Feb 02, 2021 02:58 UTC
  • Jumanne, Februari 2, 2021

Leo Jumanne tarehe 19 Mfunguo Tisa Jamadithani 1442 Hijria mwafaka na tarehe Februari Pili 2021 Miladia.

Tarehe 14 Bahman 1357 Hijria Shamsia yaani miaka 42 iliyopita, wananchi wa Iran walipokuwa katika sherehe na shamrashamra za kurejea nchini Imam Khomeini akitokea uhamishoni nje ya nchi, Imam alizungumza na waandishi habari akieleza misimamo ya mfumo ujao wa utawala wa Kiislamu hapa nchini na kutangaza kuwa ataunda serikali ya mpito ya mapinduzi muda mfupi baadaye. Imam Khomeini alitangaza kuwa serikali hiyo ya mpito itakuwa na jukumu la kutayarisha kura ya maoni ya Katiba mpya ya Iran. Vile vile alimtahadharisha Shapour Bakhtiar Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah kwamba, iwapo ataendelea kuwakandamiza wananchi angetangaza vita vya jihadi. Imam Khomeini vile vile alilitaka jeshi lijiunge na mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo pia ilitangazwa kwamba, Wamarekani elfu 35 walikuwa wamekwishaondoka katika ardhi ya Iran na kwamba wengine elfu 10 wako mbioni kuondoka.

Imam Khomeini (MA)

##########

Miaka 11 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilirusha kwa mafanikio roketi ya kwanza ya kubebea satalaiti angani iliyojulikana kwa jina la Omid. Miaka iliyofuata Iran ilituma viumbe hai angani kwa mafanikio ikiwa ni pamoja na kobe na tumbili na hatua hiyo iliingiza Iran katika klabu ya nchi zenye teknolojia ya anga za mbali tena katika kipindi hicho cha vikwazo vikali vya kiuchumi vya nchi za Magharibi.

#########

Siku kama ya leo miaka 229 iliyopita, mkataba wa kihistoria wa Berlin, ulitiwa saini baina ya Leopold II mfalme wa wakati huo wa Austria na Frederick William aliyekuwa mfalme wa Prussia. Mkataba huo ulikuwa natija ya maafikiano baina ya viongozi hao wawili yaliyofikiwa tarehe Pili Agosti mwaka 1791 huko Pillnitz kwa ajili ya kukabiliana na mapinduzi ya Ufaransa. Hii ilitokana na kuwa, watawala wa Ulaya walikuwa wameingiwa na woga mkubwa kutokana na baadhi ya nadharia za wapigania uhuru wa Ufaransa. Licha ya kuweko mkataba huo na hata mashambulio ya pamoja ya Austria, Prussia na Uingereza dhidi ya Ufaransa na himaya yao kwa wapigania mfumo wa utawala wa Kifalme wa nchi hiyo, harakati hizo hazikuwa na natija kwani hatimaye wanamapinduzi wa Ufaransa waliibuka na ushindi. 

Leopold II mfalme wa wakati huo wa Austria na Frederick William aliyekuwa mfalme wa Prussia

##########

Na Katika siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, Dmitri Ivanovich Mendeleev msomi na mwanakemia wa Kirusi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73 huko Saint Petersburg uliokuwa mji mkuu wa Russia wakati huo. Dmitri alizaliwa mwaka 1834 na kusoma taaluma ya kemia. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mwingi muhimu katika taaluma ya kemia ambapo baadaye ulikuja kujulikana kwa jina la jedwali la Mendeleev.

Dmitri Ivanovich Mendeleev

#########

 

Tags