Jun 02, 2021 02:27 UTC
  • Jumatano tarehe Pili Juni mwaka 2021

Leo ni Jumatano tarehe 21 Mfunguo Mosi Shawwal 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe Pili Juni mwaka 2021.

 Miaka 1350 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, ardhi ya Andalusia huko Uhispania ya leo ilidhibitiwa na jeshi la Kiislamu lililoongozwa na Tariq bin Ziyad. Tariq ambaye alikuwa na wapiganaji karibu ya elfu 12, alivuka kwa boti mlango bahari ulioko kati ya Morocco na Uhispania ambao umepewa jina lake Tariq bin Ziad au "Gibraltar". Tariq bin Ziyad aliamuru kochomwa moto boti zote zilizotumiwa na wapiganaji wake kuvukia lango bahari na Gibralta ili kuwahamasisha zaidi kupigana na maadui. Katika kipindi cha karne 8 za utawala wao huko Andalusia, Waislamu walianzisha vituo mbalimbali vya utamaduni na taasisi za kiuchumi na kwa kipindi kirefu ardhi hiyo ilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu barani Ulaya.

Tariq bin Ziyad

Miaka 1088 iliyopita mwafaka na leo, alifariki dunia Ibn Habban, mtaalamu wa hadithi, elimu ya fiq'hi na mwanahistoria mashuhuri wa karne ya 14 Hijiria. Alipata elimu ya msingi kwa walimu mashuhuri wa zama zake na kisha akaelekea Neishabur kaskazini mwa mashariki mwa Iran, ambao katika kipindi hicho ulikuwa ni moja ya vituo muhimu vya kielimu. Ibn Habban anahesabika kuwa mtu mwenye nadharia muhimu katika elimu ya hadithi. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha"At-Thuqat" na Rawdhatul-Uqalaai wa Nazahatul-fudhalaai."

Katika iku kama hii ya leo miaka 139 iliyopita alifariki dunia Giuseppe Garibaldi kamanda mzalendo na kiongozi wa harakati ya kuleta umoja wa Italia. Giuseppe alizaliwa mwaka 180 na wakati wa ujana wake alifanya kazi mbalimbali na mwishowe kujiunga na jeshi. Baadaye alichaguliwa kuwa kamanda wa wanaharakati wa kupigania uhuru wa Italia na alifanya jitihada nyingi za kuleta umoja nchini humo. Kwa ajili hiyo alijulikana katika historia ya Italia kama shujaa wa taifa.

Giuseppe Garibaldi

Siku kama ya leo Miaka 51 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim

Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo,  sawa na tarehe 12 Khordad mwaka 1379 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Hujjatul Islam Sayyid Ali Akbar Abuturabi, mwanzuoni mwenye mwamko na mwanaharakati wa Iran katika ajali ya gari pamoja na baba yake Ayatullah Sayyid Abbas Abuturabi. Hujjatul Islam Sayyid Ali Akbar Abuturabi alizaliwa mwaka 1318, kwa mujibu wa kalenda ya Iran, katika mji wa kidini wa Qum. Alijifunza elimu ya dini kutoka kwa maulamama wakubwa akiwemo Imam Khomeini (M.A). Hujjatul Islam Abuturabi katika mapambano ya kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu mara kadhaa alikamatwa na kuteswa na vibaraka wa Shah. Wakati vya vita vya Iran na Iraq mwaka 1359 alikamatwa mateka na askari wa utawala wa Baath wa Iraq na kufungwa kwa miaka 10 katika jela zenye mateso makali za Iraq. Lakini alivumilia kiasi cha kuwa mashuhuri miongoni mwa mateka wa Iran kwenye jela hizo. Alipoachiliwa huru aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya mateka na walioachiliwa huru.

Sayyid Ali Akbar Abuturabi