Feb 20, 2020 04:22 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 20 Februari, 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 25 Jamadithani 1441 Hijria sawa na Februuari 20 mwaka 2020.

Katika siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, vita kati ya Ufaransa na wapigania uhuru wa Mexico vilimalizika kwa ushindi wa Ufaransa na kushika hatamu za uongozi mwanamfalme wa Austria, Maximilian. Katika vita hivyo vilivyoendelea kwa kipindi cha miaka 5, awali Ufaransa iliungana na Uhispania na Uingereza na baada ya muda mfupi nchi hizo mbili zilijitenga na Ufaransa ambayo iliendeleza vita dhidi ya wapigania uhuru wa Kimexico waliokuwa wakiongozwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Benito Juárez. Benito Juárez aliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni wa Kifaransa hata baada ya kurudi nyuma na kukimbilia katika maeneo ya milimani ya Mexico. Kiongozi huyo hatimaye alifanikiwa kuangusha utawala wa Maximilian akisaidiwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo.

Benito Juárez

Katika siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Februari 1947, Uingereza hatimaye ilikubali kuipatia India uhuru wake baada ya kuikoloni nchi hiyo kwa zaidi ya karne mbili. Uhuru wa India ulipatikana kutokana na mapambano ya muda mrefu yaliiyoongozwa na Mahatma Gandhi. Katika kipindi chote cha utawala wake wa kikoloni huko India, Uingereza ilipora utajiri na maliasili za nchi hiyo na kuwasababishia hasara kubwa raia wa India. Mwezi Agosti mwaka huohuo India ikajipatia rasmi uhuru wake na ikagawanyika katika nchi mbili za India na Pakistan.

Bendera ya India

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi Esfand 1366 Hijria Shamsia, ndege moja ya abiria ya Iran ilishambuliwa na kutunguliwa kwa kombora la majeshi ya utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein wa Iraq na kuangushwa, wakati wa vita vya Iran na Iraq. Katika tukio hilo, Hujjatulislam Fadhlullah Mahallati, mwakilishi wa Imam Khomeini kwenye Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) aliuawa shahidi akiwa pamoja na maafisa wa serikali na wabunge 39 wa Iran.

Hujjatulislam Fadhlullah Mahallati

Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 25 Jamadithani mwaka 1415 Hijria alifariki dunia Ayatullah Muhammad Ali Araki, mmoja wa marjaa wakubwa wa taqlidi wa Waislamu akiwa na umri wa miaka 103. Mwanzuoni huyo wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Arak katikati mwa Iran na tangu akiwa na umri mdogo alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza elimu ya dini. Ayatullah Muhammad Ali Araki kwa muda mrefu alifundisha katika chuo kikuu cha kidini cha Qum na miongoni mwa vitabu vyake ni risala ya Ijitihadi na Taqlidi pamoja na Sherhe ya Uruwatul Uthqaa.

Ayatullah Muhammad Ali Araki

Na tarehe 20 Februari miaka 4 iliyopita aliaga dunia Sheikh Ahmad A'mir, qari na msomaji maarufu wa Qur'ani tukufu wa Misri. Alizaliwa mwaka 1927 katika eneo la Salihiyah huko mashariki wa Misri na kuhifadhi Qur'ani yote akiwa bado mdogo. Baadaye alijiunga na jeshi na mwaka 1963 alifanya kazi kwenye radio ya nchi hiyo.

Qari huyo mashuhuri wa Misri alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kusoma Qur'ani na alifika nchini Iran mara kadhaa katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu kama jaji wa mashindano hayo. Mara ya mwisho msomaji huyo mkubwa wa Qur'ani alitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka 2013 na kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu. Baada ya mashindano hayo, Sheikh Ahmada A'mir alisoma Qur'ani katika majlisi iliyohudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei wakati huo akiwa na umri wa miaka 86. Qiraa ya Sheikh Ahmad A'mir katika majlisi hiyo iliwagusa sana hadhirina na kuwafanya wengi wabubujikwe na machozi.

Ayatullah Muhammad Ali Araki

 

Tags