Jun 30, 2021 02:22 UTC
  • Jumatano, Juni 30, 2021

Leo ni Jumatano mwezi 19 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 30 Juni 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 724 iliyopita, yaani mwezi 19 Mfunguo Pili Dhulqaad mwaka 718 Hijria, Kamaluddin Farsi, mwanahisabati wa Kiirani alifariki dunia. Kamaluddin Farsi alikuwa mwanahisabati na mwanafizikia wa Kiirani mwenye kipaji cha kipekee na alitembea maeneo mbalimbali ili kuchota elimu kutoka kwa wasomi wakubwa wa zama zake. Ijapokuwa alifariki dunia akiwa bado kijana, lakini amevirithisha vizazi vya baada yake turathi bora na muhimu sana katika upande wa hisabati na fizikia. Miongoni mwa athari muhimu za Kamaluddin Farsi ni risala ya "Tadhkiratul Ahbab" kinachotoa nadharari ya idadi ya namba. Athari nyingine ya kipekee ya mwanafizikia na mwanahisabati huyo bingwa wa Kiirani ni kitabu cha Tanqih al Manadhir ambacho hadi hivi sasa ni kitabu cha marejeo cha wasomi wa zama hizi.

Kamaluddin Farsi

 

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, yalianza mapambano ya raia wa Iraq chini ya uongozi wa Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Shirazi dhidi ya wavamizi wa Uingereza. Itakumbukwa kuwa baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kufuatia makubaliano ya waitifaki wa vita hivyo juu ya kugawana utawala wa Othmania, uongozi na usimamizi wa Iraq, Jordan na Palestina ulikabidhiwa mkoloni Mwingereza. Kuanzia wakati huo ukoloni wa London ukaanza rasmi kupora vyanzo na utajiri mkubwa wa nchi hizo. Baada ya kubainika makubaliano hayo ya kugawana mataifa ya Waislamu, kuliibuka mapinduzi makubwa katika maeneo yote ya Iraq. Aidha baada ya Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Shirazi kutoa fatwa ya jihadi, raia wa nchi hiyo walisimama kukabiliana na ukoloni huo wa Uingereza dhidi ya nchi yao, hata hivyo kutokana na uungaji mkono mkubwa wa madola ya kikoloni ya Magharibi kwa Uingereza na kadhalika njama mbalimbali za adui, mapinduzi hayo ya wananchi hayakuweza kufikia malengo yake makuu na badala yake Faisal Hussein akateuliwa kuwa mfalme wa Iraq.

Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Shirazi

 

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Jenerali Omar Hassan Ahmad Al Bashir wa Sudan aliongoza mapinduzi ya kijeshi yasiyo ya umwagaji damu dhidi ya utawala wa Swadiq Al Mahdi, uliokuwa ukikabiliwa na matatizo ya ndani. Baada ya mapinduzi hayo Omar Hassan Al Bashir kwa kushirikiana na Hassan Al Turabi alianzisha chama cha Congress ya Kitaifa huku akiwa mwenyekiti wa chama hicho na rais wa nchi. Baada ya Al Bashir kutwaa urais alijitahidi kujitenga na siasa za Marekani, hatua ambayo iliipelekea serikali ya Washington kuichukia serikali ya Khartoum na kuanzisha hatua za kiaduai dhidi ya Al Bashir. Miongoni mwa hatua hizo ni kuwaunga mkono waasi wa Kusini mwa Sudan ambapo mwaka 2011 eneo hilo la kusini lilijitenga na Sudan na kujitangazia uhuru wake. Hatimaye rais huyo wa muda mrefu wa Sudan aliondolewa madarakani tarehe 11 Aprili 2019 kupitia mapinduzi ya kijeshi kufuatia maandamano ya miezi minne ya wananchi dhidi yake.

Jenerali Omar Hassan Ahmad Al Bashir wa Sudan

 

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, yaani sawa na tarehe 30 Juni 1960, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaani Zaire ya zamani ilitangaza uhuru wake na Joseph Kasa-Vubu akachaguliwa kuwa Rais, huku Patrice Lumumba akichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, kabla ya uhuru, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilikuwa ikikoloniwa na Wabelgiji. Mapambano ya wapigania ukombozi wa Kongo chini ya uongozi wa mpigania uhuru mashuhuri wa Kiafrika Patrice Lumumba yalifikia kilele miaka kadhaa baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kupelekea kukombolewa Zaire ya zamani. Hata hivyo baada ya nchi hiyo kupata uhuru wake, serikali ya Ubelgiji ilihusika pakubwa katika kuzusha uasi nchini humo. Aidha ulijiri mzozo kati ya Lumumba na Moise Tshombe kibaraka aliyekuwa na uhusiano na wakoloni wa Kibelgiji na hivyo kuzidisha hali ya machafuko huko Zaire. Nchi hiyo ilizidi kuwategemea wageni baada ya kuuawa Lumumba na vibaraka wa ndani. Hatimaye Mobutu Seseseko alichukua madaraka katika mapinduzi ya mwaka 1965 kwa uungaji mkono wa Marekani na kuanza kuwakandamiza wananchi wa nchi hiyo.

Bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

 

Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, sawa na tarehe 9 Tir 1365 Hijria Shamsia, ilianza operesheni ya kijeshi ya Karbala -1 kwa ajili ya kukomboa mji wa Mehran huko magharibi mwa Iran uliokuwa umetwaliwa na jeshi vamizi la Saddam Hussein wa Iraq. Mji huo ulikaliwa kwa mabavu muda mfupi baada ya jeshi la Baath la Iraq kuvamia ardhi ya Iran Septemba 1981 na ulikombolewa na wapiganaji shupavu wa Iran katika operesheni makini ya Karbala-1.

operesheni ya kijeshi ya Karbala -1

 

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita yaani mwaka 1991 Milaadia, mfumo wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ulimalizika. Kuanzia mwaka 1948, watu weupe walio wachache walianza kutekeleza siasa za kibaguzi dhidi ya wazalendo weusi. Kwa mujibu wa siasa hizo, weupe hao waliounda asilimia 20 tu ya wananchi wote wa Afrika Kusini walijiona kuwa bora kuwaliko wenzao weusi na hivyo  kuhodhi nafasi zote muhimu za utawala nchini humo. Sheria za kibaguzi kama vile za kupiga marufuku watu weusi kuoana na watu weupe na kuzuiwa wazalendo kushiriki katika harakati za kisiasa ni baadhi tu ya sheria za kibaguzi zilizotekelezwa na makaburu nchini Afrika Kusini. Siasa hizo ziliwakasirisha sana walimwengu suala lililopelekea nchi nyingi duniani kukata uhusiano na utawala huo wa kibaguzi.

Nelson Mandela, mkombozi wa Afrika Kusini

 

Tags