Nov 20, 2020 02:32 UTC
  • Ijumaa tarehe 20 Novemba 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 4 Mfungo Saba Rabiuthanil 1442 Hijria sawa na Novemba 20 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1269 iliyopita, alizaliwa Sayyid Abdul Adhim al Hassani aliyekuwa mmoja wa wajukuu wa Imam Hassan al Mujtaba (a.s) huko katika mji wa Madina. Sayyid Abdul Adhim alikuwa mmoja kati ya shakhsiya walioaminiwa na Imam al Hadi (as) na alinukuu hadithi moja kwa moja kutoka kwa maimamu watukufu kama vile Ridha, Jawad na al Hadi (as). Sayyid Abdul Adhim alihamia Iran kutokana na pendekezo la Imam al Hadi (as) kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu na akaishi katika mji wa Rei karibu na Tehran ya sasa. Sayyid Abdul Adhim aliuawa shahidi mwezi Shawwal mwaka 250 Hijria. Kaburi la mtukufu huyo liko katika eneo la Rei na ni miongoni mwa maeneo yanayotembelewa na Waislamu kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Haram ya Sayyid Abdul Adhim al Hassani

Siku kama ya leo, miaka 929 iliyopita alizaliwa mjini Baghdad Abubakr Muhammad Anbari, faqihi, mtaalamu wa hadithi na lugha. Anbari alipata kusoma elimu ya dini, nahwu na lugha akiwa kijana mdogo kutoka kwa baba yake. Baada ya kuhitimu masomo yake katika nyanja tofauti, alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi. Alitokea kuwa faqihi mkubwa na kutabahari katika elimu ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Manshurul-Fawaaid.’

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita alifariki dunia mwandishi mashuhuri wa Kirusi, Leo Tolstoy. Mwandishi huyo alizaliwa mwaka 1828 na aliondokewa na baba na mama yake akiwa bado mdogo. Alifanya safari za kitalii na uchunguzi katika jamii nyingi za Ulaya na mambo aliyoyashuhudia katika safari hizo yalimfanya achukie ustaarabu wa kimaada wa nchi za Magharibi. Tolstoy alilipa umuhimu mkubwa suala la kuwapa elimu na malezi watoto wadogo na alikuwa akijitahidi mno kusaidia matabaka ya watu maskini na wasiojiweza. Leo Tolstoy ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Kiyama", "Kipindi cha Utotoni" na riwaya ya "Vita na Amani".

Leo Tolstoy

Tarehe 20 Novemba miaka 100 iliyopita mapambano makubwa ya wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni wa Kiingereza yalishindwa. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kusambaratika utawala wa Kiothmania, serikali za Ufaransa na Uingereza ziligawana ardhi za utawala huo katika Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo Uingereza ilichukua Iraq na kukabiliwa na mapambano makali ya wananchi tangu hapo mwanzoni. Mapambano hayo yaliongozwa na wanazuoni wa Kiislamu waliotoa wito wa kufukuzwa wakoloni wa Kiingereza na kuundwa serikali huru itakayozingatia sheria za Kiislamu.

Askari wa Uingereza wakiingia Baghdad mwaka 1917 

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, aliuawa shahidi Sheikh Izzuddin Qassam ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni maghasibu na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali huko Syria, Sheikh Qassam aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha al Azhar huko Misri. Wananchi wa Palestina walianza mapambana dhidi ya mkoloni Mwingereza mwaka 1930 chini ya uongozi wa Sheikh Izzuddin Qassam. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa Wazayuni maghasibu walishirikiana na wakoloni wa Kiingereza na kumuuwa kigaidi kiongozi huyo wa harakati ya mapambano ya Palestina.

Sheikh Izzuddin Qassam

Katika siku kama ya leo miaka 70 iliyopita majeshi ya Marekani na China yalipambana uso kwa uso kwa mara ya kwanza kabisa katika vita vya Korea. Mapigano hayo yalitokana na himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa Korea Kusini na uungaji mkono wa China na Urusi kwa Korea Kaskazini. Vita vya Korea vilisababisha hasara kubwa mno kwa pande zote mbili. Vita hivyo vilisimama kutokana na upatanishaji wa Umoja wa Mataifa na hadi sasa Korea Kaskazini na Kusini zimebakia nchi mbili zilizojitenga.

Bendera za Korea Kaskazini na Kusini