Jumamosi, Juni 26, 2021
Leo ni Jumamosi tarehe 15 Mfunguo Pili Dhulqaada 1442 Hijria sawa 5 Tir mwaka 1400 Hijria Shamsiya inayosadifiana na Juni 26 mwaka 2021 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 942 iliyopita, kwa mujibu wa riwaya mbali mbali za historia, Ibn Fakhr, msomi maarufu Muislamu ambaye pia alikuwa mtaalamu wa lugha alifariki mjini Baghdad. Katika ujana wake alisafriki mara kadhaa kuelekea Makka na Yemen kwa ajili ya kupata elimu kutoka kwa wasomi bingwa wa zama hizo. Kati ya vitabu vyake mashuhuri ni Jawab al Masail.

Miaka 185 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, aliaga dunia Rouget de Lisle, malenga na mtunzi wa nyimbo za kimapinduzi wa Ufaransa. Rouget alihudumu pia jeshini na alikuwa akisoma mashairi ya kuwahamasisha wanamapinduzi wa Ufaransa na kutunga nyimbo za hamasa na za kusisimua. Rouget de Lisle alitunga wimbo wa kimapinduzi kwa jina "La Marseillaise" ambao baadaye ulikuwa wimbo rasmi wa taifa.

Miaka 76 iliyopita sawa na tarehe 26 Juni 1945, mkutano wa kimataifa wa San Fransisco ulimaliza shughuli zake katika mji unaojulikana kwa jina hilo huko Marekani kwa kupasishwa hati ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ambao ulikuwa wa kwanza wa kimataifa kuwahi kufanyika baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi 50 waitifaki katika vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita kisiwa cha Madagascar kilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Uingereza na Ufaransa zilianzisha ushindani wa kuidhibiti nchi hiyo ya Kiafrika katika karne ya 18. Mwishoni mwa karne ya 19 Ufaransa ilikidhibiti kikamilifu kisiwa cha Madagascar. Hata hivyo wananchi wa Madagascar waliendesha mapambano mengi ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa, miongoni mwake ni yale ya mwaka 1947 ambapo karibu watu elfu 80 waliuawa.

Na tarehe 26 Juni miaka 24 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuwatetea Wahanga wa Mateso kwa lengo la kufuta kabisa vitendo hivyo viovu duniani. Vitendo vya mateso vina historia ndefu duniani lakini ilitazamiwa kuwa maovu hayo yangehitimishwa kikamilifu katika zama hizi hususan baada ya kupasishwa nyaraka kadhaa zinazohusiana na haki za binadamu. Hata hivyo bado kuna nchi zinazotumia mateso kuwakandamiza wapinzani. Marekani ambayo inajinadi kuwa mtetezi mkubwa wa haki za binadamu ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kutesa wapinzani kote duniani. Vilevile utawala wa Kizayuni wa Israel unaosaidiwa na kuungwa mkono na nchi za Magharibi hususan Marekani umekuwa ukiwatesa na kuwanyanyasa raia wa Palestina katika korokoro na jela zake za kutisha.

Na Kila mwaka Juni 26 huadhimishwa siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya na usafirishaji haramu. Siku hii ilianishwa katika kikao kilichofanyika katika siku kama hii mwaka 1987 huko Vienna, Austria. Kikao hicho pia kilijadili htua za kuchukuliwa kukabiliana na mihadarati ambayo sasa ni tatizo kubwa dunaini.
Mwaka 2020 Mwakilishi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Mihadarati na Uhalifu (UNODC) hapa mjini Tehran aliishukuru Iran kwa jitihada zake za kupambana na mihadarati na kusema Iran imechukua hatua kubwa katika kunasa dawa za kulevya. Alezander Fedulov, Mwakilishi wa UNODC mjini Tehran aliyasema hayo katika kikao maalumu kilichofanyika kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya. Akizungumza katika kikao hicho ambacho kilifanyika kwa njia ya video Fedulov alisema: "Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2020 ya Umoja wa Mataifa, asilimia 90 ya afiuni, asilimia 26 ya heroini na asilimia 48 ya mofini duniani imenaswa na maafisa wa Iran."
