Alkhamisi, Septemba 30, 2021
Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Mfunguo Tano Safar 1443 Hijria sawa na Septemba 30 mwaka 2021 Milaadia.
Leo tarehe 8 mwezi Mehr kwa mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi Jalaluddin Muhammad bin Bahauddin maarufu kwa jina la Maulawi, arifu na mshairi mkubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 604 Hijiria Shamsia katika mji wa Balkhi ambao zama hizo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran baada ya muda akahamia katika mji wa Konya nchini Uturuki akiandamana na baba yake na baadaye kuelekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu. Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maanawi, Fihi ma Fihi, Maktubat Maulana na Rubaiyat. Jalaluddin Rumi alifariki dunia tarehe 5 Jamadul Thani mwaka 672 akiwa na umri wa miaka 68 na kuzikwa katika mji wa Konya nchini Ituruki.
Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita kulifanyika mkutano wa kihistoria wa Munich huko Ujerumani. Mkutano huo uliwakutanisha pamoja viongozi wa Ujerumani Adolph Hitler, kiongozi wa Italia Benito Mussolini na mawaziri wakuu wa wakati huo wa Uingereza na Ufaransa. Lengo la mkutano huo lilikuwa kutafuta njia ya kutatua hitilafu za Ujerumani na Czechoslovakia. Matokeo ya mkutano huo yalikuwa kumegwa sehemu ya ardhi ya Czechoslovakia na kuunganishwa na Ujerumani. Mkataba huo ulikuwa na taathira kubwa katika matukio ya baadaye barani Ulaya na ulidhihirisha zaidi sura na tabia ya kikoloni ya nchi za Magharibi. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa Ujerumani hapo mwaka 1945, Czechoslovakia ilichukua tena sehemu hiyo ya ardhi.
Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita nchi ya Botswana ilifanikiwa kujipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Mwaka 1885 Botswana iliwekwa katika himaya ya Uingereza. Mapambano ya wapigania uhuru nchini humo yalishadidi tangu mwaka 1920 na mwaka 1966 nchi hiyo ilipata uhuru. Botswana inapatikana kusini mwa bara la Afrika na inapakana na nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mitetemeko ya ardhi Charles Richter. Akishirikiana na mhakiki mwingine, Richter alipima mitetemeko hiyo kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko ya ardhi toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta. Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa mujibu wa athari ya nje ya kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika.
Leo tarehe 30 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Viziwi. Lengo la siku hii kupewa jina la Siku ya Kimataifa ya Viziwi ni kutaka kuimarisha utamaduni wa kuwa na mawasiliano ya watu wenye ulemavu huo, kustawisha maarifa ya lugha ya ishara na kuwazindua wanasiasa na watu wa kawaida kuhusu matatizo ya watu wa tabaka hilo.
