Jumatatu tarehe 11 Novemba mwaka 2019
Leo ni Jumatatu tarehe 13 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1441 Hiria sawa na Novemba 11 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, aliaga dunia Yasser Arafat Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa. Alizaliwa mwaka 1929 na kuanza harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel akiwa katika rika la ujana. Mwaka 1946, Yasser Arafat alielekea nchini Misri kwa ajili ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Cairo na miaka mitano baadaye alihitimu masomo katika taaluma ya Usanifu Majengo. Mwaka 1965 alirejea Palestina na kuasisi Harakati ya Fat-h ili kupambana na utawala wa Tel Aviv. Miaka minne baadaye alichukua hatamu za kuongoza PLO hadi alipoaga dunia.
Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo, Angola ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Wakoloni wa Kireno kwa mara ya kwanza waliingia katika ardhi ya Angola mwaka 1483 Miladia. Wakati huo, ardhi ya Angola ilikuwa sehemu ya ufalme wa Kongo, Zaire ya zamani.
Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, virusi vinavyosababisha maradhi hatari ya kupooza viungo vya miili ya watoto yaani Polio viligunduliwa. Virusi hivyo vilipewa jina la virusi vinavyolemaza watoto kwa sababu ya kuwashambulia zaidi watoto wadogo na kuwapoozesha viungo vyao vya mwili. Baadaye kidogo mwanasayansi Dakta Jonas Salk aliyegundua virusi vya Polio alifanikiwa pia kugundua chanjo yake.
Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, Vita vya Kwanza vya Dunia vilifikia kikomo baada ya kutiwa saini mkataba wa kuacha vita hivyo. Vita vya Kwanza vya Dunia vilipiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 kati ya nchi waitifaki yaani serikali za Russia, Uingereza, Ufaransa na Italia kwa upande mmoja, na nchi za Ujerumani, Bulgaria, Utawala wa Othmania na ufalme wa Austria na Hungary kwa upande wa pili. Watu zaidi ya milioni 15 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 20 kujeruhiwa. Vilevile vilisababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150 kwa nchi zilizopigana vita hivyo.
Na katika siku kama ya leo miaka 1151 alizaliwa Qadhi Jorjani maarufu kwa lakabu ya Abulhassan, faqihi, mwandishi na malenga wa Kiislamu. Jorjani alipata masomo ya kidini kwa Qadhi Mkuu wa mji wa Rei ulioko karibu na Tehran ya leo. Qadhi ameandika vitabu vingi kama "Tafsirul Qur'an" na "Tahdhib al Tarikh". Qadhi Jorjani alifariki dunia mwaka 366 Hijria huko Neishabur na akazikwa Jorjan au Gorgan ya leo kaskazini mashariki mwa Iran.