Oct 03, 2021 23:10 UTC
  • Jumatatu, Oktoba 4, 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 27 Mfunguo Tano Safar 1443 Hijria sawa na Oktoba 4 mwaka 2021 Milaadia

Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru wake. Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kufuatia Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo.

Bendera ya Ubelgiji

Katika siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, ilivumbuliwa dawa ya penicillin na tabibu Alexander Fleming. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu wa nchini Uingereza, alizaliwa tarehe sita Agosti mwaka 1881 katika familia ya wakulima huko magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasiwasi mkubwa. Miaka 10 baada ya kumalizika vita, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda.

Fleming. Fleming

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na wasomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikawa zimeanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputniki 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini.

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Serikali ya Kuwait ilimnyima Imam Khomeini idhini ya kuishi nchini humo na hivyo kulazimika kuelekea nchini Ufaransa. Hatua ya Imam kuelekea Paris, ilikuwa sababu ya kuharakisha mwenendo wa mafanikio ya Mapinduzi nchini Iran, kinyume kabisa na matarajio ya dikteta Saddam wa Iraq na Mohammad Reza Pahlavi, mfalme kibaraka wa wakati huo wa Iran ambao waliamini kwamba kwa kumbaidisha Imam Khomeini (MA) wangekuwa wameua harakati zake za kimapinduzi. Akiwa mjini Paris, Imam aliishi katika kijiji kilichoitwa Neauphle-le-Château, kilometa 50 kutoka mji huo, ambapo aliendeleza harakati zake za kimapinduzi kupitia barua na kanda za sauti kwa wanamapinduzi nchini Iran.

Imam Khomeini

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari mwanachuoni mashuhuri wa Iran. Ayatullah Sabzawari alizaliwa mwaka 1290 Hijiria Shamsia, katika mji huo uliopo kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanachuoni huyo alipata elimu ya msingi katika miji ya Sabzawar na Mash’had, na baadaye alielekea Najaf nchin Iraq na kupata elimu ya juu ya maarifa ya Kiislamu. Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari ameandika vitabu vingi na maarufu zaidi ni tafsiri ya Qur'ani ya ‘Mawaahibul-Rahman fii Tafsiril-Qur’an’ chenye juzuu 20, ‘Muhadh-Dhibul-Ahkaam fii Bayaanil-Halali wal-Haraam’ chenye juzuu 30 na ‘Tahdhibul-Usuul’ chenye juzuu mbili.