Jul 06, 2020 02:28 UTC
  • Jumatatu tarehe 6 Julai 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 14 Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Julai 6 mwaka 2020.

Katika siku kama ya leo miaka 166 iliyopita alifariki dunia George Simon Ohm mwanahisabati na mwanafizikia wa Ujerumani akiwa na umri wa miaka 67. Simon Ohm alizaliwa mwaka 1789 na kuanza kupenda sana somo la fizikia na kufanikiwa kuvumbua kanuni katika uwanja wa umeme kutokana na utafiti mkubwa aliokuwa akiufanya katika uwanja huo. Alizipa kanuni hizo jina lake yaani "Ohm Laws". Kanuni ambazo zinatumiwa hadi leo hii.

George Simon Ohm

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, yaani tarehe 16 Tir 1301 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Rabbani Zinul Abidine Marandi. Msomi huyo mkubwa alisoma elimu za awali katika mji aliozaliwa wa Marand, huko katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki nchini Iran. Baada ya hapo alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Ayatullah Sayyid Mohammed Hassan Husayni Nouri Shirazi na Habib Allah Rashti. Baada ya muda fulani Ayatullah Marandi alikuwa marjaa taqlid katika maeneo ya Azerbaijan na hatimaye akafariki dunia siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 72 na kuzikwa katika makaburi ya Wadi-us-Salaam mjini Najaf.

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul-Huda Karbasi, msomi mkubwa wa fiqhi na masomo mengine ya kidini. Baada ya kuhitimu masomo ya awali ya dini ya Kiislamu alielekea mjini Najaf kwa ajili ya kukamilisha masomo yake ya kidini yapata mwaka 1281 Hijiria Shamsia, ambapo aliweza kusoma masomo ya ngazi ya juu ya usulu fiqhi na fiqhi kwa maulama wakubwa wa mji huo kama vile Ayatullah Akhund Mohammad Kazem Khorasani na Mohammed Kazem Yazdi. Aidha Ayatullah Mirza Abul-Huda Karbasi ameandika vitabu kadhaa kama vile 'Kifaayatul-Usul' 'al-Badrut-Tamaam' 'Zallatul-Aqdaam' na 'al-Fawaaidur-Rijaaliyah.'

Ayatullah Mirza Abul-Huda Karbasi

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, aliaga dunia mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. William alizaliwa mwaka 1897. Baada ya kushiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Faulkner alirejea tena nchini kwake. Alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Hadithi za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa leo nchini Marekani.

William Faulkner

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita nchi ya Kiafrika ya Malawi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kabla ya Malawi kupata uhuru, ilikuwa ikijulikana kwa jina la Nyasaland. Mwaka 1859, makundi ya Wamishonari kutoka Scotland wakiwa pamoja na mvumbuzi David Livingstone waliwasili Nyasaland na kufuatiwa na Uingereza. Uingereza iliunga mkono uvamizi wa Ujerumani na Ureno huko Nyasaland na hatimaye mwaka 1891 nchi hiyo ikawekwa chini ya mamlaka yake. Kwa utaratibu huo Nyasaland ambayo ni Malawi ya leo ikawa miongoni mwa makoloni ya Uingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika. Malawi iko kusini mashariki mwa Afrika ikipakana na Tanzania, Zambia na Msumbiji.

Nendera ya Malawi

Tarehe 6 Julai miaka 45 iliyopita, visiwa vya Comoro vilipata uhuru. Raia wengi wa visiwa vya Comoro walianza kuingia katika dini ya Kiislamu na kueneza utamaduni wa dini hiyo visiwani humo, baada ya wafanya biashara wa Kiislamu kuwasili visiwani humo katika karne ya 12 Miladia.Tangu karne ya 16 visiwa vya Comoro vilikuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno na baadaye Sultan wa Oman alifanikiwa kuhitimisha ukaliwaji mabavu wa visiwa hivyo. Hata hivyo mwaka 1842 sehemu kadhaa za visiwa hivyo ziliingia chini ya udhibiti wa Wafaransa na taratibu wakoloni hao wakaidhibiti ardhi yote ya nchi yote hiyo. Mapambano ya wananchi yalipelekea kutangazwa uhuru rasmi wa nchi ya Kiislamu ya Comoro mwaka 1975. Comoro ina ukubwa wa kilomita mraba 1862 huku ikipatikana kusini mashariki mwa bara la Afrika katika bahari ya Hindi.

Bendera ya Comoro