Nov 06, 2020 02:31 UTC
  • Ijumaa, Novemba 6, 2020

Leo ni ijumaa tarehe 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 6 Novemba mwaka 2020.

Miaka 992 iliyopita alifariki dunia Abu Tayyib Tabari, faqihi na mwandishi wa Kiislamu huko Baghdad. Abu Tayyib alizaliwa mwaka 348 Hijria huko Amol, moja kati ya miji ya kaskazini mwa Iran. Tabari alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa lengo la kutafuta elimu. Abu Tayyib Tabari aliishi na kufundisha huko Baghdad ambapo alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa za zama zake. Faqihi Tabari alikuwa hodari katika taaluma ya fasihi na utunzi wa mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu aliandika vitabu mbalimbali na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Jawabun fi Sama'a" na "al Ghinaa wa Al Taaliqatil Kubra fil Furu'u".

Miaka 388 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Gustav wa Pili, mfalme wa Sweden. Alizaliwa mwaka 1594 na alikalia kiti cha ufalme alipokuwa na umri wa miaka 17. Umaarufu wake ulitokana na kushinda kwake katika vita vya kidini vya miaka 30 kati ya Waprotestant na Wakatoliki vya mwaka 1618 hadi 1648.

Gustav II

Siku kama ya leo miaka 207 vita vya kwanza vya Simon Bolivar, shujaa wa uhuru wa mataifa ya Amerika ya Latini vya kukomboa nchi ya Venezuela kutoka kwa wakoloni wa Kihispania vilimalizika kwa ushindi. Katika vita hivyo askari 6500 wa Simon Bolivar waliwashinda askari elfu 13 wa Uhispania. Hatimaye shujaa huyo wa Amerika ya Latini aliikomboa Venezuela kutoka utawala wa kikoloni wa Uhispania na kisha akashiriki katika mapambano ya kupigania uhuru ya nchi nyingine kadhaa za kusini mwa Amerika.

Simon Bolivar

Siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Novemba 1860 Abraham Lincoln aliyekuwa mpinzani wa utumwa nchini Marekani, alichukua madaraka na kuwa rais wa nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wake vita kadhaa vilitokea nchini humo na kupelekea waliokuwa wakiunga mkono utumwa kushindwa. Abraham Lincoln aliuawa mwaka 1865 na mmoja wa wapinzani wa harakati za kupinga utumwa nchini Marekani.

Abraham Lincoln

Na miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo, wananchi kote nchini Iran walifanya maandamano makubwa wakipinga kuingia madarakani serikali ya kijeshi ya Jenerali Gollam Reza Azhari aliyekuwa kibaraka wa utawala fasidi wa Kipahlavi. Katika maandamano hayo wananchi Waislamu wa Iran walitangaza azimio wakisema kuwa mabadiliko ya kimaonyesho na kubadilisha nafasi za vibaraka wa Marekani hakuwezi kuzuia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Siku hiyo pia Kiongozi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa ujumbe kwa mnasaba wa mauaji yaliyofanywa na utawala wa Shah dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu tarehe 13 Aban mwaka huo huo akiwaambia wananchi kwamba: “Ninyi taifa shujaa, mumethibitisha kwamba vifaru, mitutu ya bunduki na mikuki imepata kutu na kwamba haiwezekani kukabiliana na irada ya chuma ya wananchi.”  

Gollam Reza Azhari