Nov 09, 2019 03:15 UTC
  • Jumamosi, 9 Novemba, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1441 Hijria mwafaka na tarehe 9 Novemba 2019 Miladia.

Siku kama ya miaka 148 iliyopita, alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allama Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikwea kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia. ***

Allama Agha Bozorge Tehrani (aliyeko katikati)

 

Miaka 142 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa nchini Pakistan Allama Muhammad Iqbal Lahori mwandishi, mwanafikra na malenga mzungumza lugha ya Kifarsi. Baada ya kumaliza masomo yake ya juu, Iqbal Lahori alielekea katika nchi za Ujerumani na Uingereza kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu zaidi katika taaluma ya falsafa. Alianza kusoma mashairi akiwa kijana na shairi lake la kwanza alilipa jina la 'Naleh Yatim' kwa maana ya kilio cha yatima. Allama Iqbal Lahori alikuwa mwanaharakati pia aliyepambana kwa minajili ya kuikomboa Pakistan kutoka mikononi mwa India. Allama Muhammad Iqbal alifariki dunia mwaka 1938. ***

Allama Muhammad Iqbal Lahori

 

Katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita sawa na tarehe Tisa mwezi Novemba mwaka 1918, mfumo wa jamhuri ulitangazwa huko Ujerumani kufuatia kushindwa mara kadhaa jeshi la nchi hiyo na vikosi vya waitifaki katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kuzuka uasi nchini humo. Matukio hayo yalipelekea kujiuzulu Wilhelm wa Pili mtawala wa mwisho wa kifalme wa nchi hiyo. Siku mbili baadaye mfalme huyo alikimbilia Uholanzi na hivyo utawala wa kifalme ukawa umehitimishwa nchini Ujerumani. Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kufutwa utawala wa kifalme, Friedrich Ebert alishika madaraka ya nchi kama rais wa kwanza wa nchi hiyo. ***

Wilhelm II

 

Katika siku kama ya leo miaka 87 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Hassan Sadr mmoja wa maulama mahiri wa Kiislamu. Alikuwa mmoja wa mafakihi ambao walipata daraja ya Ij’tihad katika kipindi cha ujana. Sayyid Hassan Sadr alikuwa katika orodha ya walimu mashuhuri katika Chuo KIkuu cha Kidini mjini Najaf Iraq. Aliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Sadruddin katika elimu ya fikihi, Usul, Itikadi, falsafa na hadithi. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Sayyid Hassan Sadr ni Tahsil al-Furu’u al-Diniyyah fi Fikih al-Imamkiyah na Taasis al-Shiyah.***

Sayyid Hassan Sadr

 

Miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abdul Aziz bin Saud mfalme wa kwanza wa Saudi Arabia na mwasisi wa nchi hiyo. Abdul Aziz bin Saud ambaye ni mwasisi wa utawala wa kifamilia wa Aal Saud nchini Saudi Arabia, alizaliwa tarehe 15 Mei 1880. Mtawala huyo alikuwa kibaraka wa Uingereza na tangu awali alikuwa na tamaa ya kutawala nchini Saudi Arabia hususa katika maeneo matakatifu ya Makka na Madina. ***

Abdul Aziz bin Saud

 

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, nchi ya Cambodia ilijkomboa kutoka katika makucha ya mkoloni Mfaransa na kujitangazia uhuru. Kijiografia Cambodia ipo kusini mashariki mwa Asia. Akthari ya wananchi wa Cambodia ni wa jamii ya Khmer na wanazungumza lugha ya Kikhmer. Kuanzia karne ya 8 hadi 13 Miladia, Cambodia ilikuwa nchi yenye nguvu ambapo mbali na ardhi ya sasa ya nchi hiyo, sehemu kubwa ya ardhi ya Thailand, Laos na Vietnam ilikuwa katika udhibiti wan chi hiyo. ***

Bendera yay Cambodia

 

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, Charles de Gaulle mwanajeshi, mwanasiasa mashuhuri na Rais wa zamani wa Ufaransa aliaga dunia.Jenerali Charles André Joseph Marie de Gaulle aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri na shakhsia muhimu wa kijeshi nchini Ufaransa alizaliwa Novemba 22 mwaka 1890 katika mji wa Lille. Mwaka 1940 aliteuliwa kuwa jenerali kijana zaidi katika Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa. Baada ya majeshi ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani katika vita, Charles de Guelle alikimbilia Uingereza na kuongoza harakati za mapambano ya Ufaransa. ***

Charles de Gaulle

 

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopiita, Sheikh Nusratullah Ansari mwanamapambano wa Kimapinduzi wa Iran alikufa shahidi kutokana na mateso ya makachero wa Shirika la Usalama wa Taifa la utawala wa Shah lililojulikana kwa jina la SAVAK. Hujjatul Islam Nusratullah Ansari alizaliwa huko Buin Zahra. Sambamba na masomo yake ya Hawza alikuwa akiendesha pia harakati za mapambano ya kisiasa dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Shah nchini Iran. Hatimaye alitiwa mbaroni mwaka 1354 Hijria Shamsia na kufa shahidi katika siku kama ya leo baada ya miezi sita ya mateso. ***

Hujjatul Islam Sheikh Nusratullah Ansari

 

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Will Durant mwandishi na mwanafalsafa mashuhuri wa Marekani. Msomi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 96. Durant alizaliwa katika jimbo la Massachusetts huko Marekani. Alihitimu masomo yake kwa kupata daraja ya uzamivu (PhD) katika taaluma ya falsafa na kuanza kufundisha. Mwaka 1926 Will Durant alifanikiwa kusambaza kitabu chake cha The Story of Philosophy. Baadhi ya vitabu vingine vya Will Durant ni The Age of Faith, The Life of Greece na The Age of Napoleon.

Will Durant

 

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, ukuta wa Berlin ambao ulikuwa ukiugawa mji huo katika sehemu mbili za mashariki na magharibi kwa kipindi cha miaka 28 hatimaye ulivunjwa. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa mji huo lilikuwa likidhibitiwa na Urusi ya zamani, huku eneo la magharibi likidhibitiwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Machafuko yaliyotokea mjini Berlin hapo mwaka 1961 na wakazi wa mashariki kukimbilia upande wa magharibi, kulizitia wasiwasi serikali za Urusi ya zamani na Ujerumani mashariki, suala lililozipelekea nchi hizo kujenga ukuta huo ambao baadaye ulionekana kuwa nembo ya kuwaganywa Ujerumani. Hata hivyo kuporomoka kwa Urusi ya zamani ambako kuliacha taathira kubwa pia katika tawala za kikomunisti za Ulaya mashariki kulipelekea kuvunjwa ukuta huo wa Berlin hapo mwaka 1989.

Ukuta wa Berlin