Oct 11, 2019 02:44 UTC
  • Ijumaa tarehe 11 Oktoba 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 12 Safar 1441 Hijria sawa na tarehe 11 Oktoba 2019.

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, vilianza vita vya umwagaji damu kati ya wazungu wa Kiholanzi kwa jina la Boers wakazi wa Afrika Kusini na Waingereza. Wanajeshi wa Uingereza waliwasili Afrika Kusini mwaka 1841 lengo likiwa ni kuikoloni Afrika. Waingereza walidhibiti Afrika Kusini baada ya kujenga maeneo ya kiraia nchini humo. Wahamiaji wengine kutoka Ulaya hususan Waingereza walimiminika huko Afrika Kusini baada ya kugunduliwa madini ya dhahabu na Almasi. Wazungu wa Uholanzi yaani Maboers waliwasili Afrika Kusini katika karne ya 19 na kupinga kuwasili wahamiaji wapya nchini humo. Sababu hiyo ilipelekea kuanza vita kati ya Wazungu hao na wahamiaji wa Kiingereza, lakini uungaji mkono wa serikali ya Uingereza kwa wahamiaji hao, ulitoa pigo kwa Maboers na kwa msingi huo Afrika Kusini ikaloloniwa na Uingereza.

Bendera ya Afrika Kusini

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita alifariki dunia Jean Henri Fabre msomi wa elimu ya sayansi na bingwa wa elimu ya wadudu au entomolojia. Fabre alizaliwa mwaka 1823 nchini Ufaransa. Msomi huyo ambaye pia alikuwa mwandishi amefanya utafiti mkubwa na kuandika vitabu kadhaa kwenye uwanja wa elimu ya wadudu.

Jean Henri Fabre

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Haji Mirza Khalil Kamarei, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mhadhiri wa chuo kikuu. Ayatullah Kamarei alijifunza elimu za fiqih, usul-fiqih na masomo mengine ya kidini katika Hauza ya kielimu ya mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baadaye alianza kufundisha falsafa. Haji Kamarei ameandika vitabu vingi kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni tafsiri ya Qur'ani, sherhe ya Nahjul Balagha na kitabu cha maisha ya Imam Hussein (as) na mashahidi wengine wa Karbala.

Ayatullah Haji Mirza Khalil Kamarei

Na 11 Oktoba mwaka 1991 yaani siku kama ya leo miaka 28 iliyopita shughuli za Shirika la Ujasusi la Urusi ya zamani (KGB) zilifikia kikomo muda mfupi baada ya kusambaratika nchi hiyo. KGB iliundwa mwaka 1954 kwa lengo la kukabiliana na harakati zilizokuwa na lengo la kuuangusha mfumo wa Kikomonisti wa Urusi ya zamani. Shirika hilo aidha lilikuwa na majukumu kama vile kuwakandamiza wapinzani wa chama cha Kikomonisti na kuendesha operesheni za kijasusi na zile zilizo dhidi ya ujasusi ndani na nje ya Muungano wa Kisovieti.

KGB