Oct 09, 2019 02:31 UTC
  • Jumatano, tarehe 9 Oktoba, 2019

Leo ni Jumatano tarehe 10 Safar 1441 Hijria sawa na Oktoba 9 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 1112 iliyopita, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Iran, Abul-Fadhl Balaami. Balaam alikuwa mtu wa Bukhara, moja ya miji maarufu ya nchi ya Uzbekistan ya leo. Alifahamika kwa jina la Balaami kutokana na mmoja wa mababu zake kuishi mji wa Balaam, huko Asia ya Kati. Abul-Fadhl Balaam alikuwa waziri mwenye hekima na msomi mkubwa enzi za utawala wa Samanid, ambapo aliandika vitabu mbalimbali. Kitabu cha tarjama ya ‘Taarikh Twabari’ ni moja ya vitabu vinavyonasibishwa na msomi huyo na kilichopata umashuhuri katika karne ya nne Hijiria. Kitabu kingine maarufu cha msomi huyo ni ‘Taarikh Balaam’ ambapo ameashiria masuala mbalimbali ya historia.

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, mwafaka na tarehe 9 Oktoba 1962, nchi ya Uganda ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Kuanzia mwaka 1890 Uganda ilikuwa nchini ya makampuni ya Kiingereza yaliyokuwepo Afrika Mashariki, na baada ya kupita miaka kadhaa, ikatawaliwa rasmi na Uingereza. Baada ya kutawaliwa na mkoloni Mwingereza, wananchi wa Uganda walipigania uhuru na hatimaye kufanikiwa kujipatia uhuru wao mwaka 1962 katika siku kama ya leo.

Bendera ya Uganda

Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Ernesto Che Guevara mwanamapinduzi mashuhuri wa Amerika ya Latini pamoja na wenzake kadhaa. Che Guevara alizaliwa mwaka 1928 nchini Argentina. Fikra ya Ernesto Che Guevara ya kuendesha mapambano dhidi ya ubepari ilizidi kupanuka baada ya kushuhudiwa umaskini na ubaguzi uliotokana na siasa za kipebari za Marekani za kuyanyonya mataifa ya Amerika ya Latini. Ernesto che Guevara alifahamiana na Fidel Castro huko Mexico na viongozi hao wawili ndio walioongoza mapinduzi ya Cuba hadi kupatikana ushindi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Cuba mwaka 1959, Che Guevara alielekea Bolivia na kuasisi kundi la wapiganaji wa msituni. Alianza kupambana na serikali ya nchi hiyo iliyokuwa tegemezi kwa Marekani. Lakini katika siku kama ya leo mwaka 1967, wanajeshi wa Bolivia wakisaidiwa na shirika la ujasusi la CIA waligundua maficho ya Che Guevara na kumuuwa kwa kummiminia risasi.

Ernesto Che Guevara

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Majid Abu Sharar, shakhsiya mwingine wa Palestina aliuawa na utawala haramu wa Israel nchini Italia. Abu Sharar ambaye alikuwa afisa wa kampeni wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO aliuawa na vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mosad mjini Roma, Italia. Israel imekuwa ikitumia njia ya kuwauwa kigaidi shakhsiya mbalimbali wa Palestina kama moja ya njia zake kuu za kusitisha mapambano ya ukombozi ya Wapalestina.

Majid Abu Sharar

 

Tags