Ijumaa, Agosti 23, 2019
Leo ni Ijumaa tarehe 21 Mfunguo Tatu Dhulhija 1440 Hijria sawa na Agosti 23 mwaka 2019 Milaadia.
Miaka 77 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vita vya Stalingrad vilianza kati ya majeshi ya Muungano wa Sovieti ya zamani na Ujerumani. Katika siku hii pekee askari 40,000 wa pande zote mbili waliuawa katika vita hivyo vya umwagaji damu mkubwa. Umwagikaji damu huo ulitokana na ukweli kwamba Adolph Hitler wa Ujerimani alitoa amri ya kutekwa mji wa Stalingrad kwa hali yoyote ile. Kwa msingi huo, askari wa Ujerumani waliamua kuushambulia kwa nguvu zao zote lakini walikabiliwa na mapambano makali ya wakazi wa mji huo na hatimaye kushindwa. Wanahistoria wanaamini kuwa huo ndio ulikuwa mwanzo wa kusambaratika jeshi la Hitler.
Siku kama ya leo, miaka 75 iliyopia, mji wa Paris ulikombolewa kutoka kwenye uvamizi wa Ujerumani. Miezi 15 baada ya kushtadi moto wa Vita vya Pili vya Dunia na katika kuendeleza njama zake za kutaka kujitanua, dikteta Adolph Hitler aliyaamuru majeshi ya nchi hiyo kuushambulia mji wa Paris kwa lengo la kutaka kuudhibiti mji huo. Tarehe tano Juni mwaka 1940, Hitler alitoa amri ya kuharibiwa kikamilifu muundo wa majeshi ya Ufaransa na siku tatu baadaye yaani tarehe nane Juni mwaka 1940, vikosi vya Wanazi vilikishinda kikosi cha ulinzi cha Ufaransa katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa hilo, na hivyo kutoa mwanya kwa jeshi la Ujerumani kuingia nchini Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Agosti 2003, alifariki dunia Michael Kijana Wamalwa, Makamu wa Rais wa Kenya. Wamalwa alizaliwa 25 Novemba 1944 katika kijiji cha Sosio karibu na Kimilili, wilayani Bungoma. Michael Kijana Wamalwa alikuwa mtoto wa mwanasiasa na mbunge machachari William Wamalwa. Mwaka 2002, Wamalwa akiwa pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri nchini Kenya, wakiongozwa na Mwai Kibaki wa chama cha National Rainbow Coalition NARC, walifanikiwa kuung'oa madarakani utawala wa chama cha KANU uliotawala nchi hiyo kwa zaidi ya miongo minne. Kijana Wamalwa alizikwa kwenye shamba lake lililoko Kitale.
Siku hii ya tarehe Mosi Shahrivar kwa kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi mwanafalsafa, tabibu na msomi mkubwa wa Kiislamu na Kiirani Hussein bin Abdullah maarufu wka jina la Ibn Sina. Ibn Sina alihifadhi Qur'ani yote alipokuwa na umri wa miaka 10. alijifunza utabibu baada ya kupata elimu za mantiki, hisabati, nujumu, falsafa pamoja na elimu nyinginezo. Alianza kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 21 na miongoni mwa vitabu vyake maarufu ni Qanun, Shifaa na al Isharaat. Siku hii huenziwa hapa nchini Iran kama Siku ya Daktari.