Jumatano, tarehe 4, Septemba 2019
Leo ni Jumatano tarehe 4 Muharram mwaka 1441 Hijria inayosadifiana na Septemba 4 mwaka 2019.
Siku kama ya leo, miaka 1380 iliyopita, Ubaidullah bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa mji wa Kufa, Iraq alitoa hotuba katika msikiti wa mji huo. Katika hotuba hiyo, Ibn Ziyad alitoa vitisho vikali dhidi ya wafuasi wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (swa) akiwataka wasimsaidie mtukufu huyo katika ardhi ya Karbala na kwamba atamuua mtu yeyote ambaye ataasi amri hiyo. Kwa kutumia fatwa ya hila iliyotolewa na Shuraihul-Qadhi ya kuhalalisha damu ya Imam Hussein (as), Ibn Ziyad akafunga njia zote za kuingia na kutoka mji wa Kufa huku akitoa fedha kwa wakazi wa mji huo kwa ajili ya kwenda kupambana na mjukuu huyo wa Mtume huko Karbala tukio lililomalizika kwa kuuawa Imam Hussein na watu wa familia ya Mtume (swa).

Siku kama ya leo miaka 956 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Muhammad Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Naqiya, malenga, mwandishi na fasihi mkubwa wa mjini Baghdad, Iraq. Umahiri aliokuwa nao Ibn Naqiya, ndio uliofanya kuwa mashuhuri ambapo hata wataalamu wa mashairi waliyatumia mashairi yake. Kitabu cha ‘Maqaamaat’ ni moja ya athari zinazonasibishwa kwa malenga huyo. Katika kitabu hicho Ibn Naqiya, alizungumzia maovu ya kijamii kupitia hekaya na tenzi. Athari nyingine inayonasibishwa kwa msomi huyo wa Kiislamu, ni kitabu kinachoitwa ‘Al-Jamaan fi Tashbiihaatil-Qur’an’ ambayo ni tafsiri nyepesi ya Qur’an Tukufu. Katika tafsiri hiyo Ibn Naqiya amefafanua aya 226.

Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita, mota ya kwanza ya umeme ilitengenezwa. Mvumbuzi na mtengenezaji wa mota hiyo alikuwa Thomas Edison mtaalamu na mtafiti wa Kimarekani. Kwa kutumia mota hiyo ya umeme, Edison alianzisha kiwanda cha umeme katika mji wa New York na wakati huo huo akawa amefanikiwa kudhamini sehemu ya mahitaji ya mwanga katika mji huo. Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kwamba, mwaka 1879, Edison alifanikiwa kuvumbua balbu.
Tarehe 4 Septemba miaka 111 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Richard Wright. Baada ya mashaka makubwa maishani, Richard Nathaniel Wright alianza kazi ya uandishi akiwa na umri wa miaka 30. Baadhi ya vitabu vyake vinaakisi sehemu ya maisha ya kifukara na ya kuchosha ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. Ameandika vitabu vingi kama Black Boy, Native Son, Uncle Tom's Children na The Outsider.
Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, tabibu Alexander Fleming alivumbuliwa dawa ya penicillin. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu wa nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 Miladia katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasi wasi mkubwa.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, maandamano ya kwanza ya mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa Shah yalifanyika hapa nchini. Maandamano hayo yalifanyika baada ya Swala ya Idi na yalianzia katika vituo au nukta nne tafauti mjini Tehran na yakapata idadi kubwa zaidi ya watu kadiri muda ulivyosonga mbele. Waandamanaji hao ambao walikuwa wamebeba mabango pamoja na picha kubwa za Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, walisikika wakipiga nara za kutaka uhuru, kujitawala na kuundwa mfumo wa utawala wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu.