Feb 03, 2021 02:30 UTC
  • Jumatano, 3 Februari, 2021

Leo ni Jumatano tarehe 20 Mfunguo Tisa Jamadithani mwaka 1442 Hijria sawa na tarehe Tatu Februari 2021 Miladia.

Miaka 1450 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Bibi Fatima Zahra, binti mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Bibi Fatima Zahra alilelewa katika nyumba ya wahyi na chini ya malezi bora na mwongozo wa baba yake Mtume Muhammad (saw) na hivyo kuweza kufikia daraja za juu za ukamilifu. Bibi Fatima (as) alikuwa na nafasi kubwa katika kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikimkabili baba yake kutoka kwa washirikina. Mwaka wa pili Hijiria, Bibi Fatima Zahra alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) ambaye ni dhihirisho la haki, uadilifu na uchaji-Mungu katika sherehe ndogo iliyosimamiwa na Mtukufu Mtume Muhammad (saw). Vilevile Bibi Fatima akiwa na Imam Ali alifanikiwa kulea shakhsia adhimu kama Hassan, Hussein na Bibi Zainab (as). Mbali na majukumu ya kulea familia, Bibi Fatima Zahra, alijishughulisha pia na malezi ya jamii. ***   

Siku kama hii ya leo miaka 533 iliyopita sawa na tarehe tatu Februari mwaka 1468 Miladia alifariki dunia mvumbuzi wa mashine ya uchapishaji, Johannes Gutenberg. Mvumbuzi huyo alizaliwa nchini Ujerumani lakini baada ya muda alihamia Strasbourg, Ufaransa na akaanza kujishughulisha na kazi za kiufundi. Mwaka 1443 au 1444 Gutenberg alifanikiwa kutengeneza mashine ya uchapishaji na kupiga hatua muhimu katika uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible. ***

Johannes Gutenberg

Miaka 122 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa huko Khomein Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ruhullah al-Musawi Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa zaidi za kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.***

Imam Khomeini 

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita mfereji wa Suez uliokuwa ukidhibitiwa na Uingereza, ulishambuliwa na vikosi vya majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othmaniya katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Udhibiti wa mfereji huo wa Suez ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa pande mbili zilizokuwa zikipigana katika Vita vya Kwanza vya Dunia kutokana na ukweli kwamba mfereji huo ndio unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu. Uingereza ambayo haikuwa tayari kupoteza makoloni yake ya Asia, ilipigana vikali na majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othomaniya na kupata ushindi.Mfereji wa Suez uliendelea kudhibitiwa na Uingereza hadi ulipotaifishwa na kiongozi wa Misri Gamal Abdul Nasir hapo mwaka 1956. ***

Mfereji wa Suez

Na miaka 42 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo yaani tarehe 15 mwezi Bahman mwaka 1357 Hijria Shamsiya katika hali ambayo mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah yalikuwa yamefikia kileleni baada ya Imam Ruhullah Khomeini kurejea nchini akitokea uhamishoni, Waziri Mkuu wa utawala wa kifalme wa Shah, Shapur Bakhtiyar alifanya jitihada za kuwatuliza wananchi bila ya mafanikio yoyote. Bakhtiyar alifanya juhudi za kusitisha harakati za Mapinduzi kwa kujidhihirisha kuwa ni mwanademokrasia na mpigania uhuru na akasema kwamba, hatamruhusu Imam Khomeini kuunda serikali ya mpito nchini. Wakati huo uasi wa kiraia, kukimbia wanajeshi na kujiunga na safu za wananchi katika miji mbalimbali ya Iran ikiwa ni pamoja na kujiuzulu wabunge, viongozi wa ngazi za juu serikalini na kadhalika kuliifanya serikali ishindwe kudhibiti hali ya mambo nchini.***

Kuwasili Imam Khomeini (M.A) mjini Tehran