Alkhamisi, 3 Disemba, 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1442 Hijria mwafaka na tarehe 3 Disemba 2020 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, alizaliwa Dakta Rajendra Prasad, mwanasiasa na mwanafalsafa wa India huko katika mojawapo ya vijiji vya jimbo la Bihar. Rajendra Prasad aliweza kuendelea na masomo na kufikia daraja ya udaktari (PhD) licha ya hali duni ya kifedha ya familia yake. Aidha alishiriki na wananchi wa India katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao. Prasad vilevile alishirikiana bega kwa bega na Mahatma Gandhi katika mapambano ya kisiasa dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na kwa mara kadhaa aliteuliwa kuongoza chama cha Congress ya Kitaifa ya India. Rajendra Prasad aliteuliwa kuwa Rais wa kwanza wa India baada ya uhuru wa nchi hiyo na kuasisiwa mfumo wa jamhuri nchini humo mwaka 1950. ***
Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia msomi mkubwa wa hadithi Mullah Muhammad Nakhjawani. Mullah Nakhjawani alibobea sana katika elimu za fiqhi na hadithi na lifuatwa zaidi na Waislamu wa eneo la Kaukazia. Ayatullah Nakhjawani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 66 katika mji mtakatifu wa Karbala na kuzikwa katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika mji wa Najaf. Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa. ***
Miaka 101 iliyopita katika siku kama ya leo, Auguste Renoir mchoraji mkubwa wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 78. Renoir alizaliwa tarehe 7 Machi 1841 na kwa haraka mno aliweza kuonyesha dhuku na mapenzi yake kwa taaluma ya uchoraji. Akiwa na umri wa miaka 19 tayari Auguste Renoir alikuwa ameshaondokea kuwa mchoraji mahiri na mashuhuri mjini Paris. ***
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, kulitokea janga kubwa la kuvuja gesi ya kemikali katika kiwanda kimoja cha Marekani katika mji wa Bhopal huko katikati mwa India. Kiwanda hicho kilikuwa kikimilikiwa na kampuni ya Kimarekani iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Union Carbide. Uzembe wa maafisa wa kiwanda hicho na kutozingatiwa viwango vya usalama ulipelekea kuvuja kwa gesi ya sumu ya sianidi (cyanide) kutoka katika kiwanda hicho na kuenea katika hewa. Maelfu ya wakazi mji wa Bhopal walipoteza maisha na mamia ya wengine kujeruhiwa katika janga hilo ambalo lilitambuliwa kuwa janga kubwa zaidi la viwandani duniani. ***
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, mkutano wa kwanza wa Kiislamu kuhusiana na Palestina ulifanyika hapa mjini Tehran. Mkutano huo ulifanyika katika fremu ya mfungamano wa walimwengu na mapambano ya Intifadha ya Palestina na kukabiliana na wimbi la kuhajiri Mayahudi kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa kuchunguza chanzo cha mapambano ya Intifadha ya wananchi Waislamu wa Palestina, Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi hao pamoja na taathira ya matukio ya Mashariki ya Kati kwa taifa la Palestina.***
Na katika siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, maafisa wa kijeshi wa Iran walitangaza kwamba limefanikiwa kuidhibiti ndege ya kijasusi isiyokuwa na rubani (drone) ya Marekani aina ya RQ-170. Ndege hiyo iliyoingia katika anga ya mashariki mwa Iran kutokea Afghanistan, ilitumbukia katika mtego wa kikosi cha vita vya elektroniki cha Iran na kushushwa chini ikiwa nzima. Ndege hiyo ya RQ-170 ni miongoni mwa drone za kisasa kabisa za jeshi la Marekani na inatumiwa na shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufanya ujasusi. Baada ya kudhibitiwa na jeshi la Iran wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu walichunguza na kuvumbua namba za siri za ndege hiyo ya kijasusi ya Marekani na kupata ripoti muhimu za kipelelezi na teknolojia ya utengenezaji wake. Miaka mitatu baada ya ndege hiyo kushikwa na jeshi la Iran, wataalamu hapa nchini wamefanikiwa kuzalisha na kutengeneza ndege hiyo ya kisasa kabisa na kijasusi.***