Sep 20, 2020 02:38 UTC
  • Jumapili tarehe 20 Septemba 2020

Leo ni Jumapili tarehe Pili Safar 1442 Hijria sawa na Septemba 20 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1321 iliyopita, aliuawa shahidi Zaid bin Ali bin Hussein mwana wa Imam Sajjad (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Zaid bin Ali alisimama kupambana na dhulma za Banii Umayyah na kulinda matunda ya mapambano ya babu yake, Imam Hussein bin Ali (as). Baada ya mapambano ya kishujaa, Zaid bin Ali aliuawa shahidi katika mji wa Kufa nchini Iraq. Harakati ya mapambano ya Zaid ni miongoni mwa matunda ya mapambano ya Imam Hussein (as) katika medani ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria kwani baada ya mapambano ya siku ya Ashuraa kulijitokeza harakati nyingi baina ya Waislamu zilizopigana jihadi kwa lengo la kuuondoa madarakani utawala dhalimu wa Banii Umayyah. 

Siku kama yale leo miaka 1172 iliyopita, sawa na tarehe pili Safar mwaka 270 Hijiria, harakati ya mapambano za Wazanji ilifeli baada ya kuuawa kiongozi wa harakati hiyo Sahib al-Zanj. Ali Bin Muhammad maarufu kwa jina la Sahib al-Zanj ambaye alikuwa akijitambua kuwa mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) na Imam Ali bin Abi Twalib (as) alianzisha harakati ya mapambano mwaka 255 Hijiria akisaidiwa na wafuasi wake pamoja na watumwa weusi ambao walikuwa wakiitwa Wazanji, dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Bani Abbas huko kusini mwa Iraq. Sahib al-Zanj aliwaahidi watumwa hao weusi kuwaachilia huru kutoka katika minyororo ya utumwa na kuwapa haki zao za kijamii kama watu wengine suala ambalo liliwafanya watu wa jamii hiyo kuvutiwa na harakati yake. Mwaka 257 Sahib al-Zanj aliudhibiti mji muhimu wa Basra, Iraq na taratibu akaanza kutwaa maeneo mengine ya karibu na mji huo. Katika kipindi hicho majeshi ya utawala wa Bani Abbasi yalifanya hujuma kadhaa dhidi ya Wazanji lakini hata hivyo hujuma hizo zilifeli kutokana na msimamo imara wa jamii ya watu hao weusi. Hata hivyo kutokana na matatizo ya ndani Wazanji walidhoofika sana na harakati yao iliyoendelea kwa kipindi cha miaka 15 ikasambaratika baada ya kuuawa kiongozi wao Sahib al-Zanj.

Siku kama ya leo miaka 697 iliyopita, alifariki dunia nchini Misri, Abu Hayyan Gharnatwi, malenga na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 654 Hijiria huko Andalusia 'Uhispania ya leo' na baadaye alifanya safari katika miji mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Mwaka 679 Abu Hayyan Gharnatwi, alielekea nchini Misri ambako aliishi hadi mwisho wa maisha yake. Akiwa nchini humo alijishughulisha na ufundisha na kuandika vitabu. Gharnatwi alikuwa mtaalamu wa elimu ya Qur'ani, Hadithi na sharia za Kiislamu, lakini alipata umashuhuri mkubwa katika utaalamu fasihi ya lugha ya Kiarabu. Abu Hayyan Gharnatwi ambaye mwishoni mwa uhai wake alikuwa kipofu, ameacha turathi nyingi kama kitabu cha 'Al-Idraaku Lilisaanil-Atraak' 'Tadhkiratun-Nuhaat' 'Tafsirul-Bahril-Muhit' na diwani ya mashairi.

Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita, lilitengenezwa basi la kwanza lililokuwa likitumia nishati ya mvuke. Basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 30 na kwenda kwa kasi ndogo na lilitengenezwa na Gordon Branz, raia wa Uingereza. Hii leo mabasi bora na ya kisasa ni miongoni mwa vyombo muhimu vya usafiri kote duniani.

Basi la zamani lililokuwa likitumia nishati ya mvuke

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, nchi ya Hungary iliungana na ardhi ya Austria na Francois Joseph akawa mtawala wa kifalme wa nchini mbili hizo. Hungary ambayo kwa mara kadhaa katika historia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na nchi zenye nguvu za Ulaya kama vile Austria na utawala wa Othmania, baadaye ilijipatia uhuru wake mnamo mwaka 1918 mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Francois Joseph

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Jean-Bedel Bokasa, dikteta wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Bokasa alizaliwa mwaka 1922 na kusomea nchini Ufaransa. Alikuwa shabiki mkubwa wa Napoleon Bonaparte na Charles de Gaulle, viongozi wawili wa zamani wa Ufaransa. Alichukua madaraka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 1966 baada ya kufanya mapinduzi dhidi ya binamu yake, David Dacko, wakati Bokasa alipokuwa mkuu wa majeshi ya nchi hiyo. Jean-Bedel Bokasa alitawala nchi hiyo kwa mfumo wa kiimla na kwa kipindi cha miaka 13 na kusimamia moja kwa moja wizara 14 kati ya wizara 16 za nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.

Jean-Bedel Bokasa

 

Tags