kusini dhidi ya ile ya Kaskazini. Baada ya kushindwa katika vita hivyo, serikali ya wakati huo ya Washington iliongeza idadi ya askari wake huko Vietnam ya Kusini na kisha kufanya mashambulio makubwa ya anga na ardhini dhidi ya wananchi wa Vietnam ya Kaskazini. Hata hivyo mashambulio hayo yalikabiliwa na upinzani mkubwa wa wananchi wa nchi hiyo.***

Vietnam

 

Tags