Sep 03, 2021 02:32 UTC
  • Ijumaa tarehe 3 Septemba 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 25 Muharram 1443 Hijria sawa na Septemba 3 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1348 iliyopita, yaani tarehe 25 Muharram mwaka 95 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, alifariki dunia Imam Ali bin Hussein, maarufu kwa lakabu ya Imam Sajjad au Imam Zainul-Abidin, mtoto wa Imam Hussein bin Ali (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (swa). Imam Zainul Abidini alifariki dunia mjini Madina akiwa na umri wa miaka 38. Baada ya mapambano makubwa ya baba yake katika jangwa la Karbala, Iraq Imam Sajjad alikuwa na jukumu zito la kufikisha ujumbe wa mwendelezo wa malengo ya baba yake, Imam Hussein (as). Imam Sajjad alifanya juhudi kubwa za kufundisha utamaduni wa Kiislamu na kueneza mafundisho bora ya Qur'ani na Suna za Mtume Muhammad (saw), jambo ambalo lilikuwa sababu ya kubakishwa hai Qur'ani na Suna za Mtume. Imam Zainul-Abidin alifahamika kwa uchamungu mkubwa na alikuwa mwingi wa kusujudu na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya 'Sajjad' ikiwa na maana ya mtu mwenye kusujudu sana.

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita aliuawa shahidi Rais Ali Delvari, kiongozi wa mapambano dhidi ya uvamizi wa Uingereza huko kusini mwa Iran. Manzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia vikosi vya majeshi ya Urusi kutokea kaskazini na majeshi ya Uingereza kutokea kusini viliazimia kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran. Wakati huo Rais Ali Delvari alitoa wito kwa wananchi kukabiliana na wavamizi wa Uingereza kwa kutegemea fatua ya vita vya jihadi iliyokuwa imetolewa na maulama wa Kiislamu ya ulazima wa kulinda nchi mbele ya maadui. Rais Ali Delvari na wapiganaji wenzake shupavu walikabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya majeshi yaliyokuwa yamejizatiti kwa silaha na kuzuia kutekwa mji wa Busher. Mapambano ya wananchi wa Tengestan karibu na mji wa kuisni wma Iran wa Busher dhidi ya majeshi vamizi ya Uingereza yaliendelea kwa kipindi cha miaka 7. 

ais Ali Delvari

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, Damascus mji mkongwe na wa kihistoria wa Kiislamu ulikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Uingereza. Moja kati ya malengo makuu ya serikali za Ulaya wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia ilikuwa kuugawa utawala wa Othmania, lengo ambalo baadaye lilifanikiwa. Wakati utawala wa Othmania ulipokuwa ukigawanywa, maeneo yaliyokuwa chini ya utawala huo, nayo moja baada ya jingine yalidhibitiwa na Ufaransa na Uingereza, ambapo mji wa Damascus katika Syria ya leo, pia ulishambuliwa na katika siku kama ya leo ukakaliwa kwa mabavu. Hata hivyo kwa mujibu wa makubaliano ya hapo kabla kati ya London na Paris, Syria ukiwemo mji mkuu wake, Damascus, ilidhibitiwa na Ufaransa.

Haram ya Hazrat Zainab (as) katika mji wa Damascus

Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufaransa na Uingereza ziliitangazia vita Ujerumani na kwa utaratibu huo Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikaanza. Baada ya jeshi la Ujerumani kuishambulia Poland, serikali ya Uingereza iliitumia Ujerumani ujumbe ikiitaka iondoke haraka katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu ya Poland. Hata hivyo Ujerumani ilipuuza takwa hilo la Uingereza. Baadaye Uingereza iliipatia Ujerumani makataa ya kuhitimisha operesheni zake za kijeshi. Hata hivyo Adolph Hitler kiongozi wa wakati huo wa Ujerumani ya Kinazi alikataa kutekeleza takwa hilo. Hatimaye katika siku kama ya leo, Uingereza na Ufaransa zikaitangazia vita Ujerumani. Sio Adolph Hitler pekee ambaye hakutaraji kama Ufaransa na Uingereza zingeingia vitani kwa ajili ya Poland bali hata Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti pia hakutarajia hilo.

Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, mkataba wa kusalimu amri Italia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ulitiwa saini baina ya wawakilishi wa Italia na nchi waitifaki. Kwa mujibu wa mkataba huo, Waziri Mkuu wa Italia alikubali bila masharti kusalimu amri nchi yake na kwa utaratibu huo, mmoja wa waitifaki muhimu wa Ujerumani ya Kinazi katika vita hivyo, akawa ameondoka katika medani ya vita.

Benito Mussolini

Miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Qatar ilipata uhuru toka kwa mkoloni Mwingereza. Qatar iliwahi kudhibitiwa na Ufalme wa Othmania. Hata hivyo kufuatia kudhoofika utawala huo, Qatar ambayo kuanzia mwaka 1882 na kuendelea kivitendo ilikuwa ikiendeshwa na Uingereza, mwaka 1916 nchi hiyo ya Kiarabu ikawa imetambuliwa rasmi kuwa koloni la Muingereza. Hadi mwaka 1971 Qatar ilikuwa bado inakoloniwa na Uingereza ambapo mwaka huo huo, kwa ushirikiano wa viongozi wa eneo la pambizoni mwa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, likaundwa Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu. Hata hivyo mnamo Septemba mwaka huo huo, yaani 1971, Qatar ilijiondoa katika Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu na kujitangazia uhuru.