Jumamosi, Septemba 5, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 16 Mfunguo Nne Muharram 1442 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe 5 Septemba 2020.
Siku kama ya leo miaka 182 iliyopita, hatimaye baada ya miaka 15 ya mapambano dhidi ya wavanmizi Wafaransa nchini Algeria Amir Abdul-Qadir al-Jazairi alitiwa mbaroni na wavanmizi hao. Sababu ya kushindwa Abdul-Qadir ni kuwa mwanamapambano huyo hakuwa na kambio na vituo vya kuendeshea harakati ndani ya Algeria. Maeneo yote ya nchi hiyo yalikuwa chini ya udhibiti wa wavamizi Wafaransa. Ndio maana alilazimika kuendesha harakari na mapambano yake katika maeneo ya mpakani na Algeria na Morocco. Amir Abdul-Qadir al-Jazairi alifungwa jela kwa miaka 9 nchini Ufarasa na baadayae akaachiliwa yhuru kwasharti kwamba asirejee nchini Algeria.***
Miaka 163 iliyopita Auguste Comte mwanafalsafa na mwanahisabati wa Kifaransa alifariki dunia. Comte alizaliwa mwaka 1798. Alishirikiana kwa muda fulani huko Paris na Henri de Saint Simon, mwanafalsafa mashuhuri wa zama hizo na baadaye Comte alianza kufundisha. Auguste Comte alikuwa mwasisi wa mfumo wa elimu jamii. Comte ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha The Positive Philosophy of Auguste Comte.***
Katika siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, mkataba wa Portsmouth ulitiwa saini na hivyo kuhitimisha vita kati ya Russia na Japan. Februari 8 mwaka 1904, vikosi vya majeshi ya Japan vilifanya mashambulio ya kushtukiza dhidi ya meli za kivita za Russia na kuyadhibiti maeneo ya Manchuria ambayo yalikuwa chini ya mamlaka ya Russia. Russia ilipata vipigo mfululizo katika vita hivyo. Hatimaye kwa upatanishi wa Marekani, katika siku kama ya leo pande mbili zilitia saini mkataba wa Portsmouth na huo ukawa mwisho wa vita kati ya Japan na Russia.***
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, baada ya kupamba moto harakati za mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah, kulifanyika maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali kote nchini. Kwa sababu hiyo utawala wa Shah uliokuwa umepatwa na wasiwasi mkubwa kutokana na harakati hizo za mapinduzi, uliamua kupiga marufuku maandamano ya aina yoyote ile. Wakati huo huo huo Imam Ruhullah Khomeini MA aliyekuwa uhamishoni huko Najaf nchini Iraq alitoa taarifa akiwataka wananchi wa Iran kudumisha harakati za mapambano. Katika sehemu moja ya taarifa yake kwa wananchi, Imam Khomeini aliyataja maandamano yanayofanywa kwa ajili ya kufikia malengo ya Kiislamu kuwa ni ibada. ***
Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 15 Shahrivari 1361 Hijria Shamsia, kulitokea mlipuko mkubwa katika moja ya barabara zenye msongamano mkubwa wa watu katika mji wa Tehran, Iran. Makumi ya watu waliuawa shahidi na kujeruhiwa katika tukio hilo. Jinai hiyo ilitekelezwa na vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqin la Mujahidina Khalq. Mlipuko huo ulikuwa mkubwa mno kiasi kwamba, ulisikika katika mji wote wa Tehran. Mlipuko huo ulitekelezwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa dikteta wa wakati huo wa Iraq Saddam Hussein ambaye jeshi lake lilikuwa limeshindwa vibaya na wanamapambano shupavu wa Iran***
Na katika siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, moja kati ya misikiti mikubwa katika ulimwengu wa Kiislamu ulifunguliwa rasmi huko Casablanca nchini Morocco. Msikiti huo umejengwa mwa mtindo wa kisasa na una minara inayoakisi usanifu majengo wa hali ya juu wa Kiislamu. Eneo la uwanja wa msikiti huo lina uwezo wa kuchukua waumini 75,000. Eneo la ndani la msikiti huo limepambwa kiufundi. Pembeni ya msikiti huo kumejengwa maktaba moja kubwa na Chuo Kikuu cha Kidini. Msikiti huo unahesabiwa kuwa moja kati ya misikiti mikubwa na maridadi sana katika ulimwengu wa Kiislamu.***