May 14, 2020 17:08 UTC
  • Alkhamis, tarehe 14 Mei, 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Ramadhani 1441 Hijria, sawa na tarehe 14 Mei, 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1433 iliyopita sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka wa 8 Hijiria, jeshi la Kiislamu lililokuwa na wapiganaji elfu kumi chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (saw) liliukomboa mji wa Makka. Mtume Mtukufu alichukua hatua hiyo baada ya makafiri kukiuka makubaliano ya amani ya Hudaibiya ambayo yalisainiwa mwaka wa Sita Hijria kati yake na wakuu wa Makuraishi. Mtume Muhammad (saw) alitoa msamaha kwa wakazi wote wa Makka baada ya kukombolewa mji huo katika hali ambayo huko nyuma watu hao walikuwa wakipinga na kupiga vita Uislamu na pia walimuudhi mno Mtume na kuwatesa Waislamu. Muamala huo wa huruma na upendo wa Mtume (saw) uliwavutia watu wa kabila la Kuraishi na kuwafanya waingie kwa wingi katika dini tukufu ya Uislamu. Kwa msingi huo mji wa Makka ulikombolewa pasina kuwepo umwagaji damu.

Kukombolewa mji wa Makka

Siku kama ya leo miaka 899 iliyopita, yaani sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 542 Hijiria, alifariki dunia Ibn Shajari Baghdadi, fasihi na mtaalamu wa elimu ya nahau wa Kiislamu. Abu Sa'adat Hibatullah Ibn Ali Alawi Hassani, mtaalamu wa nahau, lugha ya Kiarabu, fasihi na malenga wa Kishia, alizaliwa mwaka 450 Hijiria. Nasaba ya msomi huyo inarejea hadi kwa Imam Hassan (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) na ni kwa ajili hiyo ndio maana akaitwa Alawi, Hassani. Akiwa kijana alianza kusomea fasihi, nahau, hadithi na elimu mbalimbali za zama zake na kamwe hakuwahi kuacha kusoma, kama ambavyo hata alipokuwa mzee, bado aliendelea kujifunza kwa wasomi wa zama zake. Aidha alifundisha lugha ya nahau kwa kipindi cha miaka 70 ambapo alitokea kupata wanafunzi mashuhuri katika uwanja huo. Miongoni kwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Al-Aamaal' 'Al-Hamaasah' na 'Mandhumat Ibn Shajarah.' Hatimaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 92 mjini Baghdad Iraq na kuzikwa mjini hapo.

Ibn Shajari Baghdadi

Siku kama ya leo miaka 815 iliyopita, sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 626 Hijiria, alifariki dunia Yaqut Hamawi mmoja wa waandishi na wasomi tajika wa Kiislamu wa karne ya Saba Hijria na alikuwa mtaalamu mashuhuri wa jiografia. Alizaliwa mwaka 539 Hijria huko Baghdad ambapo ujanani mwake alikamatwa mateka na kufanywa mtumwa. Hata hivyo baada ya kupita muda mfanyabiashara mmoja wa Baghdad alimnunua Hamawi na baadaye akamuachia huru. Miongoni mwa athari za uandishi za Yaqut Hamawi tunazoweza kuziashiria ni vitabu vyake viwili alivyovipa majina ya "Mu'jamul-Buldan" na Mu'jamul- Udabaa."

Yaqut Hamawi

Siku kama ya leo miaka 767 iliyopita, sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 674 Hijiria, alifariki dunia Ibn Saai Baghdadi, fasihi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Sheikh Tajud-Din Abu Twalib Ali Ibn Anjub Ibn Uthman Baghdadi, Maarufu kwa jina la Ibn Saai, alizaliwa mwaka 593 mjini Baghdad, Iraq. Awali alianza kujifunza elimu za zama zake kwa walimu mbalimbali na kuibukia kielimu. Kwa miaka kadhaa Ibn Saai alisimamia maktaba ya utawala wa wakati huo mjini Baghdad na ambayo ilitumiwa kwa ajili ya kutwalii. Na baada ya Baghdad kudhibitiwa na silsila ya utawala wa Wamongolia, hatimaye Ibn Saai Baghdadi aliteuliwa na Nasir al-Din al-Tusi kwa ajili ya kusimamia maktaba mbalimbali za mji huo. Ni katika kipindi hicho ndipo akatokea kuwa mwandishi mkubwa, jambo ambalo lilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha. Kitabu cha 'al-Khulafaau' ni miongoni mwa athari mashuhuri za Ibn Saai. Aidha ameandika kitabu cha 'Akhbaarul-Udabaa' 'Akhbaarul-Hallaj' na 'Akhbaaru Qudhaatu Baghdad.' Abin Saai, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 na kuzikwa mjini Baghdad.

Ibn Saai Baghdadi.

Siku kama ya leo miaka 445 iliyopita, sawa na tarehe 14 Mei 1575 Miladia, ardhi ya Angola ilikaliwa kwa mabavu na mkoloni Mreno. Kabla ya Wareno kuwasili Angola, ardhi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Kiafrika wa Guinea. Baada ya Wareno kuiteka nchi hiyo walianzisha vituo vya biashara katika maeneo yake yote ya pwani. Baada ya kumalizika vita vya Pili vya Dunia, harakati kadhaa zilianzishwa nchini Angola kwa lengo la kupigania uhuru wa nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1975 harakati za wapigania uhuru zilizaa matunda baada ya nchi yao kupata uhuru.

Ramani ya Angola

Siku kama ya leo miaka 224 iliyopita, sawa na tarehe 14 Mei 1796 Miladia, kwa mara ya kwanza ilifanyiwa majaribio nchini Uingereza chanjo ya ugonjwa wa ndui. Hata kama leo hususan katika nchi zilizoendelea kuna kiwango kidogo cha athari zinazotokana na ugonjwa huo, lakini hadi kufikia karne ya 18, maradhi hayo yalienea sana ndani ya mataifa hayo na kusababisha madhara makubwa. Mwaka 1717 mwanamke mmoja wa Uingereza alianzisha utafiti na uchunguzi mkubwa katika suala hilo, ambapo juhudi zake zilipunguza sana idadi ya waathirika wa maradhi hayo. Hatimaye tarehe 14 Mei mwaka 1796 Miladia, Dakta Edward Jenner aliifanyia majaribio chanjo ya ndui kupitia mwili wa mtoto mdogo na kutoa majibu mazuri.

Ugonjwa wa ndui

Siku kama ya leo miaka 209 iliyopita, sawa na tarehe 14 Mei 1811 Miladia, nchi ya Paraguay ilijipatia uhuru wake. Paraguay iligunduliwa katika karne ya 16 Miladia na Muhispania mmoja na ikawa chini ya utawala wa Uhispania kwa zaidi ya karne mbili. Baada ya uhuru nchi hiyo ilitawaliwa na serikali ya kidikteta na kushuhudiwa majaribio kadhaa ya mapinduzi na kila aliyeingia madarakani aliongoza kidikteta. Uchaguzi wa kwanza huru wa rais ulifanyika nchini humo mwaka 1989. Kijiografia Jamhuri ya Paraguay inapatikana huko Amerika Kusini baina ya nchi za Brazil, Argentina na Bolivia.

Bendera ya Paraguay

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, sawa na tarehe 14 Mei 1867 Miladia, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 74, Joseph Reinaud, msomi na mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufarasa. Kutokana na kupendelea sana lugha za eneo la Mashariki ya Kati, alianza kujifunza lugha na fasihi ya Kiarabu. Baada ya muda mfupi, Reinaud alianza kufundisha lugha hiyo katika chuo kikuu nchini Ufaransa. Aliandika vitabu kuhusiana na historia ya Uislamu ambapo moja ya vitabu hivyo ni 'Fat'hul-Arab' na 'Al-Islamu wal-Muslimin.

Joseph Reinaud

Na siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, sawa na tarehe 14 Mei 1955 Miladia, mkataba wa kisiasa na kijeshi wa Warsaw ulitiwa saini baina ya nchi nane za kikomonisti barani Ulaya. Makubaliano hayo yaliyojulikana kama The Warsaw Pact yalitiwa saini katika mji mkuu wa Poland, Warsaw, lengo lake lilikuwa ni kukabiliana na Mkataba wa Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi (NATO) uliotiwa saini na madola ya Magharibi waitifaki wa Marekani. Nchi zilizotia saini makubaliano hayo ziliahidi kutotumia nguvu na mabavu katika ushirikiano wao. Aidha zilikubaliana kwamba, kushambuliwa kijeshi mwanachama mmoja ni sawa na kuchokozwa nchi zote wanachama. Hatimaye baada ya miaka 36, mkataba huo ulifutwa mwaka 1991 baada ya nchi hizo kukutana huko Budapest mji mkuu wa Hungary.

Tags