Jul 26, 2021 02:36 UTC
  • Jumatatu tarehe 26 Julai 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 15 Mfunguo Tatu Dhulhija 1442 Hijria sawa na Julai 26 mwaka 2021

Siku kama ya leo miaka 1227 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Ali Naqi (AS) mashuhuri kwa lakabu ya al-Hadi, mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW, katika mji mtakatifu wa Madina. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Jawad AS, Imam Hadi alichukua jukumu zito la Uimamu na kuongoza Umma wa Kiislamu. Zama za Uimamu wake zilisadifiana na kipindi cha utawala wa ukoo wa Bani Abbas, na Mutawakkil ndiye aliyekuwa ameshika hatamu za uongozi wakati huo. Baada ya mtawala huyo kuhisi kuwa Imam Hadi (as) na wafuasi wake walikuwa hatari kwa utawala wake, aliamrisha Imam atolewe Madina na kuhamishiwa Samarra, Iraq ili amuweke chini ya uangalizi. Licha ya hayo yote, lakini Imam Naqi aliendelea kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 174 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Liberia ilipata uhuru. Liberia iko katika mwambao wa bahari ya Atlantic na inapakana na nchi za Guinea, Sierra Leone na Ivory Coast. Idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo yenye jumla ya karibu watu milioni tano wanafuata dini za kijadi na kimila na asilimia 16 ya raia wake inaundwa na Waislamu. Lugha rasmi ya raia wa Liberia ni Kingereza. Liberia iliundwa mwaka 1822 kwa ajili ya Waafrika waliokuwa watumwa huko Marekani. Mwaka 1841 nchi hiyo iliandika katiba na kupewa jina la Liberia lenye maana ya ardhi ya watu huru. 

Bendera ya Liberia

Katika siku kama ya leo miaka 165 iliyopita, George Bernard Shaw mwandishi, muigizaji wa michezo ya kuchekesha na mkosoaji wa Ki-Ireland alizaliwa katika mji wa Dublin. Baba yake alikuwa mtumishi wa serikali. Akiwa katika rika la kuinukia George Bernard alianza kuandika visa na tamthiliya. Alijitahidi kutoa taswira ya matatizo ya kijamii katika visa vyake. 1925 Shaw alitunukiwa tuzo ya nobel ya fasihi. 

George Bernard Shaw

Miaka 65 iliyopita katika siku kama ya leo, Gamal Abdul-Nasser rais wa wakati huo wa Misri aliitangaza kuutaifisha Mfereji wa Suez. Mfereji huo ulianzishwa mwaka 1896 baada ya Misri kukaliwa kwa mabavu na Uingereza na kwa utaratibu huo, njia ya baharini baina ya Ulaya na Asia ikawa imefupishwa. Udhibiti wa Uingereza na Ufaransa kwa Mfereji wa Suez uliendelea hadi serikali ya Abdul-Nasser ilipokuja kuutaifisha na kuutangaza kuwa mali ya taifa. Hatua hiyo ilifuatiwa na mashambulio ya kijeshi ya Uingereza, Ufaransa na utawala dhalimu wa Israel. Hata hivyo mashinikizo ya kimataifa dhidi ya madola vamizi na mapambano ya wananchi Waislamu wa Misri, yalivifanya vikosi vamizi viondoke katika kanali hiyo muhimu na mfereji huo ukawa katika miliki ya serikali na taifa la Misri. 

Gamal Abdul-Nasser

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, visiwa vya Maldives huko kusini mwa bara Asia vilipata uhuru. Visiwa vya Maldives vilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Wareno mwanzoni mwa karne ya 16. Visiwa hivyo baadaye vilidhibitiwa na Waholanzi na Wafaransa na hatimaye mwishoni mwa karne ya 19, vikakaliwa na Waingereza. 

Bendera ya Maldives

 

Tags