Alkhamisi tarehe 16 Januari 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari 16 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 759 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Jamadil Awwal 682 Hijria, alizaliwa Muhammad bin Hassan Hilli mwenye lakabu ya Fakhrul Muhaqqiqiin katika mji wa Hilla nchini Iraq. Muhaqqiq Hilli alibobea na kutabahari kwenye elimu za Tafsiri ya Qur’ani, Fiqh na Usulul Fiqh. Mwanachuoni huyo alipata elimu ya kidini kutoka kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameandika vitabu vingi miongoni mwavyo ni "Sharh Mabadiul Usul", "Tahswilul Najat" na “al Kafiya”." Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 771 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 704 iliyopita yaani tarehe 20 Jamadil Awwal mwaka 737 alifariki dunia faqihi wa Kiislamu Abu Abdullah Muhammad ibn Hajj al-Abdari al-Fasi mashuhuri kwa jina la Ibn Hajj. Al Fasi awali alipata elimu kwa maulamaa wa mji wa Fas huko Morocco ya leo. Baadaye alielekea Cairo na kuishi huko hadi mauti yalipomfika. Faqihi Abu Abdullah al Fasi ameandika vitabu vingi vya thamani kikiwemo kile cha al Mad-khal. Katika kitabu hicho, Ibn Hajj amechunguza masuala mbalimbali yakiwemo ya kiakhlaqi, kifiqi, kijamii na kiuchumi.

Katika siku kama ya leo miaka 174 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Januari 1846, vilianza vita baina ya Marekani na Mexico baada ya Washington kuishambulia nchi hiyo. Vita hivyo vilivyochukua muda wa miaka miwili, vilitokea baada ya Marekani kudai kwamba wahajiri wa nchi hiyo wanateswa nchini Mexico. Hata hivyo ukweli ni kuwa, Marekani ilianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuyatwaa baadhi ya maeneo ya Mexico hususan eneo la Texas. Katika vita hivyo, Marekani iliyakalia kwa mabavu majimbo ya Texas, California, Nevada, Utah, Arizona na New Mexico.
Miaka miaka 63 iliyopita katika siku sawa na ya leo alifariki dunia mtunzi wa nyimbo mwenye asili ya Italia kwa jina la Arturo Toscanini. Toscanini alizaliwa mwaka 1867 na alianza kupenda muziki akiwa kijana. Arturo Toscanini alikuwa kiongozi wa bendi baada ya kufanya mazoezi mengi na kusafiri katika nchi mbalimbali duniani. Aidha alipata umashuhuri kutokana uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi na kuwa makini katika utunzi wa nyimbo. Toscanini aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90 yaani miaka mitatu baada ya kustaafu kazi ya muziki.
Tarehe 26 Dey 1357 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi, mfalme wa mwisho wa Iran alitoroka nchini kwa kisingizio cha kwenda kupata matibabu nje ya nchi, baada ya kushadidi wimbi la harakati za mapinduzi. Muhammad Reza Pahlavi alichukua kiti cha ufalme mwaka 1320 Hijria Shamsia baada ya serikali ya Uingereza kumpeleka uhamishoni baba yake, Reza Shah, kwa sababu aliiunga mkono Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Siku chache kabla ya tukio hilo, Imam Ruhullah Khomeini ambaye wakati huo alikuwa Ufaransa, alitoa ujumbe mzito akisema kuwa: "Safari ya Shah bila ya kung’atuka madarakani haitabadilisha lolote na utawala wa kifalme nchini Iran unapaswa kuangushwa kikamilifu".
Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita Rais Laurent Desire Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alipigwa risasi na mmoja wa walinzi wake katika ikulu ya Rais na kujeruhiwa vibaya. Baada ya tukio hilo kulienea habari za kutatanisha juu ya hatima ya kiongozi huyo. Tarehe 18 Januari yaani siku mbili baadaye, serikali ya Kinshasa ilithibitisha kufariki dunia Rais Laurent Desire Kabila . Kabila alizaliwa mwaka 1939 huko Katanga na kupata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania. Aliingia madarakani mwaka 1997 baada ya vikosi vya askari aliokuwa akiwaongoza kuuteka mji wa Kinshasa na kumlazimisha Mobutu Sese Seko, rais wa wakati huo wa Zaire ya zamani kukimbilia nje ya nchi. Tarehe 26 Januari Joseph Kabila mwana wa Rais Kabila alishika hatamu za uongozi nchini Congo.