Jul 29, 2020 02:30 UTC
  • Jumatano tarehe 29 Julai mwaka 2020

Leo ni Jumatano tarehe 8 Dhulhija 1441 Hijria sawa na Julai 29 mwaka 2020.

Leo tarehe 8 Dhulhija ni Siku ya Tarwiya. Siku hii imepewa jina la Siku ya Tarwiya kwa maana ya kijitosheleza kwa maji kwa sababu katika zama za Nabii Ibrahim (as) maji yalikuwa hayapatikani katika jangwa na Arafat na kwa msingi huo watu walikuwa wakipeleka maji eneo la Arafat kutoka Makka tarehe 8 Dhulhija wakijitayarisha kwa ajili ya mahitaji ya maji ya kesho yake yaani tarehe tisa.  

Katika siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu wa Mtume SAW aliondoka Makka na kuelekea Kufa nchini Iraq baada ya kukataa kumbai na kutoa kiapo cha utiifu kwa Yazid bin Muawiya. Miezi minne kabla ya hapo, Imam Hussein alikuwa amewasili mjini Makka akiwa pamoja na familia yake na alikitumia kipindi cha kuweko waumini waliotoka katika pembe mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufanya ziara katika nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu, kuwaamsha na kuwabainishia dhulma na ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa wa utawala wa Yazid mwana wa Muawiya. Wakati huo huo kutokana na wito wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na njama za utawala wa Yazidi za kutaka kumuuwa, Imam Hussein aliondoka Makka na kueleka Kufa.

Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 29 Julai 1883, alizaliwa Benito Mussolini mwanasiasa, dikteta na mwasisi wa chama cha Kifashisti nchini Italia. Ufashisti ni utawala wa kidikteta uliojikita katika aidiolojia ya kibaguzi na kitaifa, kuwakandamiza wapinzani na kupotosha itikadi na fikra za wananchi. Mwaka 1922 Mussolini alinyakua wadhifa wa uwaziri mkuu wa Italia, na hivyo udikteta kuendelea kutawala nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler na kuandaa mazingira ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia.

Benito Mussolini

Tarehe 29 Julai miaka 63 iliyopita Umoja wa Mataifa ulianzisha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Lengo la kuasisiwa wakala huo lilikuwa kusimamia shughuli za vituo vya nyuklia kwa lengo la kuzuia uzalishaji na usambazaji wa silaha za nyuklia na kuzalisha silaha za maangamizi ya umati. Ofisi ya wakala huo iko mjini Vienna, Austria na maabara ya utafiti ya wakala huo katika mji huo, hutoa natija ya uchunguzi mbalimbali kuhusiana na matumizi ya nishati ya nyuklia kwa nchi wanachama. Hata hivyo kutokana na kwamba wakala huo umeathiriwa na madola makubwa, umekengeuka malengo yake na kufuata mielekeo ya kisiasa.

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Ali Akbar Faydh mashuhuri kwa jina la Ayatullah Mishkini. Ayatullah Mishkini alisoma kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Burujerdi na Imam Khomeini. Alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kujiunga na harakati ya mapambano ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah. Alitiwa nguvuni na kufungwa jela mara kadhaa sambamba na kubaidishwa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mishkini alishika nyadhifa mbalimbali, na muhimu zaidi ni ule wa Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi Zake. Alimu huyo ameandika vitabu vingi.

Ayatullah Mishkini

Tarehe 8 mwezi Mordad kwa mwaka wa Kiirani wa hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi mwanafalsafa, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu Shahabuddin Sohravardi aliyepewa lakabu ya Sheikhul Ishraq. Sheikhul Ishraq alizaliwa mwaka 549 Hijria karibu na mji wa Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Alibobea haraka katika taaluma nyingi za Kiislamu za wakati huo hususan falsafa. Sheikh Sohravardi alifanya safari katika miji mbalimbali ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu. Aliasisi mfumo mpya wa falsafa uliopewa jina la Ishraq. Sheikhul Ishraq ameandika vitabu vingi kama vile "Hikmatul Ishraq", al Mabda wal Maad", na "Talwihat".

Shahabuddin Sohravardi