Jumatatu tarehe 22 Machi, mwaka 2021
Leo ni tarehe Pili Farvardin mwaka 1400 Hijria Shamsiya sawa na tarehe Nane Shaaban 1442 Hijria inayosadifiana na 22 Machi 2021.
Siku kama ya leo miaka 880 iliyopita alizaliwa Ibn Rumiyya mpokezi wa hadithi, mtaalamu wa mimea na dawa wa Kiislamu wa karne ya sita Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Rumiyya alijifunza hadithi kutoka kwa wasomi na wapokezi hadithi wakubwa wa zama hizo na kujifunza elimu ya utaalamu wa mimea sambamba na elimu ya dini. Akiwa Andalusia, Ibn Rumiyya alianza kuchunguza na kutambua sifa za mitishamba na baadae alifanya safari katika nchi mbalimbali kama Misri, Iraq na Hijaz. Alijishughulisha na masuala ya utafiti wa mitishamba akiwa huko bila kusahau kujifunza hadithi. Ibn Rumiyya aliandika vitabu vingi kuhusu mitishamba, fiqih na hadithi, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya vitabu hivyo vimepotea.

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita ulianzishwa Muungano wa Soka wa Kimataifa kwa shabaha ya kusimamia mashindano ya mpira wa miguu kote duniani. Kabla ya kuundwa muungano huo, mashindano ya soka yalikuwa yakifanyika katika nchi mbalimbali kwa muundo usiokuwa rasmi. Muungano huo ulibadilisha muundo wake na kujulikana baadaye kwa jina la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na liliandaa pambano rasmi la kwanza la kimataifa mwaka 1901, kati ya Uingereza na Ujerumani.

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita aliuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwanachuoni na mwasisi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas pamoja na watu wengine 10. Sheikh Ahmad Yassin aliuawa shahidi baada ya kumaliza swala ya Alfajiri katika msikiti mmoja ulioko eneo la Ukanda wa Gaza, wakati aliposhambuliwa na helikopta za utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheikh Ahmad Yasin aliasisi harakati ya Hamas mwaka 1987 akishirikiana na wanamapambano wengine kadhaa wa Kipalestina na miaka miwili baadaye alifungwa jela na utawala ghasibu wa Israel. Mauaji ya mpigania uhuru huyo ambaye alikuwa kiwete na kipofu wakati wa kuuawa kwake, yalidhihirisha tena ugaidi wa kiserikali wa utawala haramu wa Israel.
Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, ilianza operesheni kubwa ya 'Fat-hul Mubiin' ya wapiganaji shujaa wa Kiislamu huko kusini magharibi mwa Iran kwa shabaha ya kuyarejesha nyuma majeshi vamizi ya Iraq. Kwenye operesheni hiyo iliyopelekea kukombolewa miji ya Dezful, Andimeshk, Shush na mamia ya vijiji vya eneo hilo, wanajeshi wasiopungua elfu 25 wa Iraq waliuawa na wengine elfu 15 kukamatwa mateka.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, yaani sawa na tarehe 22 Machi 1945, iliundwa Jumuiya ya Waarabu kutokana na mapendekezo ya Farouk, aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Misri na kutiwa saini makubaliano ya kuundwa jumuiya hiyo na serikali za Syria, Iraq, Saudi Arabia, Misri na Yemen mjini Cairo. Lengo la kuanzishwa jumuiya hiyo lilikuwa ni kuhifadhiwa ardhi zote, kujitawala nchi wanachama na kuwepo ushirikiano wa karibu wa kisiasa kiuchumi na kiutamaduni kati ya nchi hizo.