Oct 17, 2020 02:42 UTC
  • Jumamosi, 17 Oktoba, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 29 Mfunguo Tano Safar 1442 Hijria mwafaka na tarehe 17 Oktoba 2020 Miladia.

Katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar miaka 1235 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Ali bin Mussa ar Ridha AS, mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW. Mtukufu huyo alizaliwa mwaka 148 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Mussa al-Kadhim AS. Mnamo mwaka 200 Hijria, Maamun, Khalifa wa Bani Abbasi, alimtaka Imam Ridha AS aelekee kwenye makao ya Khalifa huyo yaliyokuwa katika mji wa Marw, kusini mashariki mwa Turkemenistan ambayo ilikuwa sehemu ya Khorasan Kuu. Ijapokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam Ridha kuwa mrithi wake, lakini kwa njia hiyo alikusudia kuimarisha zaidi nguvu za utawala wake. Utukufu na daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi aliyokuwa nayo Imam Ridha na ushawishi wake uliokuwa ukiongezeka siku hadi siku ndani ya fikra na nyoyo za watu, vilimtia woga na hofu Maamun, na hivyo akaamua kufanya njama za kumpa sumu na kumuua shahidi Imam Ridha katika siku kama leo. Imam AS amesema:"Mja bora zaidi ni yule ambaye kila anapofanya jema hufurahia, na kila anapokosea huomba msamaha, inapomfikia neema hushukuru, anapokumbana na masaibu husubiri na wakati anapoghadhibika husamehe". ***

Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imama Ridha AS

 

Miaka 1125 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria aliaga dunia Abdallah Muhanmmad ibn Jabir ibn Sinan mwanahisabati mkubwa wa Kiislamu. Ibn Sinan alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu na mtaalamu mahiri wa elimu za nujumu, hisabati na jiometri. Alizaliwa nchini Misri na alijishuhughulisha na elimu za nujumu la falaki kwa zaidi ya miaka 40. Ibn Sinan ameandika vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Taadil al-Kawakib na Miqdar al-Itisalaat.***

Abdallah Muhanmmad ibn Jabir ibn Sinan

 

Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita,  nchi za Kiarabu zinazouza nje mafuta zilianza kutekeleza vikwazo vya mafuta dhidi ya Marekani, Uingereza na makampuni yanayouuzia mafuta utawala wa Kizayuni wa Israel. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa Marekani na Uingereza kwa utawala ghasibu wa Israel katika vita vya Israel dhidi ya Syria na Misri. Hatua hiyo ilipandisha sana bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa na kutoa pigo kubwa kwa nchi hizo za Magharibi. Muda mfupi baadaye nchi za Kiarabu zilikiuka vikwazo hivyo vya mafuta na kuanza tena kuiuzia mafuta Marekani na Uingereza. Vikwazo hivyo vilionesha kuwa, nchi za Kiislamu zina silaha muhimu inayoweza kutumiwa dhidi ya uungaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi kwa utawala katili wa Israel. ***

 

Miaka 37 iliyopita aliaga dunia mtaalamu wa masuala ya jamii wa Kifaransa kwa jina la Raymond Aron. Aron alizaliwa mwaka 1905. Msomi huyo wa Kifaransa alikuwa akifundisha pia taaluma hiyo ya masuala ya jamii katika Chuo Kikuu cha Sorbonne, Paris kwa miaka kadhaa. Vile vile alikuwa akiandika makala katika majarida ya Le Figaro na Express mjini Paris. Raymond Aron ameandika vitabu vingi. ***

Raymond Aron. Aron

 

Na leo tarehe 17 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umasikini Duniani. Umoja wa Mataifa uliainisha siku hii katika kuhamasisha jamii na serikali kupambana na umaskini. Mwaka 1992 Umoja wa Mataifa uliitangaza siku hii kuwa “Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini.” Tangu wakati huo, juhudi zinafanyika kuhakikisha kuwa, kila mwanadamu anapata mahitaji muhimu ya kimaisha ikiwa ni pamoja na chakula, makazi, mavazi na huduma muhimu za kijamii na tiba. Hata hivyo wakati dunia ikiadhimisha siku ya kung'oa mizizi ya umaskini, idadi kubwa ya watu bado wanaishi katika umasikini wa kupindukia na wanashindwa kukidhi mahitaji yao ya kila siku, wengi wakiwa ni kutoka katika nchi za ulimwengu wa tatu.***

Siku ya Kimataifa ya Kung'oa Mizizi ya Umasikini