May 08, 2020 23:59 UTC
  • Jumamosi, 9 Mei, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 15 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1441 Hijria, mwafaka na tarehe 9 Mei 2020 Miladia.

Miaka 1438 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, katika mwaka wa Tatu Hijria  alizaliwa Imam Hassan al-Mujtaba (as), mmoja wa Ahlul-Bait wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Imam Hassan (as) alikulia na kupata malezi na usimamizi wa babu yake Bwana Mtume SAW, mama yake Bibi Fatimatul Zahra binti ya Mtume na baba yake, yaani Imam Ali (as). Baada ya kuuawa shahidi baba yake mwaka wa 40 Hijiria, mtukufu huyo alifanya kazi kubwa ya kusimamia na kuwaongoza Waislamu. Mwanzoni Waislamu wengi walimbai na kumpa mkono wa utiifu Imam Hassan, lakini mfumo wa utawala wa Bani Umayyah uliokuwa ukiongozwa na Muawiya mwana wa Abu Sufiyan ambao wakati huo ulikuwa na nguvu kubwa, ulianzisha uadui na chuki dhidi ya Imam huyo. Hatimaye Imam Hassan (as) alijiandaa kukabiliana na Bani Umayyah, lakini viongozi wengi wa jeshi lake walidanganyika na ahadi za uongo za maadui na kumuacha peke yake Imam, hali iliyomlazimisha mtukufu huyo kufanya suluhu na mtawala huyo wa Bani Umayyah kwa lengo la kuilinda na kuinusuru dini tukufu ya Uislamu. ***

 

Siku kama ya leo miaka 1058 iliyopita yaani tarehe 15 Ramadhani  mwaka wa 383 Hijria aliaga dunia katika mji wa Nishabur kaskazini mashariki mwa Iran Abubakar Muhammad bin Abbas "Kharazmi" aliyekuwa msomi na mwanafasihi mtajika wa Kiislamu. Kharazmi alikuwa hodari mno wa kubainisha mambo kwa ghibu na alikuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mashairi na historia ya Waarabu. Abubakar Muhammad bin Abbas Kharazmi ameacha athari iitwayo "Rasail" ambayo ni tunu kubwa katika fasihi ya Kiarabu na ambayo ni maarufu kwa jina la Rasail Kharazmi. ***

Abubakar Muhammad bin Abbas "Kharazmi"

 

Katika siku kama ya leo miaka 367 iliyopita, kazi ya ujenzi wa jengo la Taj Mahal linalohesabiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kuvutia zaidi duniani na moja kati ya mifano bora zaidi ya usanifu majengo wa Kiislamu huko India ilimalizika baada ya miaka 22. Ujenzi wa jengo la Taj Mahal ulianza baada ya kufariki dunia mke wa Shah Jahan, mfalme wa India huko katika jimbo la Agra. Jengo hilo lilijengwa kwa kutegemea ramani iliyochorwa na msanifu majengo mashuhuri wa Iran, Issa Isfahani. Kwa upande wa nje, jengo la Taj Mahal limenakshiwa kwa ustadi kwa rangi mbalimbali huku kuta zake zikiwa zimeandikwa maandishi ya Kiarabu yenye aya za Qur'ani Tukufu. Ndani ya jengo hilo kuna makaburi mawili ya mfalme Shah Jahan na mkewe, Nur Jahan. ***

Taj Mahal

Tarehe 9 Mei miaka 215 iliyopita aliaga dunia mwandishi, malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kijerumani kwa jina la Johann Christoph Friedrich von Schiller akiwa na umri wa miaka 46. Von Schiller alipenda sana masuala ya uandishi tangu utotoni mwake. Friedrich Von Schiller alikuwa hodari katika fasihi ya Kijerumani na anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waandishi mahiri wa Kijerumani katika uga wa fasihi. ***

Johann Christoph Friedrich von Schiller

 

Na miaka 104 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Mei, mkataba wa kihistoria wa Sykes-Picot ulitiwa saini na wawakilishi wa Uingereza, Ufaransa na Urusi ya zamani. Hata hivyo Umoja wa Kisovieti baadaye ulijitoa kwenye makubaliano hayo baada ya mapinduzi ya Bolshevik. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, tawala za Uingereza na Ufaransa ziligawana nchi za Kiarabu zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Kiothmania. Kwa msingi huo Iraq na Jordan zikawa chini ya udhibiti wa Uingereza huku Syria na Lebanon zikitawaliwa na Ufaransa. ***

Mkataba wa kihistoria wa Sykes-Picot

 

Tags