Oct 02, 2019 04:12 UTC
  • Jumatano tarehe Pili Oktoba 2019

Leo ni Jumatano tarehe 3 Safar 1441 Hijria sawa na tarehe Pili Oktoba mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharifu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa.

Tarehe Pili Oktoba miaka 115 iliyopita alizaliwa Graham Greene mwandishi wa Uingereza. Mwandishi huyo aliakisi matendo mema na mabaya katika athari zake na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene ameacha vitabu vingi na baadhi ni 'Mtu wa Tatu', 'Utawala Unaotisha' na Muuaji wa Kukodishwa'. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.

Graham Greene

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita sawa na tarehe Pili Oktoba 1941, Adolf Hitler kiongozi wa Ujerumani ya Kinazi alitoa amri ya kuanza kwa shambulizi la pili la jeshi la Ujerumani dhidi ya Urusi ya zamani. Kwenye vita vya kwanza dhidi ya Urusi vilivyoanza tarehe 22 Juni 1941, Ujerumani iliikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Urusi. Lengo la kufanywa shambulio hilo la Dikteta Hitler, lilikuwa kurahisisha operesheni za kijeshi, kudhoofisha nguvu za Jeshi Jekundu na kudhibiti ardhi zaidi ya Urusi, hasa Moscow mji mkuu wa nchi hiyo.

Adolf Hitler

Na miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba 1958, nchi ya Guinea Conakry ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno walianza kumiminika nchini Guinea mwishoni mwa karne ya 15, na mwanzoni mwa karne ya 19, Wafaransa walipata satua zaidi nchini humo. Mwaka 1849 nchi hiyo ilikoloniwa rasmi na Ufaransa. Guinea Conakry inapakana na nchi za Senegal, Mali, Ivory Coast, Liberia, Sierra Leone na Guinea Bissau.

Bendera ya Guinea Conakry