Mar 17, 2021 02:28 UTC
  • Jumatano tarehe 17 Machi mwaka 2021

Leo ni Jumatano tarehe 3 Shaabani 1442 Hujria inayosadifiana na tarehe 17 Machi mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib (as) mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Kipindi bora cha maisha ya Imam Hussein (as) ni cha miaka sita wakati mtukufu huyo alipokuwa pamoja na Mtume Mtukufu wa Uislamu. Imam Hussein (as) alijifunza maadili mema na maarifa juu ya kumjua Mwenyezi Mungu kutoka kwa baba yake Imam Ali (as) na mama yake Bi Fatimatul-Zahra (as), ambao walilelewa na Mtume Mtukufu. Imam Hussein alishiriki vilivyo katika matukio mbalimbali wakati Uislamu ulipokabiliwa na hatari. Daima alilinda turathi za thamani kubwa za Mtume kwa kutoa darsa na mafunzo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kiitikadi, kifikra na kisiasa. Imam Hussein (as) alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu mwaka 50 Hijria, baada ya kuuawa shahidi kaka yake yaani Imam Hassan bin Ali bin Abi Talib (as). Hatimaye Imam Hussein (as) aliuawa shahidi huko Karbala, Iraq mwaka 61 Hijria wakati akitetea dini tukufu ya Kiislamu.

 

 Miaka 1385 iliyopita inayosadiafina na leo, ardhi ya Baitul Muqaddas huko Palestina ilikombolewa na Waislamu. Vita vya kwanza kati ya Waislamu na Warumi vilijiri huko kaskazini mwa Bahari Nyekundu baada ya kudhihiri Uislamu. Jeshi la Waislamu lilitoa pigo kwa Warumi na eneo la kusini mwa Palestina likakombolewa katika zama za utawala wa Umar bin Khattab. Baada ya kushindwa huko, mfalme wa Roma alituma jeshi kubwa katika ardhi za Palestina. Warumi walishindwa vibaya na jeshi la Kiislamu katika vita vilivyojiri huko Palestina na mwishoni mwa mapigano hayo, kamanda wa jeshi la Roma aliuawa na Damascus ikadhibitiwa na Waislamu.

Ardhi ya Baitul Muqaddas

Katika siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita, msafara wa Imam Hussein (as) mjukuu wa Bwana Mtume (saw) uliwasili katika mji wa Makka. Imam Hussein ambaye alikuwa amehatarisha maisha yake kwa kuupinga utawala wa Yazid na kukataa kumpa baina na mkono wa utiifu kiongozi huyo, aliondoka Madina na kuelekea Makka. Alipowasili mjini Makka Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib alilakiwa na watu wengi na shakhsia wakubwa wa mji huo na akaamua kuitumia fursa ya uwepo wa Mahujaji kwa ajili ya kufichua ufisadi wa Bani Ummayh hususan Yazid bin Muawiya na kwa muktadha huo akawa amefikisha ujumbe wake katika pembe mbalimbali za maeneo ya Waislamu. Aidha akiwa mjini Makka Imam Hussein alipokea maelfu ya barua kutoka kwa wakazi wa mji wa Kufa Iraq ambao mbali na kutangaza kuupinga utawala wa Yazid walimtaka Imam aelekee katika mji huo. Baada ya kukaa kwa takribani miezi mine mjini Makka na kwa kuzingatia mwaliko wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na kutokana na hatari iliyokuwa ikimkabili kutoka kwa makachero wa Yazid, tarehe 8 Dhulhija mwaka 60 Hijria, alielekea katika mji wa Kufa.

Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita alizaliwa Ayatullah Hussein Khadimi, faqihi, alimu na mujtahidi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi na ya kati alielekea Najaf, Iraq na kupata elimu kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Mirza Naini, Sayyid Abul-Hassan Isfahani na Sheikh Muhammad Jawad Balaghi. Alifikia daraja ya ijtihadi akiwa na umri wa miaka 26 na baada ya kurejea Isfahani alijikita kTIK shughuli ya kufundisha sheria za Kiislamu (fiqhi) na usulu fiqhi. Katika tukio la amri ya mtawala wa wakati huo wa Iran ya kuwataka wanawake wavue vazi la staha la hijabu, Ayatullah Hussein Khadimi alitoa hotuba kali ya kupambana na utawala wa Reza Shah Pahlavi kama ambavyo pia alishiriki katika harakati mbalimbali za kupambana na njama za mkoloni Mwingereza kwa ajili ya kupora raslimali za Iran.

Ayatullah Hussein Khadimi

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, wawakilishi wa nchi za Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg, walitia saini mkataba wa ushirikiano mjini Brussels, Ubelgiji. Katika mkataba huo uliojulikana kwa jina la "Mkataba wa Brussels", nchi hizo zilikubaliana kuanzisha mfumo wa ulinzi wa pamoja na kupanua uhusiano wao wa kiuchumi na kiutamaduni.  Mkataba huo pia ndio uliokuwa chachu ya kuanzishwa kwa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO. Kwani ni baada ya hapo ndipo yalipofanyika mazungumzo kati ya Marekani, Canada na baadhi ya nchi wanachama wa Mkataba wa Brussels huko Washington, Marekani ambapo baadaye kuliundwa Shirika hilo la NATO mwezi Aprili 1949.

 

Tags