Jumatano tarehe 11 Novemba 2020
Leo ni Jumatano tarehe 25 Mfunguo Sita mwaka 1442 Hijria sawa na Novemba 11 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, aliaga dunia Yasser Arafat Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa. Alizaliwa mwaka 1929 na kuanza harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel akiwa katika rika la ujana. Mwaka 1946, Yasser Arafat alielekea nchini Misri kwa ajili ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Cairo na miaka mitano baadaye alihitimu masomo katika taaluma ya Usanifu Majengo. Mwaka 1965 alirejea Palestina na kuasisi Harakati ya Fat-h ili kupambana na utawala wa Tel Aviv. Miaka minne baadaye alichukua hatamu za kuongoza PLO hadi alipoaga dunia.
Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo, Angola ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Wakoloni wa Kireno kwa mara ya kwanza waliingia katika ardhi ya Angola mwaka 1483 Miladia. Wakati huo, ardhi ya Angola ilikuwa sehemu ya ufalme wa Kongo, Zaire ya zamani.
Katika siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, virusi vinavyosababisha maradhi hatari ya kupooza viungo vya miili ya watoto yaani Polio viligunduliwa. Virusi hivyo vilipewa jina la virusi vinavyolemaza watoto kwa sababu ya kuwashambulia zaidi watoto wadogo na kuwapoozesha viungo vyao vya mwili. Baadaye kidogo mwanasayansi Dakta Jonas Salk aliyegundua virusi vya Polio alifanikiwa pia kugundua chanjo yake.
Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, Vita vya Kwanza vya Dunia vilifikia kikomo baada ya kutiwa saini mkataba wa kuacha vita hivyo. Vita vya Kwanza vya Dunia vilipiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 kati ya nchi waitifaki yaani serikali za Russia, Uingereza, Ufaransa na Italia kwa upande mmoja, na nchi za Ujerumani, Bulgaria, Utawala wa Othmania na ufalme wa Austria na Hungary kwa upande wa pili. Watu zaidi ya milioni 15 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 20 kujeruhiwa. Vilevile vilisababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150 kwa nchi zilizopigana vita hivyo.
Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita alizaliwa Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".
Na siku kama ya leo miaka 1006 iliyopia sawa na tarehe 25 Rabiul Awwal mwaka 436 Hijiria alifariki dunia Sayyid Murtadha Alamul Huda mwanafunzi mashuhuri wa Sheikh Mufid. Alizaliwa mwaka 355 Hijiria huko Baghdad na alijifunza elimu za zama zake. Baada alianzisha kituo cha elimu ambacho kilikuwa kikihudhuriwa na watu wenye itikadi na mielekeo tofauti. Sayyid Murtadha ameacha vitabu vingi na miongoni mwa vitabu hivyo ni Tanzihil Anbiyah, Taqribul Usul pamoja na kitabu cha maashairi chenya beti elfu 20.